Rais Magufuli ang’ata kila upande.
Rais John Pombe Magufuli
Dar/mikoani. Wapo wanaofurahia hatua za Serikali ya Awamu ya Tano (SAT) kudhibiti na kubana matumizi, lakini uamuzi huo umeathiri sekta nyingi kutokana na fedha kutoweka.
Hiyo ndiyo hali iliyolikumba Taifa kwa wakati huu ambao Serikali ya Rais John Magufuli inabana matumizi yasiyo ya lazima, huku ikidhibiti mianya ya ukwepaji kodi katika jitihada za kupata fedha za kutosha kutekeleza ahadi zake kwa wananchi ilizozitoa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Si hoteli, baa, mashirika ya usafiri, kampuni za huduma za chakula, wala za usafirishaji zilizoepuka athari hizo za uamuzi wa SAT kubana matumizi.
Kilio hicho kinalingana na kilichokuwapo mwanzoni mwa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa chini ya Rais Benjamin Mkapa, wakati wananchi walipoipachika hali ngumu ya maisha jina la “ukapa”.
Uamuzi huo mgumu ulitangazwa na Magufuli kwa nyakati tofauti mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Alitangaza kufuta safari za nje Novemba 7, 2015 wakati alipokutana na makatibu wakuu wa wizara na watendaji wa taasisi za Serikali, ikiwa ni siku chache baada ya kuapishwa.
Pia, katika hotuba yake bungeni Novemba 20, 2015, Rais alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi ambazo ni kudhibiti ziara za nje zisizo na tija, safari za mafunzo nje ya nchi, warsha, semina, makongamano na matamasha; kusimamia Sheria ya Manunuzi ya Umma, ununuzi wa samani, magari na kudhibiti matumizi ya Serikali.
Rais alitaja bayana taasisi zenye safari nyingi za nje kuwa ni Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Utekelezaji wa uamuzi huo sasa unaonekana kuanza kuathiri sekta tofauti.
“Awali biashara yetu ilitegemea watu kutoka serikalini, ambao walikuwa wakisafiri kwa makundi, lakini kutokana na Rais Magufuli kuzuia safari za nje, wamekuwa wakisafiri kwa vibali maalumu,” alisema mfanyakazi mmoja wa kampuni ya uwakala wa ndege aliyeomba jina lake lihifadhiwe na kuongeza: “Tunapata mteja mmoja au wawili pekee. Biashara imekuwa ngumu kiasi kwamba ndege moja ya Emirates iliyokuwa ikisafiri saa 5:00 usiku, imeondolewa na kubaki moja inayoondoka saa 10:00 jioni.”
Wakala huyo alisema licha ya kwamba Januari huwa na wateja wachache, kwa mwaka 2016 hali imekuwa mbaya zaidi na dalili zilionekana tangu Novemba mwaka jana walipoanza kupata wateja wachache.
Mwananchi lilipomtafuta meneja wa Emirates Tanzania, Abdul Aziz Alhai, alikataa kuzungumzia suala hilo akisema si msemaji na kwamba suala la kupunguza safari linaweza kujibiwa na mhusika ambaye hakumtaja.
Maofisa wa mashirika mengine ya ndege hawakutaka kuzungumzia suala hilo wakisema itakuwa kama wanaingilia maagizo ya Rais wa nchi.
Uamuzi huo pia umeikumba sekta ya huduma za vyakula ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ikitegemea semina, warsha na mafunzo kujipatia fedha baada ya zabuni za sherehe kama za harusi kushikiliwa na wamiliki wa hoteli na kumbi.
Huduma za chakula
Janerose Kintu wa kampuni ya huduma za chakula ya Mama Kintu Catering, alisema tegemeo lao kwa kiasi kikubwa lilikuwa semina na warsha mbalimbali hasa za taasisi za Serikali.
“Semina zilikuwa za aina mbalimbali za Serikali na sekta binafsi. Sasa zilipopigwa marufuku imekuwa kama tishio kwetu,” alisema Kintu na kuongeza:
“Sasa kwa sisi wengine ambao ni wajane kwa kweli inatisha. Huenda tukashindwa hata kusomesha watoto.”
Juliana Mtei, ambaye ana kampuni ya huduma za chakula ya Mama Mtei Catering, alisema alichoona ni kwamba mzunguko wa fedha umepungua kwa kiasi kikubwa.
“Wakati ule nilikuwa naweza kupata tenda hata nne kwa mwezi, lakini sasa hakuna kitu. Nilichobaini ni kwamba kuna hali ngumu kwenye maeneo mengi, siyo sisi tu,” alisema Mama Mtei.
Baa hali ngumu
Kasi hiyo pia imeonekana kutikisa kwenye biashara ya vileo ambako wamiliki wa baa wanasema wateja wamebadilisha tabia katika siku za karibuni.
“Kiukweli unywaji wa wateja umepungua sana, sielewi ndiyo hali ngumu au nini,” alisema Asha Gwandu wa baa ya Bilima Inn iliyopo Mtoni kwa Aziz Ali.
“Zamani mtu anaweza kunywa hata bia 15 na bado akatoa ofa, lakini siku hizi ni nadra kuwakuta watu wa namna hiyo,” alisema.
Meneja wa baa ya Triple E iliyopo Yombo jijini Dar es Salaam, Erick Onesmo alisema huenda hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na wafanyakazi wa Serikali na sekta mbalimbali kubana matumizi.
“Kuna masuala mawili nayaona hapa kwanza hali ngumu ya uchumi, Januari watu wametoka kulipa kodi na ada, hivyo ni nadra kuwakuta wakiburudika baa,” alisema Onesmo na kuongeza:
“Jambo jingine ni hii kasi ya Magufuli, maana wateja wanalalamika hali ngumu, pesa imekuwa adimu, hivyo inawalazimu kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.”
Hoteli zalia ukata
Kwa kiasi kikubwa hoteli ndizo zinaonekana kuathirika zaidi.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika hoteli tisa za Bagamoyo na Dar es Salaam umebaini kuwa katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili tangu SAT ishike hatamu, hoteli zimepoteza wateja wake wa uhakika, ambao ni taasisi za Serikali.
Hatua hiyo ya Magufuli imesababisha baadhi ya wamiliki wa hoteli kufikiria kuanza kupunguza wafanyakazi.
Meneja wa Hoteli ya Leopard iliyopo mjini Moshi, Priscus Tarimo alisema wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuzuiwa kwa vikao na mikutano hotelini na kwamba tangu agizo hilo litolewe hawajawahi kupata wateja.
“Kwa sasa wateja tunaopata ni wale wa taasisi na kampuni binafsi pekee. Kama hali hii itaendelea hivi, itatubidi tufanye maamuzi mengine ambayo ni pamoja na kupunguza wafanyakazi,” alisema Tarimo.
Meneja masoko wa Hoteli ya Kibo Home iliyoko mjini Moshi, Stanley Kimario, alisema kutokana na Serikali kuacha kufanya mikutano kwenye hoteli yao, baadhi ya wafanyakazi wamekosa kazi.
“Yaani hakuna kabisa biashara siku hizi kulinganisha na ilivyokuwa awali wakati wageni walikuwa wanakuja kulala hotelini kwetu. Kwa sasa ni kama ulivyotukuta, hakuna kazi, kuanzia asubuhi hadi jioni, ni hivi hivi tu tunakaa,” alisema Kimario.
Ingawa menejimenti za baadhi ya hoteli hazikuwa tayari kuzungumzia hali hiyo, wafanyakazi wake walieleza kuwa hali ya hoteli nyingi ni tete kutokana na kukosekana kwa shughuli hizo za Serikali huku kukiwa na hatari ya wao kupunguzwa.
Kati ya mikutano mitano hadi 20 ilikuwa ikifanywa na taasisi za Serikali kwenye hoteli moja.
Hoteli nyingi zilikuwa zikipokea kati ya watu 30 hadi 200 kwa kila mkutano huku kila mmoja akilipiwa kati ya dola 40 za Marekani hadi 135 kwa siku, mbali na malipo ya posho.
“Kwenye hoteli yetu kama wanasemina watatakiwa kupata chai, chakula cha mchana na usiku, kila mmoja anatakiwa kulipa dola 135 (Sh270, 000) kwa siku. Kama ni chai na chakula cha mchana tu, atalipa dola 42 (Sh84,000) tu,” alisema mmoja wa wahudumu wa hoteli moja iliyopo Bagamoyo.
Uchunguzi umebaini hoteli nyingine ambayo ilikuwa ikipokea hadi mikutano 20 kwa siku mjini Bagamoyo haijaambulia mkutano wowote tangu Serikali mpya iingie madarakani.
“Hakuna mkutano wa Serikali uliofanyika kwetu siku za karibuni, kwa sasa tunaambulia wateja wa kawaida tu wanaokuja mmoja mmoja. Zamani hadi mikutano 20 ilikuwa ikifanyika kwa wakati mmoja, na tuna kumbi hadi za kubeba watu 100,” alisema mmoja wa wahudumu wa hoteli hiyo.
Uamuzi huo wa kudhibiti semina na mikutano mahotelini, sasa unazifanya baadhi ya taasisi kufanya kwa siri. “Juzi kulikuwa na mkutano lakini uliendeshwa kisiri sana. Walitupa masharti ya kuhakikisha magari yao hayaonekani na tusiweke tangazo lolote ambalo lingewajulisha wapo hapa,” alisema muhudumu wa hoteli nyingine ambaye aliomba jina lake lisitajwe na kuongeza:
“Walikaa siku tano na kuondoka. Hii kasi ya Magufuli ndiyo iliyotuletea balaa.”
Dar es Salaam
Tofauti na ilivyo kwa Bagamoyo, katika hoteli za Dar es Salaam baadhi ya wafanyakazi walisema hawategemei mikutano ya Serikali, hivyo kupungua kwake, hakutawaumiza.
“Hoteli yetu ni ya kitalii kuna wageni wengi wanakuja na mikutano mingi ya taasisi binafsi inaendelea kufanyika. Hatutegemei sana mikutano ya Serikali ndiyo maana hatujashuka sana kama wenzetu,” alisema mfanyakazi mmoja.
Hata hivyo, katika hoteli nyingine tatu za Giraffe, White Sands na Serena, kilio cha wafanyakazi ni kutokuwapo kwa mikutano, semina na warsha za Serikali huku wengi wakihofia ajira zao.
Nyumba za wageni zaathirika
Kilio cha hoteli za kitalii kukosa shughuli hizo kumeathiri nyumba za wageni zilizokuwa zikitegemea wateja waliokuwa wakitaka kubana fedha. “Bagamoyo tulikuwa hatukosi wageni hata siku moja, lakini kwa sasa inaweza malizika siku hakuna cha mgeni na kama wakija ni wale binafsi wanaokuja kwenye kazi za kawaida,” alisema mhudumu wa moja ya nyumba za kulala wageni Bagamoyo.
Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Rais Magufuli ang’ata kila upande.
Reviewed by Zero Degree
on
1/21/2016 11:35:00 AM
Rating: