Mv Serengeti yaanza safari Mwanza-Bukoba.
MV Serengeti
Mwanza. Meli ya Mv Serengeti inayofanya safari kati ya mikoa ya Mwanza na Kagera, imeanza tena kusafirisha abiria baada ya kusitisha huduma kwa muda wa siku nane kutokana na hitilafu za kiufundi.
Meli hiyo ilipata hitilafu katika mfumo wake wa shafti na majembe ya kulia tangu Januari 6, mwaka huu ikiwa safarini kutoka Mwanza kwenda Bukoba na kulazimika kutia nanga Bandari ya Bukoba saa sita mchana badala ya saa 12:00 asubuhi.
Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Mkoa wa Mwanza, Michael Rogers alisema wameiruhusu meli hiyo kuendelea na safari baada ya mafundi kufanikiwa kurekebisha kasoro zilizojitokeza.
Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Josephat Mshumbuce alisema wanaendelea kufuatilia safari za meli hiyo ili kuhakikisha usalama wa abiria.
Pamoja na kufurahia kurejea kwa huduma ya usafiri wa meli hiyo, baadhi ya abiria waliokutwa wakiingia melini waliiomba Serikali kuboresha huduma ya usafiri wa majini ndani ya Ziwa Victoria kwa kununua meli mpya. “Serikali itekeleze ahadi ya muda mrefu ya kununua meli mpya ya abiria katika Ziwa Victoria kwa sababu hii ya Mv Serengeti imechoka na inahitaji matengenezo makubwa,” alisema mkazi wa Bukoba, Petronila Amon.
ZeroDegree.
Mv Serengeti yaanza safari Mwanza-Bukoba.
Reviewed by Zero Degree
on
1/19/2016 08:13:00 PM
Rating: