Loading...

Serikali kuwasaka wahusika wa ukeketaji jijini Dar.


Wanafunzi wakiwa kwenye maandamano ya kuadhimisha siku ya kupinga Ukeketaji yaliyoanzia viwanja vya Mwalimu Nyerere hadi Mtaa wa Njejengwa mjini Dodoma jana. 



Dar es Salaam. Serikali imesema inawasaka ngariba katika maeneo mbalimbali jijini hapa wanaodaiwa kuwakeketa watoto wa kike kwa siri.

Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Familia wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Rose Minja alitoa taarifa hiyo juzi katika siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji wa wanawake nchini.

Minja alisema msako huo, unafanywa baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa watoto husafirishwa kutoka mikoani hadi jijini hapa na kufanyiwa ukeketaji katika maeneo ya Banana, Ukonga na Kitunda.

Ngariba hao wanadaiwa kuwafanyia ukeketaji watoto kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwamo Mara na Geita.

Juzi, Shirika la Plan International liliandaa maandamano kupinga ukeketaji huo chini ya mradi wake wa Youth for Change uliowashirikisha vijana kuhamasisha vita dhidi ya ukeketaji.

Akizungumzia mbinu za ngariba hao Minja alisema wizara inazifahamu ikiwamo ile ya kuwakeketa wakiwa wachanga.

“Tunafanya kazi na kamati za malezi ya mtoto katika kila mkoa, ndiyo maana huko Singida watoto wa kike wanachunguzwa wakipelekwa kliniki ili kujua kama wamefanyiwa ukatili huo kwa sababu Singida inaongoza kuwakeketa watoto wa kike wachanga,” alisema.

Kuhusu utendaji wa Serikali, Minja alisema baadhi ya ngariba wameshakamatwa na kufunguliwa kesi huku sera na sheria zikiendelea kuchukua mkondo wake.

Alisema Serikali inawajibika kupinga ukeketaji na kwamba Sheria na 21 ya mwaka 2009 na ile ya makosa ya kujamiiana zikitumiwa vyema katika masuala ya ndoa za utotoni na ukeketaji zitatokomeza ukatili huo.

Mwanaharakati wa Mradi wa Youth for Change, Aristarick Joseph alisema ukeketaji bado ni tatizo kwani takwimu za mwaka 2010 zinaonyesha kuwa asilimia 15 ya wanawake bado wanakeketwa.

“Mikoa ya wafugaji hasa Arusha na Manyara bado ina takwimu za juu za ukeketaji ndiyo maana tunafanya kila jitihada ikiwamo maandamano kama haya kupinga ukeketaji,” alisema.

Maadhimisho ya mwaka huu yaliongozwa na kauli mbiu isemayo, ‘Kutokomeza ukeketaji kwa maendeleo endelevu ifikapo 2030.’


Source: Mwananchi




ZeroDegree.
Serikali kuwasaka wahusika wa ukeketaji jijini Dar. Serikali kuwasaka wahusika wa ukeketaji jijini Dar. Reviewed by Zero Degree on 2/08/2016 09:55:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.