Loading...

Serikali kuwapatia UHAMISHO WANAFUNZI WALIOKOSA makazi.


Wakati shule za umma za msingi na sekondari zikifunguliwa leo nchini, Serikali imesema itaanda utaratibu wa kuwasaidia kupata uhamisho wanafunzi ambao makazi ya wazazi wao yamekumbwa na bomoabomoa jijini hapa.


Pia, imesema itafanya utaratibu wa kutoa maeneo mengine kwa wakazi waliovunjiwa nyumba zao waliokuwa na hati.

Kauli hiyo ilitolewa jana wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba baada ya kutembelea maeneo ya Kinondoni Mkwajuni, Buguruni Mivinjeni na maeneo ambayo nyumba zimewekwa alama za X kwa ajili ya kubomolewa.

“Nimetoa agizo kwa viongozi wa Serikali za Mitaa watoe taarifa ya wanafunzi wote waliokuwa wanaishi maeneo ambayo nyumba zimebomolewa ili tufanye utaratibu wa kuwaandikisha upya kwenye makazi yao mapya,” alisema.

Alisema utaratibu huo utarahisisha mchakato wa uhamisho kwa ajili ya wanafunzi kuendelea na masomo yao kwa wakati kuliko wazazi kufanya wenyewe.

Ingawa hakuna takwimu kamili, Desemba 28, mwaka jana wakati utekelezaji wa operesheni hiyo ulipokuwa umefikisha siku 12, ilielezwa kuwa zaidi ya wanafunzi 70 wa shule za msingi na sekondari huenda wakashindwa kuendelea na masomo kutokana na familia zao kubomolewa nyumba.

Mjumbea wa shina la Kawawa (CCM) ambaye pia ni mjumbe wa Serikali ya mtaa wa Mkwajuni, Erasto Mayani aliliambia gazeti hili kuwa wanafunzi hao wangeshindwa kuendelea na masomo kutokana na athari za bomoabomoa.

Maeneo kwa wenye hati

Mbali na suala hilo, Makamba pia alisema Serikali itawapatia maeneo mengine wakazi ambao nyumba zao zilibomolewa, lakini walikuwa na hatimiliki.

Alisema kati ya nyumba 774 ambazo zimeshabomolewa ni 20 ambazo zimebainika wamiliki wake walikuwa na hati.

“Kwa sababu walikuwa na hati hiyo ni dhahiri kwamba Serikali ilitoa kibali kwao na kama ndiyo hivyo basi itawalipa…hao wangine hatuhusiki nao,” alisisitiza Makamba.

Alisema operesheni bomoabomoa itaendelea kufanywa kwa makazi yaliyojengwa katika bonde la Mto Msimbazi na kingo zake.

“Tutafanya kwa utaratibu wa wazi. Tutawaangalia wenye mahitaji maalumu, lakini wenye ubishi hatutawaacha. Baada ya siku tatu ya kutoa notisi kama hawajaondoka tunavunja,” alisema.



Source: Mwananchi

Comment & Share this
Serikali kuwapatia UHAMISHO WANAFUNZI WALIOKOSA makazi. Serikali kuwapatia UHAMISHO WANAFUNZI WALIOKOSA makazi. Reviewed by Zero Degree on 1/11/2016 06:26:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.