Fatma Karume: Maana ya Mapinduzi imepotea Zanzibar
Fatuma Karume
Mwanaharakati wa Marekani, Huey Newton alisema: “Mapinduzi siku zote yapo mikononi mwa damu changa. Ni vijana tu ndiyo huyarithi na kuyafaidi mapinduzi.”
Hakika maneno ya Newton yanasadifu kwa kiasi kikubwa kauli ya Fatma Karume, Wakili wa Kampuni ya Uwakili ya IMMMA, ambaye pia ni mtoto wa rais wa zamani wa Zanzibar, Abeid Aman Karume.
Wakati leo tukisherehekea miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Fatma anasema: “Huu ni wakati sahihi kwa Serikali na Wazanzibari kujitathmini kama kweli tunaienzi mbegu ya mapinduzi.”
Anasema Wazanzibari wengi hawaijui Zanzibar ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi,bali wanaifahamu baada ya Mapinduzi.
Hivyo hawaelewi madhumuni yake kwa sababu hawajaiona kabla na baada ya mabadiliko hayo.
“Nasimuliwa na wakubwa zangu tu kwamba mimi nimezaliwa baada ya Mapinduzi, lakini naambiwa hapo zamani Zanzibar ilikuwa na mchanganyiko wa watu wa makabila mbalimbali,” anasema.
Anasema zamani, kabla ya Mapinduzi kulikuwa na makundi mchanganyiko ya Waafrika, Waarabu, Wahindi, Washirazi, (asili yao ni Persia) kwa sababu Zanzibar ilikuwa ni kituo kikuu cha biashara.
Fatma anaeleza kuwa mchanganyiko huo ulisababisha kuwapo kwa ubaguzi na ilikuwa vigumu kuwapo kwa ndoa za muingiliano, hakikuwa kitu cha kawaida katika jamii hiyo.
“Ninayafahamu Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na Amri namba 6 iliyotolewa Februari 25 mwaka 1964 na Baraza la Mapinduzi. Baada ya Mapinduzi Zanzibar iliendeshwa na Baraza la Mapinduzi, pamoja na waliohusika kumpindua Sultani,” anasema.
Anasema amri hiyo ilieleza kuwa madhumuni ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuondoa ubaguzi wa aina yoyote masuala wa kiuchumi, kisiasa, kijamii na kisheria ambao hapo awali uliwagawa wananchi badala yake kuhimiza usawa, upatanisho.
Fatma anasema pia amri hiyo ilitaka kila mwananchi apate haki yake kama Mzanzibari.
“Ina maana kwamba, kutokana na amri hiyo madhumuni ya Mapinduzi yalikuwa ni kila Mzanzibari kupata haki sawa, Mswahili, Mwarabu, Mhadimu na Mshirazi,” anasema.
Fatma anasema madhumuni ya Mapinduzi yalikuwa kuhimiza umoja na mshikamo na kuchukua madaraka kutoka kwenye utawala wa kisultani na kuyaleta mikononi mwa wananchi.
“Tulihama kutoka kwenye uongozi wa kisultani na kuwa na Serikali yenye umoja na usawa kama yalivyo mapinduzi yoyote na ndiyo madhumuni yake hivyo ninavyoyaelewa,” anasema.
Malengo ya Mapinduzi yamefutika
Hata hivyo, Fatma anasema kwa sasa malengo ya Mapinduzi hayapo visiwani humo kutokana na sababu mbalimbali kubwa ikiwa ni pamoja na ubaguzi unaoendelea.
“Zanzibar hatuyasherehekei Mapinduzi na wala hatutimizi malengo yake kwa sababu kuna ubaguzi. Ubaguzi wa aina yoyote ni dhambi kubwa, hakuna kitu kibaya kama ubaguzi, ni kansa kwenye uongozi, ni kitu kibaya,” anasema.
Anasema mataifa yaliyoendelea yanakemea ubaguzi, lakini baadhi ya viongozi visiwani Zanzibar wameonekana kuupalilia ubaguzi ili waendelee kubaki madarakani.
Anasema ubaguzi huo unapaliliwa baina ya watu wa Unguja, Waarabu na Waafrika.
“Ubaguzi ukifanywa na Wazungu ni mbaya, lakini ukifanywa na Waafrika unaoenakana ni mzuri. Haiwezekani, hata ukiwa Mwafrika, ubaguzi ni mbaya, hiki ni kitu kibaya,” anasema.
Anasema ubaguzi ambao ulipingwa wakati wa Mapinduzi, unaonekana hata hapa Tanzania Bara. Anatoa mfano wa aliyekuwa mrembo wa Tanzania (Miss Tanzania), Richa Adhia akisema alipingwa kwenda kwenye mashindano ya dunia na kuonekana hawezi kuiwakilisha Tanzania kwa kuwa ana asili ya India.
“Lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ni kuondoa ubaguzi wa kila aina, lakini walio madarakani wanadhani wana haki ya kubagua kulingana na rangi,” anasema.
Fatma anasema: “Zanzibar ni sawa na chungu chenye kila kitu, kuna mchanganyiko mkubwa wa wahamiaji, kila mtu anakaribishwa. Kwa nini ubaguzi kuwapo.”
CCM haitakiwi kukaa madarakani milele
Anasema wakati tunasherehekea miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar leo ni lazima walio madarakani watambue kuwa madhumuni yake hayakuwa kuiweka CCM madarakani milele.
“Najisikia kusalitiwa, Mapinduzi yalifanyika wakati CCM haikuwapo, ilikuwapo ASP, lakini ASP haikupanga iwe madarakani milele, mimi nasimuliwa kuwa babu yangu aliwahi kusema; “Utafika wakati Zanzibar itatakiwa kuwa tayari kwa mfumo wa vyama vingi.”
Anasema: “Babu yangu aliyeyafanya hayo Mapinduzi, alikuwa anajua kuwa ASP haitakaa madarakani milele. Alikuwa anafahamu kuna wakati watu watachagua nani abaki madarakani. Huyu ni mwanaume ambaye pia aliamini demokrasia ndiyo mfumo wa Serikali.”
Anasema ingawa Mzee Abeid Karume alikuwa na uwezo wa kuamrisha kwamba ni lazima Serikali ibaki madarakani milele, lakini alikadiria ndani ya miaka 50 kuwe na mfumo wa vyama vingi.
“Lakini leo hii kuna watu ambao hawakushiriki Mapinduzi ya Zanzibar, lakini wanajitaja kuwa ndiyo warithi wa Mapinduzi na wanasimama hadharani wakisema hawajaipata Serikali kwa karatasi hivyo hawataitoa kwa karatasi,” anasema.
Fatma anaenda mbali na kusema hayo si malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar bali malengo yalikuwa ni kurejesha nguvu kwa wananchi.
“Ni hatari, ni hatari sana, Mapinduzi si kitu chepesi, nchi zilizopitia zinajua hili, utaona kuwa hiki si kitu cha kuchukuliwa kwa wepesi, taasisi zinabadilika, watu wanabadilika, ni mpasuko,” anasema.
Anasema ni jambo la ajabu kuona viongozi wa CCM, hata Mwenyekiti wake hajachukua hatua na kukanusha maneno yanayosemwa na wanachama wa chama hicho.
“Mtu anasema hatukuipata nchi kwa karatasi na hatuwezi kuitoa kwa karatasi, lakini viongozi wake wala hawajitokezi kukanusha. Si vizuri kusikia maneno kama haya,” anasema.
Uchaguzi Mkuu 2015, Zanzibar
Fatma anazungumzia uchaguzi uliofutwa na kutangazwa kurudiwa tena visiwani humo akisema CCM itaendelea kupoteza watu kwa sababu imeshindwa kuwashawishi.
“Siasa ni ushawishi, kama umeshindwa kuwashawishi badala yake unawapelekea jeshi, unawapiga virungu ni dhahiri utawapoteza,” anasema.
Anasema mwanasiasa yoyote huvuna kile alichokipanda baada ya miaka mitano akidai hicho ndicho alichovuna Dk Ali Mohamed Shein katika uchaguzi uliopita Oktoba 25, mwaka jana.
Source: Mwananchi
Fatma Karume: Maana ya Mapinduzi imepotea Zanzibar
Reviewed by Zero Degree
on
1/12/2016 11:07:00 AM
Rating: