Zaidi ya makampuni 980 kuilipa Serikali Sh16 bilioni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dk Servaciaus Likwelile.
Dar es Salaam. Serikali inatarajia kukusanya Sh16 bilioni kupitia kampuni zaidi ya 980 zilizokopeshwa fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza bidhaa na malighafi kutoka nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 1980 hadi 2004.
Kiasi hicho cha fedha kitakusanywa na Kampuni ya M/S Msolopa Investment Ltd iliyoingia mkataba wa miaka miwili na Wizara ya Fedha na Mipango.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana na Wizara hiyo, fedha hizo zilitolewa kupitia wahisani mbalimbali kwa ajili ya mpango maalumu uliofahamika kama ‘Commodity Import Support’ (CIS) uliolenga kuipatia Serikali uwezo wa kuimarisha uchumi wake kupitia taasisi, kampuni, viwanda na biashara mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msolopa Investment Co Ltd, Ibrahim Msolopa alisema ni mara ya pili kwa kampuni yake kuingia mkataba na wizara hiyo, wa kwanza ulikuwa mwaka 2008 hadi 2011.
“Mkataba wa kwanza tulikusanya Sh4 bilioni kutoka kampuni 70, lakini baadaye tulisitisha mkataba kutokana na wizara kurekebisha sheria ambayo hapo awali ilikuwa hairuhusu sisi kumkamata mtu ambaye amekaidi kulipa, lakini baada ya sheria hiyo kuboreshwa sasa tuna uwezo wa kumkamata,” alisema Msolopa.
Hata hivyo, katika tangazo hilo lililosainiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Servacius Likwelile, linaeleza kuwa hata kama mkopaji alichelewa kulipa katika kipindi cha miezi 18, mkopo huo unakuwa na kufikia asilimia 17.
CIS ni Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi, ambao ulikopesha fedha za kigeni kwa baadhi ya wafanyabiashara wazalendo.
Mpango huo ulianzishwa na Serikali katika miaka ya 1980 na kudumu hadi mwaka 2000.
Fedha zake zilitoka nchi wahisani ikiwamo Japan, Uingereza, Uholanzi, Saudi Arabia, Uswis, Norway, Denmark na Ubeligiji.
Lengo la fedha hizo za kigeni ilikuwa ni kuimarisha sekta ya biashara.
Source: Mwananchi
Comment & Share this!!
Zaidi ya makampuni 980 kuilipa Serikali Sh16 bilioni.
Reviewed by Zero Degree
on
1/07/2016 01:44:00 PM
Rating: