Loading...

Serikali yafuta umiliki wa mashamba 17.


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akizungumza alipotembelea ofisi ya Idara ya Ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani jana, alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja. Kulia ni Ofisa Ardhi mteule wa Halmashauri hiyo, Majaliwa Jafari. 

Kibaha. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema Serikali imefuta umiliki wa mashamba 17 ambayo hayajaendelezwa katika Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na viongozi wa mkoa huo, Lukuvi alisema Serikali imefuta mashamba hayo baada ya mkoa kutoa mapendekezo ya kutaka yafutwe kwa sababu hayajaendelezwa.

“Baada ya kupata mapendekezo ya mkoa tumefuta miliki ya mashamba lakini wamiliki ni wananchi wa kawaida, mbona vigogo wenye mashamba yasiyoendelezwa hamjawagusa, mnawaogopa? ” aliwahoji viongozi hao.

Lukuvi aliagiza ukaguzi ufanyike kwenye mashamba yote mkoani na kutoa mapendekezo kwa wizara ili yafutwe bila kuangalia cheo wala rangi ya mtu.

Alisema migogoro ya ardhi haiwezi kumalizika kama viongozi watakuwa wanafanya kazi kwa kuangalia vyeo vya watu.

“Msimuogope mtu hata kama ni kigogo lakini msimuonee mtu, tendeni haki,” alisema.

Lukuvi alisema kuna wamiliki 35 wa mashamba mkoani humo ambao wametumia hati za mashamba hayo kukopa mamilioni ya fedha benki, lakini fedha hizo wamezitumia kwenye miradi mingine isiyo na uhusiano wa mashamba hayo.

Alisema pamoja na kukopa fedha hizo, lakini mashamba waliyotumia kupata mikopo wameyatelekeza bila kuyaendeleza.

“Wako watu wamekopa kwa kutumia mashamba ya Mkoa wa Pwani lakini fedha walizopata wamekwenda kujenga nyumba za kupangisha Kigamboni (Dar es Salaam) na mashamba hawayaendelezi tutawanyang’anya,” alisema.

Lukuvi alisema atatoa orodha ya watu hao kwa uongozi wa mkoa ili uweze kuyakagua na kutoa taarifa kwa wizara.

“Hatuwezi kuwatajirisha watu wa Dar es Salaam kwa kutumia mashamba ya Mkoa wa Pwani,” alisema.

Lukuvi alitoa orodha ya mashamba 50 ambayo yamenunuliwa kwenye vijiji vya mkoa huo, lakini hayajaendelezwa na kusababisha migogoro ya ardhi.

“Kutoendeleza mashamba kunasababisha migogoro ya ardhi kwani hivi sasa kuna watu wanayavamia,” alisema.

Bei elekezi ya viwanja

Waziri alisema wizara itatoa bei elekezi katika uuzaji wa viwanja kwa lengo la kupunguza bei.

Alisema hivi sasa halmashauri zimekuwa zikichukua mashamba na kupima viwanja na kuviuza kwa mamilioni ya fedha ambayo si rahisi kwa mwananchi wa kawaida kumudu.

Alisema matokeo yake, viwanja hivyo vimekuwa vikinunuliwa na matajiri kwa malengo ya kuviuza kwa bei kubwa huku watu wa kawaida wakiendelea kujenga kwenye maeneo yasiyopimwa.

“Halmashauri msifanye biashara katika viwanja, hii ni huduma sasa tunaweka bei elekezi ili kila mwananchi aweze kununua,” alisema.

Alizitaka halmashauri zilizochukua mashamba ya watu na kuyapima viwanja kuwalipa fidia kabla ya Juni.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mgeni Baruani alimueleza waziri kwamba mkoa huo una migogoro ya ardhi hasa zile zinazopakana na Mkoa wa Dar es Salaam.


Source: Mwananchi
Serikali yafuta umiliki wa mashamba 17. Serikali yafuta umiliki wa mashamba 17. Reviewed by Zero Degree on 1/12/2016 11:02:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.