Lindi: Serikali yawapiga kufuli akina Lowassa!!!
Waziri Mkuu alisema hayo wakati akilishukuru Jeshi la Polisi wilayani Ruangwa kwa kufanya kazi ya kusimamia Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba 25 kwa CCM kushinda kiti cha urais na kuzoa takriban viti 180 vya ubunge.
“Naendelea kuwashukuru kwa mchango wenu mkubwa kiulinzi, lakini pia usimamizi wa zoezi zima la uchaguzi na hatimaye hivi sasa watu wameshapatikana,” alisema Waziri Majaliwa nje ya ofisi za jeshi hilo.
“Na tumesema, siasa tumeshazimaliza. Sasa tunataka tufanye kazi za maendeleo. Hatuhitaji tena watu kuja kutuvuruga. Mikutano ya shukrani itafanywa na wale tu walioshinda kwenye maeneo yao. Wengine watulie.
“Vyama sasa viache wale tu waliochaguliwa kwenye maeneo yao washukuru, wengine hawa watakuja kuleta maneno ambayo yatatuvuruga. Mimi naamini mko imara.”
Wakati Waziri Majaliwa akisema hayo, tayari Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alishapanga kuanza ziara ya kuzunguka nchi nzima kwa lengo la kuwashukuru wananchi waliompigia kura.
Hata hivyo, ilipofika siku ya kuanza ziara hiyo, Chadema ilitangaza kuwa imeahirisha hadi itakapotangazwa tena, ikiweka bayana kuwa uamuzi huo hautokani na vitisho vya makamanda wa polisi wa mikoa.
Awali, amri ya kuzuia mikutano ya kisiasa ilikuwa ikitolewa kwenye mikoa na baadhi ya makamanda wa polisi, lakini tamko hilo la juzi la Waziri Majaliwa linatia msumari marufuku hiyo ya kuendesha shughuli za kisiasa kwa hoja ya kushukuru wananchi.
Lowassa, ambaye alihamia Chadema siku chache baada ya kukatwa jina lake na CCM mwezi Julai, aliweka rekodi ya kuwa mgombea wa upinzani aliyepata kura nyingi baada ya kupigiwa kura na watu milioni 6.07 ikiwa ni asilimia 39.9, huku mshindi akipata kura milioni 8.88 sawa na asilimia 58.46.
Tamko hilo la Waziri Majaliwa tayari limeanza kupingwa sehemu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kwenye mitandao ya jamii na vyama vya siasa kutoa matamko.
“Hii ni kauli ya ajabu kutolewa na mtu anayesimamia utendaji wa shughuli za kila siku za Serikali inayotaka kuwaaminisha (wananchi) kuwa itakuwa tofauti na serikali nyingine zilizopita za CCM,” inasema Chadema katika tamko lake la jana jioni kujibu kauli ya Waziri Majaliwa.
“Kama wao (CCM) ndiyo walioshinda kama ambavyo Waziri Mkuu Majaliwa amesema na kwamba wanaendelea kutekeleza wajibu waliokabidhiwa na wananchi, tunahoji hofu yao nini hasa wakiona au wakisikia Chadema wanapanga kwenda kuongea na wananchi? Wanaogopa nini?”
Taarifa hiyo iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano, Chadema imesema kuwa waziri Majaliwa ametoa tamko hilo siku chache baada ya kufanya mkutano mjini Lindi uliowabagua wananchi kwa itikadi zao kwa kutoa nafasi kwa chama kimoja cha siasa ambacho ni CCM kuhutubia na kufanya siasa.
“Matukio haya yanaanza kumdhihirisha Waziri Mkuu Majaliwa ni kiongozi mwenye uelekeo wa namna gani hivyo kuanza kuifunua Serikali ya Rais John Magufuli chini ya CCM kwa miaka mitano ijayo itawapeleka wapi Watanzania,” inaeleza taarifa hiyo.
“Ni dalili za wazi za watu waliolewa madaraka na kuchoka kuwa viongozi na sasa wanataka kuwa watawala wenye kudhani kuwa fikra zao ndizo zinazongoza nchi badala ya misingi ya inayokubalika miongoni mwa jamii nzima kupitia Katiba, Sheria, Kanuni na taratibu mbalimbali.”
Naye makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema uamuzi huo ni kinyume na Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa na kwamba Serikali inazuia wapinzani kufanya mikutano ya kushukuru wananchi kwa kuwa inajua watatoa ushahidi wa jinsi kura zilivyoibwa.
“Wanatuzuia kwa sababu wanajua tutakwenda kutoa ushahidi wa jinsi CCM ilivyoiba kura za urais na ubunge,” alisema Profesa Safari.
“Kiongozi anaweza kuzuia mkusanyiko iwapo tu nchi itakuwa katika hali ya hatari. Jambo hili hata Rais hawezi kulizua kienyejienyeji tu,” alisema Profesa Safari ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Alisema Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 imeeleza wazi majukumu ya vyama vya siasa, kuwa ni pamoja na kufanya mikutano na maandamano.
Pamoja na tamko la Waziri Mkuu kumruhusu kufanya mikutano kutokana na ukweli kuwa alishinda uchaguzi wa ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alizungumzia marufuku hiyo kuwa ni kauli ya kisiasa isiyo na mantiki.
“Mikutano inaratibiwa na Sheria ya Vyama vya Siasa. Hii kauli ya Majaliwa naona kama ilikuwa ya kisiasa zaidi. Jeshi la polisi ndilo lenye jukumu la kuzuia mikutano na litafanya hivyo kama kutakuwa na hali ya hatari na si vinginevyo,” alisema Zitto.
Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alimtaka Waziri Mkuu kujikita katika uwajibikaji badala ya kuingilia vyama vingine.
“Sheria hairuhusu mtu yeyote kuzuia mikutano ya kisiasa isipokuwa kama kuna tishio la vita,” alisema Sungusia.
“Kuruhusu baadhi ya watu kufanya mikutano na wengine kuwazuia ni kuwanyima haki watu.”
Credits: Mwananchi
Mshirikishe na mwenzako kuhusu habari hii!!
Lindi: Serikali yawapiga kufuli akina Lowassa!!!
Reviewed by Zero Degree
on
12/25/2015 11:02:00 AM
Rating: