Loading...

Aliyezikwa na kreti za bia aacha maswali mengi.


Mjane wa Marehemu Murashi Lutaja, Tabu Mazinge,(kulia) akizungumza na mwandishi wa habari wa Mwananchi Mkoa wa Shinyanga, Shija Felcian (katikati), nyumbani kwake katika kijiji cha Mwamande wilayani Kahama. Kushoto ni Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Oswald Lukunja. 

Familia ya Marashi Lutaja (61), aliyefariki wilayani Kahama na kisha kuzikwa katika Kijiji cha Mwamande na mali zake yakiwamo masanduku ya bia na soda, imeibuka na kudai kabla ya kifo chake, aliacha wasia ulioelekeza mazishi yake.

Katika mahojiano na mwandishi wa gazeti hili, mjane wa pili wa Lutaja, Tabu Mazinge (55), anasema mumewe aliacha wasia huo ulioeleza yeyote atakayerithi mali hizo naye atakufa.

Hata hivyo, Tabu anasema wosia huo haukufafanua zaidi.

“Alitoa hadhari hiyo bila kueleza sababu ya kuzikwa na mali zake, nasi tuliheshimu maelekezo yake aliyotoa kila wakati alipokuwa mgonjwa, maana aliugua kwa zaidi ya miaka mitano na shughuli zote za uzalishaji mali zilisimama,” anasema Tabu.

Lutaja alifariki dunia mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini wakati wa mazishi yake alizikwa na mali zake zikiwamo baiskeli mbili, masanduku ya bia, soda, vitanda vinne na magodoro yake pamoja na mabegi ya nguo.

Hata hivyo, Lutaja aliyekuwa akiishi na mke wake mdogo eneo la makao makuu ya Kata ya Mwanase kabla ya mke huyo kufariki, alihamia Kijji cha Mwamande walipokuwa wakiishi wake zake wawili akiwa na mali hizo.

Kwa mujibu wa Tabu, Lutaja alirejea kijijini hapo akiwa mgonjwa, na wakati wote wa kuuguza alikuwa akiwaambia kwamba mali zote alizokuja nazo hazipaswi kurithiwa na mtu yeyote katika familia yake.

“Kabla ya kifo chake, Lutaja alisisitiza mali zake zote kutorithiwa na mtu yeyote na katika kifo chake alikataza mtu yeyote kulia au kusononeka. Alizuia wanawake wote kufika kwenye kaburi lake wakati wa kuzikwa kwake,” anasema Tabu.

Anasema mbali na kauli hiyo, mume wake pia alitoa maelekezo ya kumzika nje ya eneo analoishi, na baada ya kuzidiwa aliomba apelekwe kwa mke mkubwa, huku akisisitiza kwa kumtaka kutokuwa na tamaa ya kurithi mali hizo, na kuzuia watu watakaofuata mali zake.

“Kwa kweli kauli zake hata sisi zilitutia mashaka, hatutamani tena mali zake, tuliziogopa kwa kuwa hatukujua alikotoka nazo alizipataje. Kauli zake kwamba akifa azikwe na mali zake tuliziheshimu hata alipokufa kila kilicho chake alizikwa nacho,” anasema Tabu.

“Lutaja alipokuwa Kijiji cha Mwanase, mke wake wa tatu alikuwa akifanya biashara ya kuuza vinywaji (baa) na baada ya mwanamke huyo kufariki alifungasha vitu vyote na kurudi navyo kwetu na aliweka makazi kwangu kabla ya kuzidiwa na kuomba apelekwe kwa mke wake wa kwanza, ambako alifariki dunia,” anasema Tabu.

Anasema mumewe huyo alizikwa kimila na hapakuwa na kiongozi yeyote wa kidini.

Mwandishi wa gazeti hili hakufanikiwa kumpata mjane mkubwa wa Lutaja, huku mtoto wake mmoja akikimbia baada ya mwandishi kufika nyumbani hapo kwa kuongozana na viongozi wa Serikali ya kijiji hicho.

Kukimbia kwa kijana huyo katika familia hiyo kulisababisha hofu kwa watoto waliobaki, ambao umri wao bado mdogo na hawakuweza kuzungumza chochote juu ya tukio hilo.

Kwa mujibu wa mashuhuda, kaburi la Lutaja lilichimbwa kwa takriban siku nzima, kazi iliyofanywa na wakazi wa kijiji hicho likikadiriwa kuwa na ukubwa unaoweza kufikia mita tano za mraba.

Baada ya mazishi yaliyofanyika mbali na eneo lake kama alivyoagiza kupitia wosia wake, kaburi la Lutaja lilifukiwa na kujazwa udongo kama kichuguu.

Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Oswald Lukunja anawataka wenyeviti wa vitongoji katika eneo hilo kutoa elimu kwenye familia hiyo akieleza tukio la kukimbia kwa kijana huyo linaleta hofu juu ya tukio zima la Lutaja kuzikwa na mali zake kinyume na maadili na utu wa binadamu.

“Kifo hicho kina mashaka kwenye familia hiyo kwa kuwa baada ya kuzikwa na mali hizo na tukio hilo kutangazwa kwenye vyombo vya habari, walikimbia na kuhama nyumbani kwao hata baada ya Ofisa Mtendaji wa kata hiyo kwenda kuwasihi warudi, hawakuwa tayari,” anasema Lukunja.

Anasema kuna hofu ya kiimani juu ya marehemu Lutaja kuzikwa na mali zake, na ndiyo sababu ya mtoto wake kukimbia baada ya kuona watu wenye sura ngeni wanakwenda nyumbani kwake.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Paul Shilinde amewataka viongozi wa dini na wanasiasa kutumia mikusanyiko ya watu kutoa elimu kwa jamii, akisema mtu kuzikwa na mali zake kunachangiwa na imani potofu inayoendekeza ushirikina.

“Suala hili liko kiimani zaidi kwa kuwa kuna imani potofu zimeingilia, lakini familia hiyo ingekuwa na dini kwa kumwamini Mungu wasingefanya hayo, hawana imani yoyote kuhusu uwezo wa Mungu ndiyo sababu walifanya hayo ambayo sijawahi kuyaona,” anasema Shilinde

Tukio la kuzikwa na mali zake kwa marehemu huyo limekuwa la aina yake na kuacha gumzo katika maeneo mbalimbali nchini, baada ya vyombo vya habari kuandika habari za hali ilivyokuwa kwa familia ya marehemu huyo aliyeacha watoto na wajukuu 32.

Maelezo ya tukio hilo yanafuatia taarifa za mazishi ya Lutaja kuandikwa na gazeti hili Januari 27.

Habari ilivyoandikwa

Wakati Serikali ikipigia kelele kukemea imani za kishirikina, wilayani Kahama bado ni kitendawili baada ya mkazi wa Kijiji cha Mwamande, Kata ya Mwanase Halmashauri ya Msalala kufariki na baadaye wanakijiji kumzika na mali zake zote yakiwamo makreti ya bia na soda aliyokuwa akiyatumia kwenye biashara yake ya baa.

Tukio hilo limetokea katika kijiji hicho baada ya mwanakijiji huyo, Lutaja kufariki na baadaye familia yake kupitisha maazimio ya kumzika na mali zake zote kwa imani ya kwamba kifo chake kimetokana na kurogwa na wao kuhofia wakibaki na mali zake nao watakumbwa na mauti.

Kwa mujibu wa diwani wa Kata ya Mwanase, Samson Masanja, Lutaja baada ya kifo chake alizikwa na baisikeli, vitanda vinne, magodoro, masanduku ya nguo zake zote na vitu vingine alivyokuwa akivitumia.

Alisema Lutaja alizikwa na makreti ya bia na soda ambayo kabla ya kifo chake alikuwa akiyatumia kwenye biashara yake ya kuuza vinywaji kwenye kijiji hicho cha Mwamande.

Wakati akiugua ndugu zake waliamini ugonjwa uliosababisha kifo chake ulitokana na kurogwa.

Source: Mwananchi






ZeroDegree.
Aliyezikwa na kreti za bia aacha maswali mengi. Aliyezikwa na kreti za bia aacha maswali mengi. Reviewed by Zero Degree on 2/08/2016 09:48:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.