Maalim Seif atoa msimamo mkali
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Hamad Shariff ametoa msimamo mkali kuhusu mkwamo wa kisiasa visiwani humo akisema suluhu yake ni kutangazwa kwa mshindi ili iundwe Serikali ya Umoja wa Kitafa na si vinginevyo.
Pia, Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alisisitiza msimamo wa chama chake wa kupinga kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo na kutoa mapendekezo matano ya kuutatua.
Oktoba mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alitangaza kufuta matokeo yote ya uchaguzi kwa madai kuwa kuna taratibu zilikiukwa wakati mchakato huo unaendelea.
Hadi leo, ikiwa imepita miezi mitatu tangu Jecha alipotoa uamuzi huo, kumekuwa na sintofahamu kuhusu mzozo huo wa kisiasa licha ya viongozi wa mbalimbali ngazi za juu kufanya mazungumzo ya namna ya kuutatua.
Hata hivyo, wakati mazungumzo baina ya viongozi hao yakiendelea makada kadhaa waandamizi wa CCM wamekuwa wakitoa matamko ya kurudia uchaguzi huo, huku wale wa CUF wakipinga.
“Hoja ya kurudiwa uchaguzi ambayo imeshikiliwa bango na CCM, Zanzibar ni kutafuta manufaa ya kisiasa baada ya kushindwa kwenye uchaguzi,” alidai Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye pia ni katibu mkuu wa CUF alisema kufuta uchaguzi ni batili na chama chake hakiwezi kuendelea kuhalalisha haramu kwa kurudia uchaguzi na hata viongozi waliopo madarakani kwa sasa visiwani humo wapo kibabe.
“Ikiwa Tume italazimisha kutangaza marudio ya uchaguzi tutaitisha kikao kikubwa kuja kufanya maamuzi na msimamo wetu upo hivyo,” alisema.
Maalim Seif alisema CCM inaringia vyombo vya dola kwa sababu inadhani inaweza kufanya lolote na vyombo hivyo vikaikingia kifua na kusahau nguvu za umma.
“Umma ukiamua hakuna chombo cha dola kitakachozua. Ombi langu kwa CCM ni kwamba wasiwafikishe wananchi kuona kuingia barabarani ndiyo suluhu. Hatutaki tena yatokee yaliyotokea 2001 katika nchi yetu,” alisema.
Kiongozi huyo ambaye mwezi uliopita alikuwa kwenye meza ya mazungumzo na Rais John Magufuli kujadili suala hilo, alitoa mapendekezo matano ya kutatua mgogoro huo.
Alisema ili kulinda misingi ya Katiba ya Zanzibar, na ZEC kujenga uhalali na heshima katika kutekeleza kazi zake, ni lazima mwenyekiti wa uchaguzi akae pembeni kwa kujiuzulu au kusimamishwa kazi kwa makosa aliyofanya.
Alisema pendekezo la pili ni kumaliziwa kutangazwa kwa matokeo ya urais katika majimbo tisa ambayo yalishahakikiwa na kumaliza kuhakiki matokeo ya urais kwa majimbo 14 yaliyobaki na kutangaza matokeo.
“Hatua hiyo ni halali na sahihi chini ya kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar. Pia chini ya kifungu cha 42 (6) cha Sheria ya Uchaguzi ambayo inataka matokeo ya urais yatangazwe ndani ya siku tatu,” alisema.
Pendekezo la tatu ni kwa Rais Magufuli kuongeza juhudi zenye lengo la kufanikisha jambo hilo.
Alisema ana imani na Dk Magufuli kwani tangu mwanzo alionyesha nia ya kutaka suluhu ipatikane kwa njia ya amani.
Nne ni kufanyika mazungumzo ya haraka kati ya uongozi wa juu wa vyama vya CUF na CCM ili kukamilisha taratibu ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya mshindi wa urais katika Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.
“Kupitia vikao hivyo, kama kuna mambo yoyote yanayohitaji kujadiliwa na kupata mwafaka juu uundwaji wa Serikali hiyo yajadiliwe na kupata mwafaka,” alisema Maalim Seif.
Katika pendekezo la tano, alisema mfumo wa uchaguzi wa Zanzibar unahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuondoa kasoro zilizopo kwa nia ya kuimarisha mfumo huo kwa ajili ya chaguzi baadaye.
“Tunaamini kwamba ufumbuzi wa mgogoro uliopo lazima uzingatie Katiba, sheria na misingi ya utawala bora,” alisema. “ …Zanzibar kuna tatizo kubwa ambalo halipaswi kuendelea kupuzwa. Wakati umefika kwa mamlaka zinazohusika kutokwepa wajibu kwa wananchi wa Zanzibar.”
Source: Mwananchi
Maalim Seif atoa msimamo mkali
Reviewed by Zero Degree
on
1/12/2016 10:47:00 AM
Rating: