Aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alia kuchezewa rafu na NEC.
Matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa jimbo hilo yalikwama kutangazwa kwa siku kadhaa kutokana na kutokea mabishano kati ya Kafulila aliyekataa kura kuhesabiwa upya kwa madai kuwa maboksi yalilala polisi bila ya usimamizi, na Mwilima.
Baada ya mvutano huo, msimamizi wa uchaguzi alimtangaza mgombea huyo wa CCM kuwa mshindi kwa kupata kura 34,453, matokeo ambayo Kafulila, aliyetangazwa kupata kura 33,382, anayapinga mahakamani.
Jana, Kafulila amesema NEC inatupiana mpira kuhusu ombi lake la fomu za matokeo ya vituo vyote 382 vya kupigia kura vilivyopo katika jimbo hilo lenye kata 16 ili azitumie kama ushahidi mahakamani.
Kafulila, ambaye alijipatia umaarufu baada ya kuibua kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, alisema kwa nyakati tofauti ametoa malalamiko yake kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima na aliyekuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Andrea Majaliwa lakini hajafanikiwa kupata chochote.
Kafulila alisema katika kesi hiyo anaitaka mahakama ifanye majumuisho na kumtangaza mshindi kwa madai kuwa fomu namba 21B za matokeo ya vituo vyote, zinaonyesha amepata kura 34,212 dhidi ya kura 33,390 za Mwilima.
Anavyozungushwa.
Alisema Novemba 12, alimuandikia barua msimamizi wa uchaguzi wa jimbo, akitaka kupatiwa fomu ya majumuisho ya kura na kujibiwa kuwa tayari ilikuwa imetumwa makao makuu ya NEC jijini Dar es Salaam.
Alisema siku moja baadaye alimuandikia barua Kailima kuomba apatiwe fomu hizo kwa kuwa alijibiwa kuwa zimetumwa makao makuu ya tume hiyo.
“Zilipita siku 10 bila majibu. Novemba 24 nilionana na Kailima na alipewa maelekezo na (Jaji Damian Lubuva-Mwenyekiti Nec). Kailima alimpigia simu msimamizi msaidizi wa jimbo na kumtaka anipe fomu hizo kupitia kwa msaidizi wangu,” alisema Kafulila.
Alisema licha ya agizo hilo la Jaji Lubuva, mpaka sasa bado hajapewa fomu hizo na Mfune ambaye baada ya kuhamishwa halmashauri mpya, nafasi yake ilikaimiwa na Daniel Kamwela.
“Majaliwa yeye alishiriki mchakato mzima wa uchaguzi na Kamwela alikuwa mgeni tu pale. Nakumbuka Majaliwa alinijibu kuwa amepewa maelezo na Kailima ili anipatie zile fomu.”
“Alinieleza kuwa angenipatia baada ya siku tatu, majibu ambayo pia niliyapata kutoka kwa Kailima. Ilinishangaza, iweje waandae fomu wakati fomu hizo si za kuandaliwa na zipo tayari maana uchaguzi ushafanyika?” alihoji.
Alisema siku hizo zimepita na kila akikumbusha suala hilo kwa barua, hakuna majibu yoyote anayopewa na kudai kuwa kuna agizo limetolewa kwamba asipatiwe fomu za matokeo.
“Hivi sasa hata mikutano ya kushukuru wananchi nimezuiwa kufanya katika jimbo la Kigoma Kusini na hawataki kutoa fomu hizo kwa sababu wanajua kuwa matokeo yaliyotangazwa si sahihi,” alisema.
Alisema kuna “mchezo” umechezwa kuhakikisha anakwamishwa huku akitolea mfano kuhamishwa kwa Mfune, NEC kumzungusha na kupuuzwa kwa agizo la Kailima.
“Kinachonishangaza ni nguvu ya ushirikiano kupungua kutoka NEC. Kwa sasa hawataki kunisaidia na hawana ushirikiano kabisa,” alisema.
Kauli ya Nec
Akizungumzia suala hilo, Kailima alisema: “Kila mgombea au chama kiliweka wakala katika vituo vya kupigia kura, kuhesabia kura ambapo wakala au mgombea atapewa fomu namba 21B na katika kituo cha kujumlishia kura watapewa fomu namba 24B.
“Fomu hizo zina matokeo ya kila kituo na katika kituo cha kujumlisha kura zote. Mawakala wake (wa Kafulila) walipewa sasa anataka tumpe zipi? Kama amefungua kesi yeye awasilishe malalamiko yake na msimamizi atawasilisha huo ushahidi wake.”
Kailima alisema msimamizi wa uchaguzi hawezi kumpa ushahidi mlalamikaji na kama akifanya hivyo atakosa cha kuwasilisha mahakamani.
“Kama hakuweka mawakala siyo jukumu la NEC, lilikuwa jukumu lake yeye na chama chake,” alisema.
Kailima alisema suala hilo linaweza kufafanuliwa kwa kina na msimamizi wa uchaguzi aliyekuwepo katika uchaguzi huo, utangazaji wa matokeo.
Gazeti hili lilipowasiliana na Majaliwa hakukubali wala kukataa kuhusu suala hilo, akidai kuwa yeye si mhusika.
Aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alia kuchezewa rafu na NEC.
Reviewed by Zero Degree
on
12/28/2015 03:15:00 PM
Rating: