Baraza dogo la Dk Magufuli laokoa bilioni 23!!!
Kiasi hicho cha fedha kingetumika katika kipindi cha miaka mitano kwa ajili ya kuwalipa mishahara mawaziri hao 21, kuwanunulia magari (mashangingi) sambamba na gharama zake za mafuta na matengenezo na kodi ya nyumba katika kipindi cha miaka mitano.
Mahitaji hayo yote, kwa mujibu wa tathmini ya gazeti hili kwa kufuata gharama za msingi, ni Sh260.8 milioni kwa mwezi ambazo kwa miaka mitano zingefikia Sh20.9 bilioni kama yasingetokea mabadiliko yoyote mbeleni.
Fedha hizo pia zinajumuisha Sh2 bilioni za semina elekezi kwa mawaziri wapya ambayo Dk Magufuli aliifuta na kusema kuwa kiasi hicho kinaweza kutumika kufanyika shughuli nyingine.
Idadi hiyo ya mawaziri inatokana na Rais huyo wa Awamu ya Tano kupunguza wizara kutoka 30 za Serikali iliyopita hadi 18.
Mpaka Rais mstaafu Jakaya Kikwete anaondoka madarakani Novemba 5, mwaka huu baraza lake la mawaziri lilikuwa na mawaziri 55.
Rais Dk Magufuli amefanya uteuzi huo siku ya 35 tangu alipoapishwa, ikilinganishwa na mabaraza ya kwanza ya marais waliomtangulia tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.
Kutokana na ahadi zake alizokuwa akizitoa wakati wa kampeni, jambo ambalo halikutarajiwa ni Rais huyo kuteua mawaziri, idadi sawa na alioanza nao mtangulizi wake (Kikwete), ambaye alivunja rekodi ya kuunda Baraza kubwa kuliko marais wote waliomtangulia tangu Uhuru.
Baraza hilo alilounda Kikwete mwaka 2005 baada ya kuingia madarakani, lilikuwa na mawaziri 60, kati yao 29 walikuwa naibu mawaziri kamili na 31 naibu mawaziri.
Kinyume chake, Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ndiyo iliyovunja rekodi ya kuwa na Baraza dogo la mawaziri 11 mwaka 1961.
Katika awamu ya pili mwaka 1985, Rais Ali Hassan Mwinyi alipoingia madarakani aliunda Baraza la Mawaziri lenye mawaziri 23 na manaibu wanane, jumla walikuwa 31.
Mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa alianza na mawaziri 27 na naibu mawaziri 10, jumla walikuwa 37 ambao aliwabatiza jina la askari la miamvuli.
Matumizi Sh22.9bilioni
Hivi karibuni, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole-Medeye alisema mshahara wa mawaziri hautofautiani na wabunge ambao ni Sh3.8 milioni kwa mwezi.
Kama Rais Magufuli angeongeza idadi ya mawaziri 21 katika baraza lake, wangeongeza mzigo wa bajeti ya mishahara kwa Sh79.8 milioni kila mwezi mbali na posho mbalimbali.
Idadi ya magari ambayo hutumiwa na mawaziri nayo imepungua na kufikia 34 kutoka 55.
Kwa kawaida mawaziri hutumia magari ya kifahari ambayo mara nyingi huwa Toyota Landcruiser matoleo ya mfululizo wa 200 ama VX V8 au GX V8.
Bei ya sokoni ya magari hayo kwa sasa ni wastani wa Dola za Marekani 119,000 (Sh250 milioni) kwa gari moja.
Kwa mantiki hiyo, Serikali itaokoa Sh5.25 bilioni kwa miaka mitano katika ununuzi wa magari hayo yajulikanayo kama mashangingi iwapo Dk Magufuli ataruhusu mawaziri wake wanunuliwe magari hayo.
Ukiachana na gharama za ununuzi wa magari ambazo ni za mara moja, vifaa hivyo vya moto huitaji matengenezo.
Mapema mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Adelhelm Meru alisema kuwa magari hayo hufanyiwa matengenezo kila baada ya kilomita 5,000 na kulipiwa wastani wa Sh1.8 milioni.
Hii inamaanisha kuwa mashangingi 21 ya mawaziri waliopunguzwa kutoka kwenye baraza la Serikali iliyopita, wangetumia 37.8 milioni kila mwezi.
Kwa kuwa katika utawala wa ‘hapa kazi tu’ viongozi wanatakiwa kutembelea zaidi wananchi vijijini, bila shaka viongozi hao wangekuwa wanazimaliza kilomita 5,000 kila mwezi na magari kuhitaji matengenezo lakini sasa gharama hizo hazipo tena.
Pia, mashangingi hutumia mafuta mengi kufanikisha safari. Taarifa zilizopo ni kwamba kila waziri hupatiwa lita 1,000 za mafuta kwa mwezi hivyo mawaziri 21 waliopunguzwa iwapo wangekuwepo wangetumia lita 21,000.
Bei elekezi ya sasa ya mafuta ya dizeli jijini Dar es Salaam kama ilivyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) Desemba, 2 ni Sh1, 823 kwa lita. Kuhakikisha kuwa mashangingi hayaishiwi mafuta, Serikali ingetakiwa kutoa Sh38.28 milioni.
Mawaziri kama watumishi wengine Serikali hutakiwa kupatiwa stahiki za msingi kama Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma toleo la mwaka 2009 na marebisho yake ya 2011 linavyoainisha na nyumba ni moja ya huduma wanazotakiwa kupatiwa.
Mara nyingi Serikali huwapatia nyumba mawaziri hao huku baadhi wakikataa na kukaa kwenye nyumba zao binafsi kama alivyoeleza Dk Meru.
Sehemu kubwa ya nyumba hizo za Serikali, ambazo humilikiwa na Wakala wa Nyumba za Serikali (TBA), zipo maeneo ya ya Mikocheni, Oysterbay na Masaki ambako thamani ya nyumba ipo juu ikilinganishwa na baadhi ya maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam.
Wastani wa bei ya kukodisha nyumba yenye hadhi ya wastani kwa waziri kwa mwezi katika maeneo hayo kwa mujibu wa bei zilizopo kwenye mtandao wa ukodishaji na uuzaji nyumba wa Lamudi ni Sh5 milioni.
Hivyo, nyumba ambazo wangekaa mawaziri 21 ambao wamepunguzwa zingegharimu Sh105 milioni kwa mwezi iwapo zingekuwa zinakodishwa kwa watu binafsi lakini fedha hizo tayari zimeokolewa na Rais Dk Magufuli.
Hata hivyo, Ole-Medeye alisema mawaziri hupatiwa Sh800,000 kwa ajili ya gharama za makazi, mawasiliano na ankara nyingine zinazohusiana na nyumba hata kwa wale wanaokaa katika nyumba zao binafsi kiasi alichosema ni kidogo.
Alisema kwa sasa nyumba ya hadhi ya waziri gharama za kukodisha kwa mwezi ni wastani wa Dola za Marekani 3,000 ambazo ni zaidi ya Sh6 milioni.
Baraza dogo la Dk Magufuli laokoa bilioni 23!!!
Reviewed by Zero Degree
on
12/11/2015 10:48:00 AM
Rating: