Loading...

Ijue SIRI ya Raisi John Pombe Magufuli kuweka kiporo wizara 4 nyeti!!!

Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais John Magufuli kuweka kiporo wizara nne nyeti alipotangaza Baraza la Mawaziri linaloapishwa leo Ikulu bila kuteua mawaziri umeibua hisia ambazo zinajibiwa na wasomi, wachambuzi kama mkakati mahsusi wa kiongozi huyo kutaka zitimize wajibu wake ipasavyo.
Juzi, Rais Magufuli alisema bado anazifanyia kazi, lakini aliteua naibu mawaziri wa kuziongoza wizara hizo ambazo ni; Maliasili na Utalii iliyokuwa chini ya Lazaro Nyalandu, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyounganishwa zile za Uchukuzi, Mawasiliano, Fedha na Mipango na Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ufundi.

Wizara ya Uchukuzi iliyokuwa chini ya Samuel Sitta, Ujenzi Dk Magufuli, Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, Fedha, Saada Mkuya na Elimu, Dk Shukuru Kawambwa.

Hiyo ni mara ya kwanza katika historia ya uteuzi wa mawaziri nchini, Rais kuanza na uteuzi wa naibu mawaziri na kusubiri uteuzi wa waziri kamili katika wizara anazoziunda.

Juzi, wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya uteuzi huo, Rais Magufuli alisema: “nimeamua kuanza na mawaziri 14, ambao tayari nimeshawapangia wizara, hizo wizara nne nitateua mawaziri wake baadaye, nawatafuta, lakini sijawapata bado.”

Akizungumzia hatua hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana kuwa uteuzi wa mawaziri ni suala la Rais ambaye ameshasema kuwa akiwa tayari atajaza nafasi za wizara zilizobaki.

“Siwezi kumzungumzia Rais, unajua yeye anafanya uteuzi wa timu yake, anateua kulingana na vile anavyoona inafaa, lakini ameteua naibu mawaziri ambao watafanya kazi kwenye wizara ambazo hazina mawaziri hadi uteuzi mwingine utakapofanyika,” alisema.

Maliasili na Utalii

Wizara hiyo imeachwa kiporo, ni wazi kutokana na unyeti wake na kwamba inahitaji kuwa na waziri makini, mzalendo na mwenye mipango ya kuinua utalii na kulinda maliasili.
Wizara hiyo ni miongoni mwa wizara zilizoongozwa na mawaziri 11 katika miaka 25 na tangu mwaka 1988 ni waziri mmoja, Zakhia Meghji aliyedumu kwa muda mrefu, akiiongoza kwa miaka minane kuanzia 1997 hadi 2005.

Kumbukumbu zinaonyesha pia kuwa awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, ilitia fora kwa kubadili mawaziri wa wizara hiyo kwani tangu mwaka 2005, imeongozwa na mawaziri watano tofauti na awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, iliongozwa na mawaziri wawili.

Wafuatiliaji wa mambo ya siasa wanaamini kutodumu huko kunatokana na mapato makubwa yanayotokana na rasilimali kama za utalii na uwindaji, ambavyo vimesababisha kuwapo kwa tuhuma nyingi za rushwa na ufisadi.

Kashfa nyingi katika wizara hiyo zimeitikisa Serikali mara nyingi kama ile ya uuzaji wa pori la Loliondo, hoteli wa kitalii zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali kwa bei ya kutupa, vitalu vya viwanja na biashara ya pembe za ndovu na vipusa.

Wasemavyo wachambuzi
Dk Benson Bana, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema nia aibu kuona madudu kwenye wizara hiyo hayaishi wakati kuna viongozi wanaoisimamia.

Alibainisha kuwa kila Mtanzania anajua ina uwezo wa kuliingizia Taifa kipato kikubwa, lakini imekuwa ikisuasua na kuingiza mapato kidogo.

Alisema umuhimu wa wizara hiyo ndiyo ambao umekuwa ukisababisha baadhi ya mawaziri wanaoteuliwa kutodumu kwa muda mrefu, jambo linalompa wakati mgumu Rais Magufuli kufanya uteuzi.

“Ni wizara muhimu kwa uchumi wa taifa, inashangaza kuona hailiingizii taifa mapato yanayokusudiwa wakati tumezungukwa na maliasili nyingi ikiwamo milima, hifadhi za taifa, wanyama wa kila aina na misitu mingi,” alisema Bana.

Naye Richard Mbunda, kutoka chuo hicho aliliambia Mwananchi kuwa, ikiwa atapatikana waziri makini wizara hiyo ina uwezo wa kuliingizia Taifa pato kubwa litakalochangia kuinua uchumi.

“Kwa hali ilivyo ni lazima Rais ajiridhishe mtu gani atakayemteua aiongoze wizara hii ambayo nina uhakika inaweza kusaidia kasi ya uchumi wananchi,” alisema.

Alisema ni matarajio yake kuwa waziri atakayepewa ridhaa ya kusimamia sekta hiyo atafumua mifumo mibovu iliyochangia kulisababishia Taifa hasara kubwa.

“Haiingii akilini, Twiga wanatoroshwa wakati waziri husika yupo, ni lazima Rais Magufuli alivalie njuga jambo hili kwa kutuletea mtu makini. Hata masuala ya kutunza utamaduni wetu yanaweza kupewa kipaumbele yakatuletea watalii wengi, tunataka mipango kwenye wizara hii,” alisema.

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ni kati ya wizara nyeti zinazotakiwa kuwa na mtu makini wa kuimamia. Wizara hiyo itakuwa na majukumu yale yale ya kusimamia na kuhakikisha wakala, anawajibika kwa matengenezo na maendeleo ya barabara kuu na mitandao ya barabara za mikoa Tanzania Bara.

Mtandao wa barabara unakadiriwa kuwa na urefu wa kilometa 86,472, kutokana na Sheria ya Barabara ya mwaka 2007. Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) inasimamia mtandao wa kitaifa wa barabara wenye kilometa 33,891, ukihusisha kilometa12,786 za barabara kuu na kilometa 21,105 za barabara za mikoa.

Mtandao uliobaki wa kilometa 53,460 za mijini, wilaya na barabara zinazoiingia barabara kuu, ambazo nyingi ziko chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Changamoto kubwa katika wizara ya Ujenzi ni ufuatiliaji wa miradi kwa makandarasi, utoaji wa zabuni za barabara pamoja na malipo, usimamizi wa ufanisi kazi za bodi za makandarasi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Kwa upande wa Uchukuzi, waziri wa wizara hiyo atakuwa na kazi ya kuhakikisha anaendeleza kufukua madudu yaliyoko kwenye eneo hilo kama ilivyobainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akifukua uvundo ndani ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, TPA ikiwamo upotevu wa makontena 2,431 pamoja na 329 ya kukwepa kodi.

Mbali na TPA, maeneo mengi yana kazi kubwa kufuatilia ikiwamo ufanisi wa Kampuni ya Reli ya TRL, Tazara, ATCL, Sumatra. Katika eneo la mawasiliano, waziri husika atakuwa na changamoto ya kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na kwamba wakati wa sasa ni wa sayansi na teknolojia, hivyo kuharakisha miundombinu mbalimbali ya mawasiliano.

Wasomi wanena
Mhadhiri wa UDSM, Richard Mbunda alisema mtazamo wa walio wengi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inabeba taswira ya Rais Magufuli kwa kuwa ametumikia kwa muda mrefu hivyo anafahamu upungufu na madudu mengi yaliyopo.

Alisema licha ya kuwa ni wizara nyeti, katika maeneo mengi ndiyo iliyokibeba chama tawala katika Uchaguzi Mkuu kutokana na umahiri aliokuwa nao Dk Magufuli kwa kuisimamia ipasavyo na utendaji wake imekuwa ni ngumu kumpata kiongozi atakayevaa viatu vyake.

Mbunda alisema kwa upande wa mawasiliano kuna upungufu mwingi ikiwamo kufa kwa kampuni ya TTCL, hivyo bado anakuna kichwa kuhakikisha atakayempata ataweza kufufua makampuni hayo.

“Ni wizara nyeti, inachukua fedha nyingi na ndiyo wizara iliyojaa rushwa, utendaji mbovu, asilimia 10, makandarasi kujenga barabara chini ya kiwango ni wizara ngumu sana, ndiyo maana hata katika masuala ya uchukuzi ameanza kusafisha kwanza TRA ili hata atakayemuweka afuate nyayo zake aendane na kasi yake,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria nchini (OUT), Hamad Salim alisema kuchelewa kuteuliwa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inaonyesha taswira namna Dk Magufuli anavyohangaika kumpata mtu atakayefaa na atakayekuwa mtendaji na si kuandikiwa ripoti na Makatibu na kwenda kuzisoma bungeni.

“Kuna unyeti wake katika wizara hii tena mkubwa, ndiyo maana katika kipindi alichokuwa akiandaa baraza lake alikuwa akiendelea kusafisha Uchukuzi, ili hata akayemteua ajue anakwenda kufanya nini ni wizara ngumu na ndiyo sababu hata mawaziri wake wamekuwa wakibadilishwa mara kwa mara ndiyo kitovu cha uchumi wa nchi,” alisema Hamadi Salim.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Patrick Myovela alisema kutokana na umuhimu wa wizara hiyo, Waziri atakayeteuliwa lazima afanye kazi kwa kiwango kinachomzidi Rais Magufuli.

“Amefanya vizuri kujipa muda wa kutafakari na kumchunguza Waziri atakayetosha kwenye nafasi hiyo kabla ya kufanya uteuzi. Hii ni wizara nyeti ambayo kusipokuwa na mipango itahatarisha ustawi wa uchumi,” alisema.

Alisema changamoto pekee atakayokabiliana nayo waziri atakayopewa dhamana ya kuendesha wizara hiyo, ni jinsi atakavyoweza kufikia kiwango cha Rais Magufuli ambaye kwa muda mrefu aliitumikia wizara hiyo.

Wizara ya Fedha na Mipango
Baada ya kuapishwa, Rais Magufuli alitembea kwa miguu hadi Wizara ya Fedha, ikiwa ni ziara ya kushtukiza ili kuangalia utendaji kazi wa wizara hiyo kutokana na unyeti wake. Katika utawala wa awamu zilizopita, wizara hiyo haikuunganishwa na Mipango, badala yake iliitwa Wizara ya Fedha.
Rais Magufuli, anasubiri kupata mtu makini mwenye dhamana ya kusimamia wizara hiyo, yenye vitengo muhimu kikiwamo cha Hazina, Benki Kuu Tanzania (BoT)na Mamlaka ya Mapato ndani ya wizara hiyo. Kwa maana nyingine, Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo ‘mkoba’ wa Taifa unaobeba jukumu la kusimamia uchumi.

Tangu uhuru, mawaziri wa wizara hiyo walikuwa wakibadilishwa mara kwa mara kila wanapoteuliwa, wakiwamo walioambulia mwaka mmoja, kutokana na unyeti wake. Waziri wa Fedha wa kwanza kuteuliwa baada ya Uhuru wakati wa Mwalimu Julius Nyerere alikuwa Paul Bomani aliyeongoza mwaka 1966-1972, akafuatiwa na Cleopa Msuya, Amir Jamal, Edwin Mtei na baadaye Kighoma Malima.

Katika awamu ya pili ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwingi, mawaziri wa Fedha waliosimamia wizara hiyo ni Cleopa Msuya, Stephen Kibona, Kighoma Malima kwa mara nyingine na kumaliziwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Miaka kumi ya uongozi wa awamu ya tatu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, wizara hiyo ilishikiliwa na mawaziri watatu ambao ni Profesa Simon Mbilinyi, Daniel Yona na Basil Mramba.

Mramba na Yona wanatumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kukutwa na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.

Mawaziri hao walidaiwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni iliyopata zabuni ya ukaguzi wa madini ya dhahabu.

Hukumu iliyowatia hatiani ni ya wajumbe wawili kati ya jopo la mahakimu watatu, ambao ni Jaji Sam Rumanyika aliyeanza kusikiliza kesi hiyo kabla ya kuapishwa kuwa Jaji na Hakimu Mkazi Mkuu, Saul Kinemela. Hukumu hiyo iliyotolewa wakati wa utawala wa awamu ya nne.

Katika utawala wake, Rais Kikwete alianza kwa kumteua Zakhia Meghji akiwa mwanamke wa kwanza kuongoza wizara hiyo nyeti na kudumu kwa miaka miwili akafuatia Mustafa Mkulo aliyefanya kazi kwa miaka minne hadi 2012 alipoteuliwa Dk William Mgimwa (marehemu).

Mgimwa alifariki dunia akiwa waziri, hivyo nafasi yake kushikiliwa na naibu wake, Saada Mkuya aliyeongoza hadi Oktoba mwaka huu, baraza la mawaziri lilipovunjwa baada ya uchaguzi mkuu.

Maoni ya wanazuoni

Wakizungumzia hatua hivyo ya kuweka viporo, wanazuoni mbalimbali walisema kuwa unyeti wa wizara husika, unaweza kuwa chanzo chanzo cha Dk Magufuli kuendelea kuwatafuta mawaziri makini wa kusimamia vyombo hivyo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana alisema unyeti wa Wizara ya Fedha ndio unaomfanya Rais Magufuli kupata kigugumizi katika kufanya uteuzi.

Alisema kasoro zilizojitokeza kwenye sekta zinazosimamiwa na wizara hiyo yanasababishwa na usimamizi hafifu ambao unamlazimika Rais kuwa makini kwenye uteuzi wake.

“Fikiria katika siku chache tu alizoingia madarakani amekutana na madudu ambayo watanzania tunashangaa hivi haya yote yalikuwa yakifanyika wakati wizara ilikuwa na viongozi? Ni lazima Rais ajiridhishe kwa sababu anajua usimamizi mbaya ndio unalifikisha taifa kwenye hasara hii kubwa,”anasema Profesa Bana.

“Watanzania tuna uhakika kuwa nchi hii ni tajiri na inakusanya mapato mengi, kitendo cha Rais kutokurupuka kupata mtu wa kumuweka kwenye wizara hiyo ni jambo la msingi ambalo tunaamini litatusaidia,” alisema.

Alidai kuwa Tanzania ina raslimali watu kubwa wanaoweza kupewa nafasi hiyo nyeti ili waiongoze, changamoto za wizi, ukwepaji kodi na ubadhilifu ndizo zinazompa wakati mgumu Rais Magufuli kufanya uteuzi.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Jimson Sanga alisema Watanzania wamechoka kuona raslimali zinazoweza kuliingizia taifa mapato ikiwemo Bandari vinatumika kiholela.

Alisema ni lazima upatikane uongozi wenye nidhamu utakaoweza kurejesha matumaini ya wananchi, hasa kwenye sekta ya fedha.

“Alikaa mwezi mmoja na zaidi akitafakari ni nani anaaa kuongoza wizara gani na kwa nini. Najua bado anatafakari kwa nafasi hizi zilizobeba moyo wa taifa letu, kwa sababu ameonyesha Imani kwa kipindi kifupi lazima apate mtu safi atakayeongoza wizara hii,”alisema.

Richard Mbunda kutoka UDSM alisema si rahisi kuendesha nchi bila kuwa na waziri makini, katika wizara hiyo aliyoiita kuwa ni kitovu cha taifa.

“Wengi tulidhani Mwigulu Nchemba angerejeshwa, lakini kubwa Rais Magufuli hakuona hivyo, kiuhalisia bila kuwa na waziri mwenye mipango, mikakati ya kukabiliana na changamoto na asiyewaonea wengine wabadhilifu haya wizara hii haiwezi kwenda,” alisema Mbunda.

Alisema kusuasua kwa Rais Magufuli kufanya uteuzi kunaonyesha umakini wa kiongozi huyo katika kufanya maamuzi.

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.

Wizara ya elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyokuwa ikiongozwa na Shukuru Kawambwa na Wizara ya Sayansi na Teknolojia iliyokuwa ikiongozwa Profesa Makame Mbarawa zimeunganishwa na kuwa wizara moja.

Kuna wakati ilianzishwa Wizara ya elimu ya juu, Sayansi na Teknolojia iliyowahi kuongozwa na Profesa Peter Msola, ambayo pia ilifutwa na sasa imeunganishwa tena. Wizara ya Elimu ni miongoni mwa wizara zilizowekwa kiporo katika uteuzi wa waziri uliofanywa na Rais Magufuli.

Tangu kuanza kwa kampeni za kuomba ridhaa ya wananchi kumpigia kura na hata baada ya kushinda, Dk Magufuli amekuwa akisisitiza uboreshaji wa sekta ya elimu ikiwamo elimu ya bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

Kwa upande wa vyuo vya elimu ya juu, Rais Magufuli amekuwa akiahidi kuhakikisha wanafunzi wote wanapatiwa mikopo kwa wakati. Changamoto kubwa inayoikabili wizara hiyo ni mitaala ya elimu isiyoeleweka kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko ulikosababisha kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.

Wananchi wamekuwa wakishuhudia kufutwa na kurejeshwa kwa mitaala kila waziri mpya anapoingia madarakani, jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele.

Wizara yenye watumishi wengi, inakabiliwa na changamoto ya kifedha ambayo imekuwa chanzo cha ongezeko la madai ya walimu yanayotokana na malimbikizo ya uhamisho, kutolipwa kwa wakati pamoja na kupandishwa madaraja na waajiriwa wapya kutolipwa stahiki za uhamisho .

Mbali na hilo, uchakavu wa miundombinu, kutokuwepo kwa vifaa vya kufundisha na sambamba na makazi duni ya nyumba za watumishi hususani walimu hasa vijijini.

Wizara hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya kuwepo kwa mrundikano wa shule na vyuo binafsi ambavyo viwango vyake vya elimu vinatishiwa shaka na utozwaji wa ada wa kujiamulia unaolalamikiwa na wananchi lakini kubwa zaidi ni jinsi mchakato uliotangazwa na Rais Magufuli wa kutoa elimu bure utakavyotekelezwa kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne kuanzia mwezi ujao.

Vilevile suala la sayansi na teknolojia ambalo limehamishiwa wizara hiyo, ni wazi masuala ya teknolojia yanayoendana na teknolojia ya mawasiliano ya Tehama pamoja na utekelezaji wa sheria za makosa ya mitandao vitakuwa miongoni mwa mambo ya vitakavyotekelezwa. Baadhi ya mawaziri waliowahi kuongoza wizara hiyo ni Charles Kabeho, Jackson Makwetta (marehemu), Joseph Mungai na Margareth Sitta.
Dk Semakafu anena

Mhadhiri wa Chuo cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili, Dk Ave Maria Semakafu alisema waziri atakayeteuliwa lazima afumue mfumo mzima wa elimu, ili kurudisha hadhi ya sekta hiyo.

“Kuna wale wakaguzi ambao kila siku wanakagua shule, wakija wanaadika ripoti mambo yapo sawa wakati hali ni mbaya, wanafanya kazi gani? Lazima Rais amteue waziri anayetambua changamoto zilizo kwenye sekta hii nyeti,” alisema.

Alisema wizara hiyo inahitaji waziri mbunifu, mwenye kujituma na ambaye anatambua kasi ya kukua kwa sayansi na teknolojia, ili akimbizane nayo wakati wa kutekeleza majukumu yake.

“Tunatambua Rais anatafuta waziri atakayetosha kwenye wizara hii muhimu kwa sababu anatambua wazi changamoto zinazowakabili walimu hasa mazingira magumu ya kufundishia ambayo yakiboreshwa yataenda sambamba na utoaji wa elimu bure,” alisema.

Kwa upande wake, Dk Bana alisema ubora wa elimu ya Tanzania umepungua kutokana na kutokuwepo kwa umakini katika usimamizi wa wizara hiyo.

“Hii ni wizara nyeti inayotakiwa uzalishaji wanafunzi bora wenye kiwango cha elimu kinachotakiwa, ndio maana hatuna wasiwasi na hatua ya Rais Magufuli kutoteua haraka waziri wa wizara hii,” alisema.

*Nyongeza na Herieth Makwetta




Credits: Mwananchi






Mshirikishe na mwenzako kuhusu habari hii!!!
Ijue SIRI ya Raisi John Pombe Magufuli kuweka kiporo wizara 4 nyeti!!! Ijue SIRI ya Raisi John Pombe Magufuli kuweka kiporo wizara 4 nyeti!!! Reviewed by Zero Degree on 12/12/2015 03:18:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.