Ugonjwa wa ajabu hatarini kuingia nchini
Dar es Salaam. Virusi hatari vinavyosababisha ugonjwa wa Zika vinaendelea kusambaa kwa kasi duniani, huku Mganga Mkuu Serikali, Profesa Muhammed Bakari akitoa tahadhari kuwa unaweza kuingia nchini.
Tahadhari hiyo inatolewa wakati ikiwa imebainika kuwa mbu wanaoeneza virusi vya Zika, Aedes Egyptiae ni wale wanaosababisha homa ya dengue, ugonjwa ulioenea nchini mwaka 2014 kabla ya kudhibitiwa, na Chikungunya mwaka 1952.
Virusi vya Zika si vipya duniani, lakini madhara yake ni mapya kwa kuwa sasa vinawaathiri watoto wanaozaliwa na wajawazito walioumwa na mbu hao.
Kwa mara ya kwanza ugonjwa huo uligundulika barani Amerika na umekuwa ukisambaa kwa kasi. Hadi leo tayari matukio ya ugonjwa huo yameshaonekana kwenye nchi 23 za bara hilo.
Zika, inayohusishwa na madhara makubwa kwa watoto wanaozaliwa Brazil, unaweza kusambaa kwa watu milioni nne barani Amerika, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mbu huyo anapomuuma mjamzito huweza kuzaa watoto wenye matatizo ya ubongo ikiwamo kuwa na vichwa vidogo (microcephaly)
Profesa Bakari alisema mbu hao wapo nchini na inawezekana ugonjwa huo ukaingia hasa katika kipindi cha mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha.
“Hili jambo tuliliona na ndiyo maana mikakati ya kupambana na mbu inaendelea hasa katika kipindi cha mvua. Tulishatoa taarifa za tahadhari za kuangamiza mazalia ya mbu,” alisema.
Alisema tahadhari nyingine ni kwa watu wanaosafiri kuwa makini na mbu ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nchini.
“La msingi ni hilo tuangamize mazalia ya mbu na nyinyi wanahabari mtusaidie kutoa elimu,” alisema.
Jana, WHO ilitoa taarifa kuwa ugonjwa huo unasambaa kwa kasi kubwa katika kipindi kifupi.
“Wasiwasi ni mkubwa kama kilivyo kiwango cha sintofahamu. Tunahitaji majibu ya haraka sana,” alisema mkurugenzi mkuu wa WHO, Dk Margaret Chan.
Kadhalika Dk Chan alitahadharisha kuwa mbu wataongezeka zaidi mwaka huu kutokana na mvua za El Nino ambazo zinatarajiwa kunyesha.
Uhusiano wa Dengue, Zika na Chikungunya
Dengue na Chikungunya ni magonjwa yanayofanana na yanayosababishwa na mbu aina ya Aedes (Aedes aegypti na Aedes albopictus) ambao wanatajwa kuishi zaidi katika maji yaliyotuama, hasa kwenye nchi za kitropiki. Mbu huyo ndiye anayehusishwa pia na ugonjwa wa Zika.
Mei mwaka jana, ugonjwa wa homa ya dengue ulilipuka nchini na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 50. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ilitoa takwimu zilizoonyesha kuwa watu waliougua dengue walikuwa 376.
Daktari wa WHO, Sylvain Aldighieri alisema makadirio ya maambukizi ya Zika yanatokana na taarifa za maambukizi ya virusi vya dengue ambao unashabihiana kitabia na Zika. Tangu Mei mwaka jana, nchi zilizo kusini mwa Bara la Amerika zimekumbwa na homa ya Zika, Brazil pekee ilikuwa na kesi 4,000 za watu walioambukizwa ugonjwa huo.
ZeroDegree.
Ugonjwa wa ajabu hatarini kuingia nchini
Reviewed by Zero Degree
on
1/30/2016 05:25:00 PM
Rating: