Magufuli atangazwa mshindi uchaguzi wa urais Tanzania
Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha CCM John Pombe Magufulindiye rais mteule wa taifa la Tanzania baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili.
Akitoa matokeo hayo mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa Magufuli alijipatia kura 8,882,935 ikiwa ni aslimia 58.46 huku mpinzani wake wa karibu Edward Lowassa wa chama cha Chadema akijipatia kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote.
Haya ndiyo matokeo kamili kama yalivyotangazwa na Jaji Lubuva:
Matokeo ya uchaguzi wa urais Tanzania | |||
---|---|---|---|
Jina | Chama | Kura | Asilimia |
Anna Mghwira | ACT | 98,763 | 0.65 |
Chifu Yemba | ADC | 66,049 | 0.43 |
John Magufuli | CCM | 8,882,935 | 58.46 |
Edward Lowassa | CHADEMA | 6,072,848 | 39.97 |
Hashim Spunda | CHAUMA | 49,256 | 0.32 |
Janken Kasambala | NRA | 8,028 | 0.05 |
Macmillan Lyimo | TLP | 8,198 | 0.05 |
Fahmi Dovutwa | UPDP | 7,785 | 0.05 |
Awali kabla ya kutolewa kwa matokeo hayo vyama vya siasa vilivyokubaliana na matokeo vilitia sahihi matokeo hayo. Lakini chama cha Chadema, chake Bw Lowassa hakikuwakilishwa. Chama hicho kimepinga matokeo hayo.
Akivihutubia vyombo vya habari mgombea wa urais kupitia chama hicho Edward Lowassa amepinga matokeo yoyote ya uchaguzi huo na kujitangaza mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 62 ya kura zilizopigwa.
Lowassa amedai kwamba tume ya uchaguzi nchini humo imeshirikiana na chama tawala CCM kufanya udanganyifu katika shughuli hiyo, madai ambayo tume hiyo imekanusha.
"Hatuna hata chembe ya wasiwasi kwamba mchakato huu ulifuata sheria na ni halali," alisema Jaji Lubuva muda mfupi kabla ya kutangaza matokeo.
Aidha, amesema tume iliendesha mchakato wote "bila shinikizo"
Akizungumzia kutoidhinishwa kwa matokeo hayo na wawakilishi wa Chadema, mkurugenzi wa uchaguzi katika tume Bw Ramadhan Kailima alisema sheria inawaruhusu kuendelea na kutangaza matokeo hata bila chama chochote kile kuwakilishwa au kuidhinisha matokeo husika.
Kwenye uchaguzi huo, kati ya wapiga kura 23,161,440 waliojiandikisha, ni 15,589,639 waliopiga kura, ambao ni asilimia 67.31 ya wapiga kura wote. Kura 402,248 ziliharibika.
Kufuatia kutangazwa kwa matokeo hayo, tume hiyo ya uchaguzi sasa inatarajiwa kumkabidhi Bw Magufuli cheti cha kuwa mshindi wa urais.
Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo, chama hicho kimeanza kusherehekea kwenye mtandao wa Twitter huku wafuasi wake nao wakianza kusherehekea katika barabara za miji.
Source: BBC
Magufuli atangazwa mshindi uchaguzi wa urais Tanzania
Reviewed by Zero Degree
on
10/29/2015 06:14:00 PM
Rating: