Serikali yabaini hekari 200 za MIRUNGI wilayani Same.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo, jana vilianzisha operesheni kabambe ya kuteketeza mashamba yote ya mirungi.
Kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Dawa za Kulevya cha mwaka 2014, anayelima mirungi adhabu yake ni faini ya Sh20 milioni au kifungo cha miaka 30 jela.
Sheria hiyo pia imetoa adhabu hadi ya kifungo cha maisha jela kwa mtu anayepatikana na dawa za kulevya, ikiwamo mirungi ambayo iko katika orodha ya dawa hizo.
Katika operesheni hiyo iliyoanza jana alfajiri katika vijiji vya Kata ya Saweni, baadhi ya wananchi walilazimika kukimbilia milimani kujificha kwa kuhofia kukamatwa.
Polisi wakiwa na magari 14, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala waliwasili katika vijiji hivyo na kuanza kazi ya kufyeka mashamba ya mirungi.
Makala alisema utafiti unaonyesha kuwa vijiji 28 katika kata 13 vinalima mirungi.
“Leo hatukukamata mtu yeyote ila nimetoa muda wa wiki mbili kwa wanaomiliki mashamba hayo kuyafyeka wenyewe na baada ya muda huo kupita watalia na kusaga meno,” alisema.
Makala alisema operesheni hiyo ilishirikisha vikosi mbalimbali vya polisi, wakiwamo wanafunzi kutoka chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA) wapatao 100.
“Tulipovamia hivyo vijiji baadhi ya watu walikimbia makazi yao, lakini baada ya kusikia hakuna mtu anayekamatwa walianza kurudi polepole na kushiriki kufyeka mashamba hayo,” alisema.
Operesheni hiyo imefanyika mwezi mmoja tangu Makala aagize kufanyika katika Wilaya ya Same, akisema wilaya hiyo ndiyo inayozalisha mirungi na kusafirishwa katika mikoa mbalimbali nchini.
“Ninapozungumzia dawa za kulevya siyo cocain pekee, hapana ni pamoja na bangi na mirungi. Same nataka ifanyike operesheni kali, sitaki kusikia eti ndiyo kitovu cha biashara ya mirungi,” alisema.
“Juzi, kuna watu walikamatwa Babati (Manyara) na mirungi walipoulizwa, walisema imetokea Same. Sitaki kusikia wahamiaji haramu wanaokamatiwa mikoa mingine wametokea Himo (Moshi Vijijini),” alisema.
Pamoja na jitihada hizo za Makala, biashara ya mirungi mkoani Kilimanjaro na miji ya jirani ni kubwa huku ulaji wake ukifanyika hadharani.
Credits: Mwananchi
Comment & Share this story!!
Serikali yabaini hekari 200 za MIRUNGI wilayani Same.
Reviewed by Zero Degree
on
12/30/2015 01:53:00 PM
Rating: