RAILA ODINGA NA GAVANA WA JIMBO LA KWALE NCHINI KENYA WACHAPWA KIBOKO MBELE YA HALAIKI
Hali ya taharuki iliibuka katika mkutano wa hadhara katika jimbo la Kwale nchini Kenya, baada ya mwanamume mmoja kwenda ukumbini na kuanza kumtandika viboko kiongozi wa upinzani Raila Odinga pamoja na wanasiasa wengine.
Raila alikuwa amejiunga na kikundi cha wanawake waliokuwa wanacheza ngoma ya kitamaduni kuwatumbuiza wageni, pamoja na gavana wa jimbo la Kwale Pwani ya Kenya Salim Mvuruya katika mkutano wa kisiasa.
Walikuwa wameambatana na viongozi wengine, wakiwemo, Seneta Juma Boy, Hassan Omar, Agnes Zani, James Orengo, Johnstone Muthama na wengineo.
Mwanamume huyo alimshambulia Odinga ambaye ni waziri mkuu wa zamani na kumchapa mara mbili kabla ya kumgeukia gavana wa jimbo hilo na pia kumchapa mara mbili. Hata hivyo mwanamume huyo alishindwa nguvu na walinzi wa Raila Odinga.
Polisi walithibitisha kuwa walimkamata mwanamume huyo na kumwachilia baada ya kugundua kuwa alikuwa na matatizo ya kiakili.
Haijulikani kwa nini mwanammume huyo alimshambulia Raila ila baadhi wanasema ni kwa sababu alighadhabishwa pale waziri mkuu alipocheza ngoma na mwanamke aliyesemekana kuwa mke wake ambaye alikuwa katika kikundi cha wanawake waliokuwa wanawatumbuiza wageni waheshimiwa.
Viongozi waliofika walilazimika kusitisha ngoma hiyo kabla ya mwanamume huyo kushindwa nguvu.
RAILA ODINGA NA GAVANA WA JIMBO LA KWALE NCHINI KENYA WACHAPWA KIBOKO MBELE YA HALAIKI
Reviewed by Zero Degree
on
10/01/2014 11:26:00 AM
Rating: