Loading...

Mtihani mwingine mgumu kwa Rais Magufuli.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikihaha kubana matumizi na kufuatilia walipa kodi, bado ina kazi nyingine kubwa ya kulipa kodi ya pango ya ofisi za wizara, idara na taasisi zake. 




NSSF Water Front ni moja ya majengo ambayo Serikali imekodi kwa ajili ya ofisi za wizara na idara zake.

Hii inatokana na Serikali kutokuwa na majengo yake na hivyo kulazimika kupanga kwenye majengo ya mashirika ya umma na binafsi ambayo kodi yake ni kubwa.

Tangu Novemba 5, 2015 wakati Rais John Magufuli alipoanza kazi, amekuwa akifanya jitihada kubwa kuongeza makusanyo ya kodi, huku akibana matumizi yasiyo ya lazima ili apate fedha kwa ajili ya kuzielekeza kushughulikia matatizo ya wananchi.

Katika kutekeleza hilo, Rais aliamua kuzuia semina elekezi kwa mawaziri na kufuta sherehe za maadhimisho ya Uhuru, Wiki ya Ukimwi zilizokuwa zifanyike mwaka jana na kuelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli hizo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) na kukarabati barabara.

Lakini juhudi hizo, sasa zinakumbana na mtihani mkubwa wa kulipia gharama ya kodi za pango za ofisi zake.

“Kwa mwaka wa fedha 2013/2014, jumla ya Sh18.77 bilioni zilitumika kugharamia kodi ya pango ya ofisi za Serikali, na kiasi hicho kiliongezeka mpaka Sh18.97 bilioni kwa mwaka 2014/2015,” alisema mtendaji mkuu wa Wakala wa Majengo (TBA), Elius Mwakalinga alipozungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi, umebaini kuwa ofisi nyingi za Serikali, idara na taasisi zake zimo kwenye majengo ya mashirika ya umma na ya kampuni binafsi ambayo kodi yake ni kubwa.

Miongoni mwa wizara ambazo hazina majengo yake ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambayo imepanga kwenye jengo la kisasa la PSPF na Wizara ya Ujenzi katika jengo la Holland House.

Baadhi ya taasisi ni pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mfuko wa Barabara, Tume ya Pamoja ya Fedha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kurugenzi ya Mashtaka ya Umma (DPP), na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Wakala wa Majengo

Kwa mujibu wa mtendaji mkuu wa TBA, mzigo wa gharama unaongezeka mwaka hadi mwaka.

Mtendaji huyo alisema mkoani Arusha, ofisi za taasisi tano za Serikali ziko kwenye majengo ya kupanga wakati Dodoma ni 16, Geita (5), Iringa (15), Kagera (12), Katavi (7), Kigoma (8), Kilimanjaro (1), Lindi (7), Manyara (8), Lindi (7), Mara (2) na Mbeya (9).

Ofisi nyingine zimepangwa katika mikoa ya Morogoro (6), Mtwara (10), Mwanza (13), Njombe (7), Pwani (43), Rukwa (3), Ruvuma (4), Shinyanga (3), Simiyu (14), Singida (5), Tabora (10) na Tanga (6).

Hata hivyo, TBA haikuwa na idadi ya taasisi zilizopanga majengo mkoani Dar es Salaam.

“Baadhi ya taasisi ambazo zinategemea majengo ya kukodi kwa kiwango kikubwa ni pamoja na Takukuru, Sumatra, Sekretarieti ya Maadili, Wakala wa Vipimo, TCRA na Mamlaka ya Dawa,” alisema Mwakalinga.

Kuhusu mkakati wa kuzuia au kupunguza gharama hizo Mwakalinga alisema: “Tutahakikisha tunaokoa kiasi kikubwa cha fedha zinazotumika kulipa pango kwa kujenga ofisi au kupangisha kwenye majengo yanayomilikiwa na TBA ambayo gharama zake ni nafuu.

“Nakumbuka Rais Magufuli wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi, mara kadhaa aliwahi kunieleza jinsi alivyokuwa akikerwa kuona ofisi ya wizara hiyo ipo kwenye jengo la kupanga.

“Alikuwa akinipa changamoto kwa kuniagiza nihakikishe jambo hilo linafika mwisho,” alisema.

Hata hivyo, alisema tayari mipango ya kuanza ujenzi wa jengo la wizara litakalogharimu Sh500 milioni imeanza baada ya kupatikana fedha hizo.

Alisema licha ya kupata fedha hizo, TBA inaendelea na mazungumzo na wawekezaji mbalimbali walioonyesha nia ya kutaka kushirikiana nao kwenye uwekezaji katika baadhi ya ujenzi wa majengo hayo.

Mwakalinga alisema TBA ina ndoto ya muda mrefu ya kutimiza madhumuni ya kuanzishwa kwake, ambayo ni kuboresha huduma zilizokuwa zikitolewa na iliyokuwa Idara ya Majengo kwa kutumia rasilimali kutokana na majengo yenyewe. “Kasi yetu inakwamishwa na fedha. Tunahitaji fedha ili kutimiza malengo na hatimaye tutachangia ukuaji wa uchumi kwa kupunguza gharama za uendeshaji serikalini zinazotokana na ofisi za kupanga,” alisema.

Mwakalinga, pia alisema TBA ina mpango wa kujenga majengo ya ofisi katika mikoa mbalimbali ambayo yatajulikana kama TBA Towers.

Majengo hayo kwa kuanzia, yatajengwa katika ‘yadi’ za ujenzi zilizopo kwenye mikoa saba ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Tanga Dodoma, Mwanza Mbeya, Arusha na Mtwara.

Naye mkurugenzi wa ushauri wa TBA, Edwin Nndunduma, alisema gharama nyingine ambazo Serikali imekuwa ikiingia ni kulipia kodi ya pango ya makazi kwa watumishi wake.

“Tulianzisha programu ya ujenzi wa nyumba 10,000, kuna baadhi ya majengo marefu ya kisasa ya ghorofa 30 yatakuwa kwa ajili ya makazi, ofisi na biashara. Tunaamini baada ya miaka michache ijayo mambo yatabadilika kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Nndunduma alisema kama hakutatokea pingamizi za kisheria, watahakikisha wanakamilisha majengo hayo saba ya kisasa yatakayogharimu Sh30 bilioni kwa kuzingatia Sheria ya Mipango Miji.

Ripoti ya CAG

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2012/2013 inabainisha kwamba kiasi cha Sh7.89 bilioni kilitumika kugharamia ulipaji wa kodi ya pango.

Katika ukaguzi uliofanywa kwenye wizara, idara na wakala 14 za Serikali kwa mwaka huo, CAG anasema zaidi ya Sh7 bilioni zilitumika kwa ajili ya kodi ya pango katika majengo ambayo baadhi yanamilikiwa na kampuni binafsi.

Pia, alisema Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ilitumia Sh1.04 bilioni; Idara ya Huduma za Habari Sh216 milioni; Wizara ya Ujenzi Sh484. 21 milioni; Tanroads Sh1. 433 bilioni na Mfuko wa Barabara Sh531.26 milioni.

Idara nyingine ni Tume ya Pamoja ya Fedha Sh159. 26 milioni; NEC Sh937.20 milioni; Kurugenzi ya Mashtaka ya Umma Sh654. 51 milioni; Mkulima wa Kisasa Sh81.12 milioni na Nida Sh1.42 bilioni.

Nyingine ni Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki (sasa iko chini ya Mambo ya Nje) Sh435. 59 milioni; Tume ya Utumishi wa Mahakama Sh129.71 milioni; Mahakama ya Kazi Sh116. 40 milioni; Mahakama ya Ardhi Sh258 milioni.

“Kuna umuhimu kwa Serikali kuwekeza katika ujenzi wa majengo yake yenyewe. Ninashauri Serikali kuwa na mpango endelevu wa kujenga majengo kwa ajili ya ofisi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wakala wa Majengo,” anasema CAG katika ripoti hiyo.

Pia, aliishauri Serikali kuhakikisha inafanya majadiliano na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, washirika wa maendeleo ikiwamo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia (WB) ili kupata mkopo au msaada kwa ajili ya kugharamia miradi ya ujenzi wa majengo hayo.


ZeroDegree.
Mtihani mwingine mgumu kwa Rais Magufuli. Mtihani mwingine mgumu kwa Rais Magufuli. Reviewed by Zero Degree on 1/20/2016 10:38:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.