Ada ya milioni 60 yatetewa Dar.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Dar es Salaam. Tofauti ya ubora wa elimu, mazingira ya kufundishia, mishahara kwa walimu na miundombinu ndicho chanzo cha kuwapo matabaka kati ya shule za kimataifa na za kawaida, kwa mujibu wa wadau waliohojiwa na Mwananchi.
Gazeti la Mwananchi lilihoji wadau mbalimbali wa elimu baada ya kuchapisha habari iliyoonyesha ukubwa wa viwango vya ada vinavyotozwa na shule za kimataifa ikilinganishwa na ada za shule binafsi za kawaida ambazo wanafunzi wake hutahiniwa na Baraza la Taifa la Mitihani la Taifa (Necta).
Katika habari hiyo iliyochapishwa jana, gazeti hili lilionyesha ada za baadhi ya shule hizo za kimataifa kufikia hadi Sh60 milioni kwa mwaka huku chekechea ikitoza hadi Sh35 milioni kwa kipindi hicho.
Pamoja na viwango hivyo vikubwa, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Hakielimu, James Kalaghe alisema shule hizo zinatoza ada kubwa kwa sababu zinatumia mfumo wa kimataifa, mazingira mazuri ya kusomea na walimu bora.
Kalaghe alisema matabaka yaliyopo katika elimu yanasababishwa na uduni wa shule za umma ambazo zinachukua asilimia 94.7 ya wanafunzi wote nchini.
Pia, alisema shule za kimataifa zinawalenga raia wa kigeni waliopo nchini, kama mabalozi na wale wanaofanya kazi katika taasisi za kimataifa zikiwamo za Umoja wa Mataifa.
“Sisi wadau wa elimu na Serikali tushughulike na shule za umma ambazo zina wanafunzi wetu. Usawa katika elimu hauwezi kupatikana kama hatutaboresha mazingira ya shule za umma,” alisema.
Alisema inaonekana shule binafsi zina viwango bora vya elimu, walimu wenye taaluma ya kutosha na wasimamizi wazuri.
“Walimu wa shule za umma wana msongo wa mawazo, hawana hela ya likizo, hawapewi stahiki zao hata wakihamishiwa vijijini. Ili usawa uwepo, shule za umma ziimarishwe ili zitoe elimu bora, tuwasimamie stahiki zao, tuwalipe vizuri,” alisema.
Mkuu wa Kituo cha Elimu (Duce), Dk Joviter Katabaro alisema kama shule si ya kimataifa inatoza ada hadi Sh60 milioni, basi mfumo huo unajenga matabaka.
“Ni bahati mbaya kwamba bado tunasubiri wizara kutoa mchanganuo wa ada elekezi katika shule binafsi.
“Ni sawa na hoteli, kila mtu anatoa bei yake kwa sababu hakuna mtu wa kumwambia,” alisema.
Hata hivyo, alisema iwapo shule inayoitwa ya kimataifa inatoza ada kubwa basi aghalabu wanaopeleka watoto hapo wanataka wafuate mitalaa ya kimataifa na wanapanga ada hizo kwa utaratibu wa kimataifa.
“Lakini tujue kuwa hiyo shule imewekwa kwa ajili ya watu gani, mabalozi au watu wengine kutoka nje, kwenye ngazi za kimataifa, labda UNDP, UNHCR. Huenda watoto wao wanatakiwa kupelekwa. Kwa hiyo matabaka hayo yameanzia kwenye aina ya kazi na utaifa,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Maina alisema ni vyema kusubiri kwanza Serikali itakachozungumza kuhusu ada elekezi ili kuwasikia wenye shule hizo za kimataifa na watakachosema. “Nasubiri Serikali itatumia vigezo gani kuweka ada elekezi na wamiliki wa shule binafsi watachukua uamuzi gani. Inashangaza kuona mwanafunzi wa chekechea analipa ada kubwa kuliko mwanafunzi wa chuo kikuu,” alisema.
Hata hivyo, Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa alisema amesikia taarifa za shule za kimataifa kutoza ada kubwa na kuzungumza na timu yake kwa ajili ya kufuatilia.
“Ingawa hatuhusiki moja kwa moja na shule za kimataifa, lakini lazima tukisikia taarifa kama hizo tuzifuatilie. Kimsingi tunafahamu shule chache zinazotoza ada kubwa,” alisema Bhalalusesa.
Alisema ingawa yupo likizo, amesoma taarifa hizo kisha kuzungumza na msaidizi wake ili kujua kwa kina kuhusu ada hizo.
ZeroDegree.
Ada ya milioni 60 yatetewa Dar.
Reviewed by Zero Degree
on
1/22/2016 11:32:00 AM
Rating: