Loading...

Dar es salaam: Pinda amkabidhi mikoba Majaliwa!!!



Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda amekabidhi ofisi kwa Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa huku akimtaka kufuatilia kwa karibu maelekezo anayoyatoa kwenda ngazi za chini. Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika Dar es Salaam jana, Pinda alisema katika kipindi cha uongozi wake kulikuwa na ucheleweshaji wa kupata majibu kutoka ngazi ya chini katika maelekezo aliyokuwa akitoa.

“Ofisi ya Waziri Mkuu ni kubwa na ina mambo mengi ya kufuatilia. Itabidi uwe makini sana katika kufuatilia hili,” alisema.

Pinda alimtaka Majaliwa ahakikishe kila idara inakuwa na mpango kazi wake na kufuatilia kila kilichopangwa.

Vilevile, alimkabidhi taarifa yenye kurasa 104 inayoelezea majukumu mbalimbali ya taasisi na idara zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Ofisi ya Waziri Mkuu ina taasisi nane, idara nane na vitengo saba.

Taasisi hizo ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).

Nyingine ni Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Idara zilizopo kwenye ofisi hiyo ni Utawala na Rasilimali Watu, Sera na Mipango, Uratibu wa Maadhimisho ya Kitaifa na Sekta Binafsi na Uwezeshaji.

Nyingine ni Bunge na Siasa, Uratibu wa shughuli za Serikali, Mpigachapa Mkuu wa Serikali na Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu.

Pinda alisema pia ameridhishwa na kasi ya utendaji kazi wa Rais John Magufuli na Waziri Mkuu huyo waliyoanza nayo na ana imani wataivusha Tanzania na kuifikisha kwenye uchumi wa kati.

Kwa upande wake Majaliwa alimshukuru Pinda na kuahidi kutekeleza yote yaliyomo kwenye taarifa aliyomkabidhi.

Pia, aliahidi kusimamia kwa karibu suala la ufuatiliaji wa maelekezo anayotoa pamoja na yale yanayotoka ngazi za juu.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka, Naibu Katibu Mkuu (OWM), Regina Kikuli, wakuu wa taasisi zote nane, wakuu wa idara na vitengo vya ofisi hiyo na wasaidizi wa Waziri Mkuu waliopo katika ofisi yake.




Mshirikishe na mwenzako kuhusiana na habari hii!!
Dar es salaam: Pinda amkabidhi mikoba Majaliwa!!! Dar es salaam: Pinda amkabidhi mikoba Majaliwa!!! Reviewed by Zero Degree on 12/02/2015 11:59:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.