Hoja 12 zilizosababisha Baraza Kuu la Uongozi la CUF kufikia uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar.
Dar es Salaam. Baraza Kuu la Uongozi la CUF limeamua kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi (ZEC), likitoa hoja 12 zilizosababisha kufikia uamuzi huo.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alitangaza kuwa uchaguzi huo wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani utafanyika Machi 20 na hautatanguliwa na kampeni wala mabadiliko ya wagombea.
Katika tamko hilo Baraza Kuu la CUF limeuelezea uchaguzi wa marudio, kuwa ni batili na hivyo kushiriki ni kuhalalisha haramu.
“Kwetu sisi uchaguzi haukufutwa,” alisema katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
“Kwanza tumekubali kurudia uchaguzi, maana yote msimamo wetu wa nyuma hauna maana. Tunahalalisha haramu iliyofika. Na chama chetu ni chama ambacho kinafuata principles, si chama kinachokwenda hivihivi.
“Kwa hiyo tunasema kuingia kwenye uchaguzi, maana yake tunahalalisha haramu. Kwa sababu CCM hawawezi kuandaa uchaguzi wa kurudia ili wakashindwe tena. Wameshajiandaa. Sisi tuna taarifa kuwa watu wa CUF kwenye Daftari la Kudumu (la wapigakura) wanafutwa.”
Maalim Seif alitangaza tamko hilo baada ya kikao cha baraza hilo, ambalo ndilo chombo cha juu cha maamuzi cha chama hicho kikuu cha upinzani visiwani. Baraza hilo lilikutana kwa dharura jijini Dar es Salaam jana baada ya ZEC kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio wiki iliyopita.
Akisoma maazimio hayo, Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima alisema hoja ya kwanza ni chama kutambua kuwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ulishafanyika Oktoba 25, 2015 na ulikamilika kwa washindi wa ubunge, uwakilishi na udiwani kutangazwa na kupewa shahada za ushindi.
“Kwa upande wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, matokeo yalishabandikwa nje ya vituo vya majumuisho vya majimbo yote 54. Kilichokuwa kinaendelea baada ya hapo ni kuhakiki matokeo kutoka majimboni,” alisema.
Pia alisema kati ya majimbo 40, matokeo ya majimbo 31 yalishakamilika na kutangazwa kabla ya Jecha kufuta matokeo.
Taslima pia alisema CUF haitashiriki uchaguzi wa marudio kwa kuwa si halali, wakati katika hoja ya tatu amesema ni kuamini katika utawala wa sheria, demokrasia na Katiba ya nchi.
Pia chama hicho kimeeleza kuwa sababu nyingine ni kutokana na matamko ya Jecha kutokuwa halali na kwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya mwaka 1984.
“Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinachotoa uwezo kwa Jecha na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio,” alisema.
Hoja ya tano, kwa mujibu wa Taslimu ni msimamo wa waangalizi wa kimataifa waliosema kwenye taarifa zao kuwa mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar ukamilishwe na mshindi kutangazwa.
CUF pia imetaja hoja ya sita kuwa ni kutiwa moyo na msimamo wa taasisi na wadau wengine wa kutaka Katiba ya Zanzibar iheshimiwe na suala la amani lizingatiwe.
Chama hicho kimesema hoja ya saba ni kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuvitaka vyama kushiriki uchaguzi wa marudio wakati akijua demokrasia imekiukwa.
Katika hoja ya nane, chama hicho kimetaja kitendo cha Rais John Magufuli kutotekeleza ahadi yake ya kutafuta suluhisho la mgogoro huo. Kikimtaka ajitathmini.
Hoja nyingine ni matumizi ya nguvu kubwa ya vyombo vya dola, ambavyo ni vikosi vya ulinzi na usalama na vile vya Serikali ya Mapinduzi licha ya wananchi kuonyesha utulivu, kikisema kinalaani vikali kitendo hicho.
Katika hoja mbili nyingine, CUF inavitaka vyombo vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai kuchunguza kauli na matamko ya viongozi na kuchukua hatua na pia kuwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa utulivu na msimamo wa kutetea maamuzi yao ya Oktoba 25.
Maalim Seif Afunguka
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Maalim Seif alisema licha ya kuyajwa kuwa alikosea kwa kujitangazia ushindi, haoni kuwa hiyo ilikuwa sababu ya kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar.
“Tuseme kweli ni kosa kama nimetangaza yalikuwa matokeo ya urais, mimi sikutangaza matokeo nimesema matokeo yametangazwa kama wanahisi ni kosa wanipeleke mahakamani kwa nini hawataki kunipeleka mahakamani? Je hili kosa ndiyo la kufuta uchaguzi mzima?” alihoji Maalim.
Katika hatua nyinyine, Serikali imesema kuwa jambo lolote litakalotokea, kama umwagaji damu utakaotokana, litakuwa juu ya wote wanaopinga uchaguzi wa marudio Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba alisema hayo wakati akijibu hoja za wabunge kuhusu hotuba ya Rais aliyoitoa wakati akizindua Bunge Novemba 20 mwaka jana.
“Hakuna mwenye uhalali kikatiba wala mahakama yoyote inayoweza kupingana na Tume kwa kuwa Katiba ya Zanzibar imeipa meno ya kufanya hayo ambayo yalifanyika,” alisema Makamba.
Alisema kuwa uchaguzi huo ulifutwa kwa kutumia Katiba ya Zanzibar ibara ya 119 iliyoipa tume uhuru mkubwa wa kuamua, pamoja na Sheria Namba 5 ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo inampa mwenyekiti mamlaka ya kufuta uchaguzi kama ataona kuna dosari.
Alitaja dosari nane ambazo ni pamoja na malalamiko kutoka kwa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo pamoja na mmoja wa wagombea kujitangazia matokeo.
Source: Mwananchi
Hoja 12 zilizosababisha Baraza Kuu la Uongozi la CUF kufikia uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar.
Reviewed by Zero Degree
on
1/29/2016 05:20:00 PM
Rating: