Loading...

Yajue MATUKIO 10 yaliyovuma sana katika mitandao ya kijamii kwa mwaka 2015.


Mwaka 2015, kama ilivyo miaka mingine yote iliyotangulia, uligubikwa na matukio mengi ambayo yaligeuka gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii, hasa Twitter na kutengenezewa hashtags (#) zilizopata wafuasi wengi zaidi.


Yafuatayo ni matukio 10 yaliyotingisha zaidi na kufuatiliwa na watu wengi kwenye Mtandao wa Twitter, kuanzia Januari mpaka Desemba.


1. SHAMBULIO LA CHARLIE HEBDO, UFARANSA


Mapema Januari, mwaka huu, watu wanaodhaniwa kuwa ni magaidi wenye msimamo mkali, walivamia ofisi za Gazeti la Charlie Hebdo jijini Paris, Ufaransa kwa madai kuwa gazeti hilo lilichapisha katuni zinazomkashifu Mtume Muhamad (S.A.W).

Katika shambulio hilo, watu 12 walipigwa risasi na kufa. Watumiaji wa Twitter wakaanzisha Hashtag ya #JeSuisCharlie ambayo ilipata wachangiaji wengi sana ndani ya muda mfupi, kila mmoja akilaani tukio hilo.


2. AJALI YA NDEGE YA GERMAN WING

Mwezi Machi nao uliwaacha wengi kwenye majonzi kufuatia ajali mbaya ya ndege ya German Wing iliyoanguka kwenye Milima ya Alps, Ufaransa na kuua watu wote 150 waliokuwa ndani ya ndege hiyo.

Eneo ilipotokea ajali pakiwa na maua

Baadaye ilibainika kwamba rubani mwenza, Andreas Lubitz ndiye aliyesababisha ajali hiyo kutokana na matatizo ya akili yaliyokuwa yanamsumbua. Hashtag ya #GermanWings ikafunguliwa na kupata wachangiaji wengi ndani ya muda mfupi.

3. MAUAJI YA WATU WEUSI MAREKANI

Kitendo cha kupigwa risasi na kuuawa kwa wanaume wawili weusi, Walter Scott na Freddie Gray kilichotokea Aprili, mwaka huu, kiliibua hisia nzito miongoni mwa jamii ya watu weusi nchini humo.

Watu weusi wakiandamana

Harakaharaka watumiaji wa Twitter wakafungua Hashtag ya #BlackLivesMatter (Maisha ya Watu Weusi ni Muhimu) iliyotumika kama jukwaa la watu weusi kuhamasishana kufanya maandamano ya kupinga mauaji hayo. Watu zaidi ya milioni tisa walichangia maoni yao ndani ya muda mfupi.

4. KURA YA KURUHUSU MAPENZI YA JINSIA MOJA

Mwezi Mei, Ireland ilianzisha mchakato wa kuwataka wananchi wake kupiga kura kuunga mkono au kukataa kuidhinishwa kwa mapenzi na ndoa za jinsi moja.

Jambo hilo lilionekana kuwavutia mashoga na wasagaji wengi waliokuwa wameikimbia nchi hiyo kwa sababu ya kukosa haki hiyo, walianza kumiminika kwa wingi kurejea makwao huku wakihamasishana kupiga kura ya kuunga mkono sheria ya kuruhusu mapenzi ya jinsia moja kupitia Mtandao wa Twitter kwa Hashtag ya #HomeToVote. Katika matokeo ya jumla, zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wa nchi hiyo, walipiga kura kuunga mkono sheria hiyo.

5. KUFILISIKA KWA UGIRIKI

Mwaka 2015 haukuwa mzuri kwa Ugiriki ambayo sera yake ya kubana matumizi, ilisababisha kudorora kwa uchumi na kuongezeka kwa madeni yenye masharti magumu kutoka kwa nchi wahisani. Hatua hiyo ilionekana kuwakera wananchi wake walioamua kuanzisha kampeni ya kukataa mikopo yenye masharti magumu kutoka kwa wahisani mwezi Julai. Kupitia Twitter, ikaanzishwa Hashtag ya #Greferendum kuwashinikiza viongozi kuchukua hatua za haraka kunusuru uchumi wa nchi hiyo.

6. SAKATA LA WAKIMBIZI ULAYA

Wakimbizi wanaokimbia machafuko katika nchi ya Syria na majirani zake na kuvuka bahari kwenda Ulaya, ni miongoni mwa matukio yaliyotingisha sana mwaka 2015. Zaidi ya wakimbizi milioni 20, walivuka bahari kukimbilia Ulaya, huku wengine wengi wakipoteza maisha baharini. Nchi nyingi za Ulaya zilikuwa zikikataa kuwapokea lakini wananchi wake wakawa wanaandamana kuzisihi serikali zao ziwapokee.

Mtandao wa Twitter ulitumika kama jukwaa kubwa la kuwatetea wakimbizi hao ambapo Hashtag ya #RefugeesWelcome (Karibuni Wakimbizi) ilichangiwa na watu wengi, wakimbizi wakapokelewa kwenye baadhi ya nchi na kupewa misaada.

7. MWANAFUNZI WA KIARABU KUHUSISHWA NA UGAIDI

Ahmed Mohamed (14), kijana mwenye asili ya Kiarabu aliyekuwa akisoma Texas, Marekani, aliingia kwenye msukosuko mkubwa kufuatia saa ya ukutani aliyoitengeneza kienyeji kwa utundu wake, kudhaniwa kuwa ni bomu.


Ahmed Mohamed

Hali hiyo ilisababisha polisi wa Texas wamvamie akiwa darasani na wenzake na kumchomoa chini ya ulinzi mkali. Tukio hilo lilisababisha hasira miongoni mwa wananchi wengi walioona mtoto huyo anabaguliwa kwa sababu ya asili yake.
Hashtag ya #IstandWithAhmed ikaanzishwa kumtetea. Baadaye aliachiwa huru baada ya kubainika kuwa alichotengeneza hakikuwa bomu bali saa.

8. MAANDAMANO YA WANACHUO AFRIKA KUSINI

Kitendo cha serikali ya Afrika Kusini kutangaza kupandisha ada za twisheni kwa wanafunzi wa vyuo vyote nchini humo, Oktoba, 2015 iliamsha hasira kali miongoni mwa wanachuo walioanza kuandamana mitaani wakiwa na mabango ya kupinga ongezeko hilo.

Hawakuishia hapo, licha ya kupambana na polisi mara kwa mara, waliendelea kuandamana na wakawa wanautumia mtandao wa Twitter kwa Hashtag ya #FeesMustFall (Ada Lazima Zishushwe) kuhamasishana kuendelea kugoma. Baadaye Rais Jacob Zuma aliamua kufuta ongezeko hilo.

9. MASHAMBULIZI YA PARIS
Wiki chache zilizopita, Novemba, 2015, Jiji la Paris, Ufaransa lilishambuliwa tena na magaidi katika mfululizo wa mashambulizi yaliyogharimu maisha ya watu 130 na kujeruhi wengine 350.

Mashambulizi hayo yaliamsha hisia kali kwa watu wa dunia nzima ambapo kupitia Hashtag ya #PrayForParis, walikuwa wakiwalaani waliofanya tukio hilo na kuwatia moyo Wafaransa. Ndani ya siku chache tu, mamilioni ya watu walikuwa wamechangia mawazo yao.

10. MKUTANO WA MABADILIKO YA HALI YA HEWA WA COP21
Uharibifu mkubwa wa mazingira dunia nzima ndiyo iliyokuwa agenda kuu ya mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa, Conference of the Parties (COP21), uliofanyika jijini Paris, Ufaransa ambapo wanasiasa na wataalamu zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali duniani walikusanyika kujadiliana juu ya nini kifanyike kuiokoa dunia.

Watumiaji wa mitandao nao hawakuwa nyuma ambapo kupitia Twitter, Hashtag ya #COP21 ilipata wachangiaji karibu kutoka kila sehemu duniani, wakiposti picha za jinsi mazingira yalivyoharibiwa nchini kwao na kupendekeza nini cha kufanya.




Source: Global publishers


Comment & Share this story!!

Yajue MATUKIO 10 yaliyovuma sana katika mitandao ya kijamii kwa mwaka 2015. Yajue MATUKIO 10 yaliyovuma sana katika mitandao ya kijamii kwa mwaka 2015. Reviewed by Zero Degree on 12/28/2015 06:11:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.