Loading...

Mgogoro wa umeya Dar kukwamisha bajeti.


Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngulumi

Dar es Salaam. Mgogoro wa uchaguzi wa mameya katika Manispaa za Kinondoni na Ilala jijini Dar es Salaa huenda ukaathiri mchakato wa uandaaji bajeti za mamlaka hizo iwapo viongozi hao hawatachaguliwa mwezi huu.



Kuchelewa kwa uchaguzi huo, kutafanya mchakato wa bajeti usiwe shirikishi kama Sheria ya Serikali za Mitaa inavyotaka hivyo kuinyima uhalali wa kisheria.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngulumi alisema jana kuwa kwa sasa, utendaji unaendelea vizuri bila tatizo, lakini vikwazo vingi vitatokea iwapo Januari itapita bila ya kuwa na baraza la madiwani.

“Kwa sasa tunatekeleza bajeti iliyopitishwa lakini tunapoelekea kwenye bajeti mpya, kuna ugumu ndiyo maana tumeambiwa isizidi Januari 16 tuwe tumekamilisha uchaguzi wa Meya.” alisema Mngulumi.

Alisema bila baraza la madiwani, uandaaji wa bajeti hiyo hautakuwa shirikishi na kwamba ilitakiwa mwezi huu usianze bila ya kuwa na chombo hicho cha uwakilishi.

Kwa takriban mwezi sasa, uchaguzi wa mameya katika manispaa za Ilala na Kinondoni umekumbwa na mgogoro baada ya CCM kutuhumiwa kupeleka wabunge wa viti maalumu kutoka maeneo mengine nje ya majimbo ya manispaa hizo.

Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema kwa sasa shughuli nyingi zimesimama kwa kuwa hakuna diwani wala mbunge yeyote mwenye taarifa rasmi za maendeleo ya Manispaa ya Ilala.

Mgogoro ulisababisha kufunguliwa kesi mahakamani kupinga uchaguzi katika mazingira hayo.

Alisema Manispaa kupitia vikao vya baraza la madiwani ingekuwa imewapatia muhtasari wa maendeleo na kwamba hadi sasa madiwani hawana nguvu yoyote ya kuhoji kwa watendaji wa kata kwa kuwa hawana taarifa za msingi.

“Kamati ambazo huundwa na Meya kwa ushirikiano na Mkurugenzi wa Manispaa hazipo. Kwa sasa shughuli zozote zinazohusu utendaji wa kamati haziwezi kufanyika,” alisema Mwita.

Alisema kwa sasa kuna suala la kubadilisha mkandarasi wa barabara ya Kitunda – Kivule – Msongola yenye urefu wa kilomita 11 kwa kushindwa kutimiza masharti, lakini kwa kuwa hakuna baraza la madiwani hakuna kinachoweza kufanyika.

Kuhusu agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene la kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika na watu wasiohusika katika halmashauri hizo kutoshiriki ili kumaliza mchakato huo ndani ya muda, Mwita alisema wamepokea kwa furaha na wanaunga mkono.

“Tunalizingatia agizo hili na tunataka makada wa CCM nao walizingatie ili tumalize huu mvutano. Hatuhitaji kupendelewa ila haki lazima itendeke.

“Sisi hatutaki kikao chenye ‘figisufigisu’ kwa sababu akichaguliwa mtu ambaye hakubaliki hata utendaji wake na utakuwa mbovu usioleta maendeleo,” alisema Mwita.

Diwani wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob alisema siku 30 za menejimenti ya Kinondoni kukaimu majukumu ya baraza la madiwani baada ya Uchaguzi Mkuu zimekwisha na kwamba kinachoendelea ni uvunjifu wa Sheria namba 288 ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982.

Alisema kutokuwapo kwa baraza la madiwani, kunaweza kukaleta matatizo katika utekelezaji wa sera ya elimu bure kwa kuwa ni lazima halmashauri ifanye baadhi ya mabadiliko katika bajeti zake.

“Manispaa ya Kinondoni ilikuwa ikitegemea ada na baadhi ya michango ya wanafunzi kama sehemu ya mapato yake na tulitarajia kukusanya takriban Sh1 bilioni. Sasa wametoa inabidi turudi na kufanya maboresho ya bajeti lakini haiwezekani,” alisema Jacob.

Alisema baadhi ya makandarasi wanaodai fedha za nyongeza hawawezi kupatiwa kwa kuwa madiwani wa kuidhinisha hawajaapishwa na hakuna vikao rasmi.

Jacob ambaye pia alikuwa diwani awamu iliyopita, alisema kuna watumishi wa manispaa waliosimamishwa kwa ajili ya kuchunguzwa na uongozi wa mkoa, lakini hatua stahiki haziwezi kuchukuliwa bila kibali cha madiwani, hivyo kukwamisha masuala ya nidhamu.

“Kuna miradi ya barabara kama Sinza 1 ambayo ina mgogoro na mkandarasi, bila shaka ni kwa sababu ya fedha ambazo tungekuwapo tungetatua. Barabara ya Sinza Mori nayo ilitakiwa kurekebishwa lakini imekwama,” alisema Jacob.



Source: Mwananchi
Mgogoro wa umeya Dar kukwamisha bajeti. Mgogoro wa umeya Dar kukwamisha bajeti. Reviewed by Zero Degree on 1/12/2016 10:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.