Loading...

Bilioni 277 zatumika kununua umeme IPTL na Aggreko.



Dar es Salaam. Serikali imetumia Sh277 bilioni kununua umeme mwaka jana katika kampuni za kufua nishati hiyo za IPTL na Aggreko, hivyo kusababisha bei yake kubaki juu licha ya kushuka kwa bei ya mafuta duniani. 

Hayo yalieleza wiki iliyopita na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini baada ya kuulizwa na wabunge kuhusu masuala mbalimbali likiwamo la upotevu wa mafuta bandarini. 

Habari za ndani kutoka katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa LAPF, Kijitonyama, Dar es Salaam, zinaeleza kuwa suala la bei ya umeme liliibuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Bupe Mwakang’ata, aliyehoji kutoshuka wakati bei ya mafuta yanayotumika katika mitambo ya kuuzalisha imeshuka. 

Katika majibu yake, Ewura ilieleza kuwa bei hiyo ilipangwa kwa mwaka 2014-2016 kwa kuzingatia mambo matatu; matumizi ya umeme unaozalishwa kutokana na maji kwa kiwango cha wastani, bei ya mafuta kuwa ya Sh1,186, mafuta mazito Sh1,707 na bei ya gesi asilia ambayo ni dola 3.34. 

“Mwaka 2015 bei ya umeme haikupungua kutokana na uhaba wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme hata kusababisha mitambo ya Mtera kuzimwa, ililazimika kuzalisha umeme wa mafuta kwa kiwango kikubwa kuliko ilivyotegemewa na kununua umeme wa mitambo ya dharura,” alieleza Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix. Ngamlagosi katika majibu kwa kamati. 

Aliongeza: “IPTL na Aggreko hazikujumuishwa katika kupanga bei, lakini Tanesco ililazimika kununua uniti 580,282,870 zilizogharimu Sh277.4 bilioni kutoka katika kampuni hizo. Hivyo bei ya umeme haikushuka kutokana na gharama hizo. 

Mbunge wa Chonga (CUF), Mohamed Juma Khatib alihoji kuhusu upotevu wa mafuta bandarini na kujibiwa na Ngamlagosi kuwa unasababishwa na miundombinu na watu na kwamba Serikali imeunda tume inayowahusisha wajumbe kutoka katika wizara na taasisi mbalimbali kushughulikia suala hilo. 

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Maryam Msabaha alihoji hatua zaidi zitakazochukuliwa na Ngamlagosi alijibu: “Ewura imeandaa kanuni ambazo zitatumika kutoa leseni na kudhibiti miundombinu ya kupokelea mafuta kwenye bandari ili kuhakikisha inakuwa na ubora na viwango stahiki na pia kuendeshwa kwa utaalamu unaotakiwa.” 

Bei ya mafuta 

Mkurugenzi huyo alieeleza kamati hiyo ya bunge kuwa bei za mafuta katika soko la ndani zimeshuka kwa viwango mbalimbali na kwamba zingeshuka zaidi iwapo zabuni za kuagiza mafuta kwa Septemba, Oktoba na Novemba mwaka 2015 zingeshindanishwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa mafuta kwa pamoja (BPS), jambo ambalo halikufanyika. 

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Catherine Magige alihoji juu ya mishahara ya watendaji wa Ewura kuwa juu na kujibiwa kuwa inasimamiwa na Msajili wa Hazina. 

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Martha Mlata alihoji kama Serikali ina chombo kinachoangalia ubora na wingi wa mafuta yanayoingia nchini na kujibiwa na Ngamlagosi kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kuweka kifaa cha kupima mafuta (flow meter) na kuwa ubora wa mafuta yanayoingia nchini unaangaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). 

Kuhusu kuwekwa vinasaba kwenye mafuta yaendayo nje badala ya yale yanayouzwa soko la ndani, Ewura ilieleza kuwa mafuta yaendayo nje si mali ya Tanzania, hivyo Serikali haiwezi kuwa na kauli ya mwisho kuhusiana na jambo hilo. 

Katika ufafanuzi huo uliotokana na swali la Mbunge wa Mbarali (CCM), Haroon Pirmohamed, Ngamlagosi alisema kila nchi ina sera zake kuhusiana na udhibiti wa ubora wa mafuta. 

“Hata kama nchi husika watakubaliana na uwekaji vinasaba katika mafuta yao, gharama hizo itabidi zilipwe na Tanzania. Kwa kuangalia kiasi cha mafuta hayo na jinsi kiasi kinavyoongezeka, ikijumlishwa na mafuta yaliyosamehewa kodi, ni dhahiri kabisa kuwa gharama za uwekaji vinasaba hazitatofautiana sana na za sasa,” alisema. 

Mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Vedasto Manyinyi alisema kupungua kwa uuzaji wa mafuta yanayopita nchini, kumetokana na mfumo mpya wa usimamizi wa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na si kwa sababu ya vinasaba vinavyowekwa na Ewura. 

Hata hivyo, Ngamlagosi alisema kumekuwa na mafanikio ya uwekaji wa vinasaba tangu mwaka 2010. Alisema utafiti uliofanywa na Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuchapishwa Aprili, 2014, ulionyesha kuwa hatua za udhibiti za Ewura zilileta mafanikio. 

“Udhibiti wa uchakachuaji na uuzaji wa mafuta yanayopita nchini kwenda nchi nyingine bila kulipiwa kodi ulikuwa umeleta mafanikio ya Sh468.50 bilioni. Uwekezaji vinasaba una faida ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya Serikali,” alisema Ngamlagosi. 

Manyinyi pia alihoji sababu za kiwanda cha Tiper kutoanza kufanya kazi ya usindikaji mafuta ili kupunguza bei ya mafuta nchini na kujibiwa kuwa kiwanda hicho kilisitisha usafishaji wa mafuta kutokana na uchakavu.

Source: Mwananchi




ZeroDegree.
Bilioni 277 zatumika kununua umeme IPTL na Aggreko. Bilioni 277 zatumika kununua umeme IPTL na Aggreko. Reviewed by Zero Degree on 2/17/2016 09:06:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.