Loading...

Dk Magufuli: Arusha, K’njaro chapeni kazi


Rais John Magufuli

Arusha. Rais John Magufuli jana, alitua kwa mara ya kwanza katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro tangu aingie madarakani na kuwataka wakazi wake kufanya kazi, kwani uchaguzi umekwisha.

Akizungumza na mamia ya watu waliojitokeza kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na barabara kuu ya Arusha -Moshi, Dk Magufuli alishukuru kwa mapokezi aliyopata na kusema hatawaangusha wananchi hao.

“Uchaguzi umekwisha ndugu zangu sasa ni kazi tu na wananchi wa Arusha na Kilimanjaro sitawaangusha, ahadi zangu zote nilizotoa wakati wa kampeni nitazitekeleza,” alisema.

Alisema anajua matatizo ya Arusha na Kilimanjaro na kama alivyoahidi atatekeleza yote.

Katika uwanja wa Kia, Dk Magufuli alipokewa na viongozi wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Arusha, Felix Ntibenda, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala pamoja wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Arusha, wenyeviti wa halmashauri na baadhi ya wabunge.

Rais Magufuli alisalimiana na viongozi na wananchi baada ya kutua Kia saa 10 jioni na baadaye alizungumza na mamia ya watu waliokuwa wamesimama kando ya barabara katika maeneo ya njiapanda ya Kia, Usa river na Tengeru.

Alisema jukumu alilonalo ni kufanya kazi na atatekeleza ahadi zake, huku akiwataka wananchi kufanya kazi.

Kutokana na hotuba yake kuwakolea, baadhi yao walisikika wakisema Arusha kuna majipu ayatumbue jambo ambalo lilimfanya acheke.

Akizungumzia katika mapokezi hayo, Ntibenda aliwapongeza wananchi kujitokeza tangu mchana hadi jioni na kumsikiliza Rais na akawataka waendelee kujitokeza katika shughuli ambazo atashiriki.

Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro na madiwani wote wa Chadema katika jiji hilo walishiriki mapokezi hayo.

Calist alipongeza hatua ya Rais Magufuli kufikia katika Ikulu ndogo ya mkoa huo.

“Tunampongeza Rais kwa kazi nzuri ya kubana matumizi kwa vitendo. Tangu juzi tumeona Ikulu inakarabatiwa ili Rais afikie, hili ni jambo zuri,” alisema.

Juzi, Ntibenda aliwataka wananchi kuonyesha moyo wa upendo na ukarimu wakati wote wa ziara ya Rais na kusisitiza kuwa ulinzi utakuwa mkali katika maeneo ya mji.

Mapema, askari walionekana wakiwa katika doria kwenye barabara zinazoingia na kutoka Ikulu ndogo.

Source: Mwananchi




ZeroDegree.
Dk Magufuli: Arusha, K’njaro chapeni kazi Dk Magufuli: Arusha, K’njaro chapeni kazi Reviewed by Zero Degree on 1/22/2016 11:37:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.