Loading...

JK aahidi kuwatumbua walioihujumu CCM mwaka 2015.


Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete akifungua pazia alipokuwa akizindua ofisi ya CCM ya Wilaya ya Kibaha Mjini mkoani Pwani. Ofisi imejengwa na familia ya mbunge wa jimbo hilo, Silvestry Koka (kulia).



Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete amesema mwanachama yeyote aliyekihujumu chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba mwaka jana atatumbuliwa bila aibu huku akisema tayari wana majina ya wasaliti hao. 

Hii ni kauli ya kwanza nzito ya Kikwete akiwa mwenyekiti tu wa CCM baada ya kustaafu urais Novemba 2015 lakini ni mwendelezo wa kauli zilizojaa matumaini ambazo hazitekelezeki.

Alipokuwa Rais katika Serikali ya awamu ya nne, Kikwete aliwahi kudai ana majina ya wala rushwa, majina ya wauza unga, majangili 40 na kiongozi wao yuko Arusha lakinia hakuwahi kuwataja hadharani wala kuwashughulikia.

Pia, kama mwenyekiti wa CCM, mwaka 2011 akisaidiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu, Wilson Mukama alianzisha kaulimbiu ya kuvua magamba wanachama aliodai ni mafisadi, akataka wajiondoe kabla ya kuondolewa lakini hakuwahi kuvua gamba lolote.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la CCM mjini hapa juzi, Kikwete aliwataja baadhi ya waliokihujumu chama na wanaostahili kutumbuliwa kuwa ni wanachama ambao baada ya mchakato wa kumpata mgombea urais Dodoma walikasirika na kuanza kukisaliti.

“Baada ya mchakato wa Dodoma wapo ambao walisusa kabisa na wakawa wanajificha. Unakuta hahudhurii mikutano yetu ya kampeni, lakini ya wenzetu upinzani unamkuta na akiulizwa anasema eti alialikwa,” alisema na kusisitiza kuwa wanachama kama hao ni wasaliti na uanachama wao una mashaka.

Kikwete alisema mchakato wa kuwaadhibu wanachama wasaliti utafanyika wakati wowote baada ya kuyapitia majina ya wote wanaotuhumiwa kukihujumu chama.

“Tayari tuna majina ya watu ambayo yanadhaniwa walikihujumu chama. Tutayapembua katika vikao mbalimbali halali kuanzia ngazi za matawi, kata, wilaya, mkoa na Taifa na tutaamua kwa haki wakati wa kuwaadhibu,” alisema.

Aliwataka wanachama hao kufanya tathmini na kutambua waliokisaliti chama lakini alionya vikao vya kuwabaini vitende haki bila kumuonea mtu akisema yapo baadhi ya majina yanatajwa kuwa ni wasaliti kutokana na migogoro binafsi baina yao.

Makundi ndani ya chama

Akizindua jengo hilo lilojengwa na mbunge wa jimbo hilo Silvestry Koka kwa thamani ya Sh 100 milioni, Kikwete alisema pindi mgombea wa urais anapopatikana wanachana hawana budi kuvunja makundi na kuwa kitu kimoja.

“Mchakato halali ndani ya chama ukishafanyika na kupitishwa jina moja basi wote sasa tunatakiwa kuvunja makundi na kuwa kitu kimoja kuunga mkono mgombea aliyependekezwa na si vinginevyo,” alisema.

Alisema iwapo chama kitamchagua mgombea mmoja lakini wakawepo watu wanaompinga hao ndiyo wasaliti na ndiyo majipu yanayotakiwa kutumbuliwa.

Alisema mwanachana ana wajibu wa kupigania usiku kucha ili chama kishinde na iwapo atatokea anayekwamisha basi huyo anapaswa kuwajibishwa.

Uchaguzi Zanzibar

Kuhusu sakata la kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, Kikwete alisema kuwa hahusiki kwa namna yoyote kama wengi wanavyomtuhumu. 


Aliwataka Watanzania kupuuza tuhuma zinazotolewa kuwa anahusika kuwatumia viongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufanikisha kufutwa kwa matokeo hayo kwani hajawahi kumpigia simu wala kuzungumza na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha juu ya jambo hilo.

“Mimi sihusiki hata kidogo na sijawahi kumpigia simu mtu yeyote hata Damian Lubuva wa NEC sijawahi kumpigia simu kumpa maelekezo yoyote ya uendeshaji uchaguzi na kutangaza matokeo. Hii siyo kazi yangu na pia si mimi tu, marais wote akiwamo John Magufuli hatuna mamlaka hayo,” alisema.

Hata hivyo, aliwaomba wana CCM kuwaunga mkono Wazanzibari na kuwaombea dua ili uchaguzi wa marudio ufannyike kwa amani.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka alisema ujenzi huo umefanyika kwa ushirikiano na familia yake. Alisema kabla ya ujenzi wa ofisi hiyo, baada ya kuchaguliwa kuwa mchumi wa wilaya alitoa mifuko 15 kwa kila kata kufanikisha ujenzi wa ofisi kwenye kila kata.

Katibu Mwenezi, Masenga Masenga, akitoa taarifa ya hali ya chama hicho alikiri kuwa wapo baadhi ya wanachama waliokisaliti wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.






ZeroDegree.
JK aahidi kuwatumbua walioihujumu CCM mwaka 2015. JK aahidi kuwatumbua walioihujumu CCM mwaka 2015. Reviewed by Zero Degree on 2/24/2016 07:04:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.