USHURU wa maegesho ya MAGARI wasababisha mgogoro mzito moshi.
Mgogoro huo umeibuka baada ya kampuni hiyo ambayo ni wakala wa kukusanya ushuru wa maegesho ya magari, kukusanya ushuru Desemba 24 na 26, mwaka huu ambazo ni siku za mapumziko kisheria.
Tayari la Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoani Kilimanjaro limeitaka manispaa kutoa maelezo ya kina ilikuwaje ikaruhusu kampuni hiyo kukusanya ushuru Desemba 24 ambayo ilikuwa ni siku ya Maulid.
“Hii si mara ya kwanza mawakala kukusanya ushuru siku za sikukuu za Waislamu ambazo ni mapumziko kisheria,” alisema Katibu wa Bakwata wa Mkoa Kilimanjaro, Rashid Mallya.
Diwani wa Kata ya Mawenzi, Hawa Mushi aliliambia gazeti hili jana kuwa, ataomba maelezo kutoka manispaa kwa nini wakala huyo alikusanya ushuru siku za kisheria za mapumziko.
“Walikusanya ushuru tarehe 24.12.2015 siku ya Maulid na wakakusanya tena tarehe 26.12.2015 siku ya Boxing Day, tunajiuliza alipata wapi hayo mamlaka ya kudharau sikukuu za kitaifa?” alihoji.
Diwani huyo ambaye kata yake ndiko sehemu kubwa ushuru huo unakusanywa, alidai kampuni hiyo imekuwa ikiwanyanyasa wamiliki wa magari ikidai wameegesha vibaya ilhali hakuna alama.
“Kuna barabara alama hazionekani au hakuna vibao vinaonyesha hii barabara ni ya kushuka au kupanda, unamkamataje mmiliki? Dereva hawezi kuota bila kuongozwa na vibao,”alidai diwani huyo.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya alisema manispaa itaupitia upya mkataba wa wakala huyo na pale itakapobainika amekiuka sheria za nchi na za halmashauri watauvunja.
“Pia, naagiza mawakala wote wenye zabuni za halmashauri waheshimu mikataba yao maana haitakuwa rafiki na mtu atakayekwenda kinyume maana tuutasitisha,” alidai Mboya.
Mmiliki wa kampuni hiyo, Moris Makoi alisema hajui nini kinachoendelea mjini kwa kuwa yupo kijijini kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka tangu Desemba 22, mwaka huu.
“Nimeondoka huko tarehe 22 kwa hiyo sijui chochote wewe watafute hao walioko ofisini watakujibu,” alisema Makoi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Okaoni, Moshi Vijijini (CCM).
Msimamizi wa kampuni huyo ambaye alitajwa kuwa ni Prosper Mmary alisema kwa wakati ukusanyaji huo unafanyika alikuwa Arusha na atakaporudi Moshi atafika ofisi za Mwananchi kutoa ufafanuzi wao.
“Tuna maelezo ya kutosha. Upo ufafanuzi mwingi subiri nikija Moshi nitakupa,” alisema Mmari hata alipoambiwa bosi wake alisema atae ufafanuzi, naye alisisitiza yupo Arusha.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Jeshi Lupembe wiki iliyopita alikaririwa na gazeti hili akisema anawasiliana na mwanasheria wa halmashauri ili kupata msimamo wa kisheria.
Credits: Mwananchi
Comment & Share this story!!
USHURU wa maegesho ya MAGARI wasababisha mgogoro mzito moshi.
Reviewed by Zero Degree
on
12/29/2015 02:31:00 PM
Rating: