Loading...

Kontena lazua kizaazaa Tabata


Wananchi wakiangalia lori lililokuwa limebeba kontena likiwa limepinduka katika Barabara Mandela eneo la njiapanda ya Tabata, Dar es Salaam jana.

Dar es Salaam. Watu sita wamejeruhiwa jana baada ya lori lililobeba kontena kuacha njia na kugonga magari matatu kisha kontena kudondoka katikati ya barabara ya Mandela na kusababisha msongamano kwa watumiaji wa njia hiyo.

Tukio hilo lilitokea jana saa 3:00 asubuhi eneo la Tabata Relini wilayani Ilala.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Ernest Matiku alisema watu sita ndiyo walioripotiwa polisi kuwa majeruhi, na wengine ambao idadi yao haifahamiki waliwahi hospitalini wenyewe.

Matiku alisema wanamsaka dereva wa lori hilo ambaye alikimbia baada ya kusababisha ajali hiyo.

Wakisimulia ajali hiyo, mashuhuda waliiambia Mwananchi kuwa lori hilo lilikuwa kwenye mwendo wa kasi likikimbizana na lori jingine lililobeba kontena. Lilipofika eneo hilo hilo lenye taa za kuongozea magari, lilijaribu kukwepa daladala lililokuwa kituoni na kuparamia kingo za barabara na baadaye kupinduka.

Shuhuda wa ajali hiyo, Said Ally alisema baada ya kuparamia na kupinduka, lori hilo lilienda kugonga magari mengine matatu yaliyokuwa katika foleni upande wa pili wa barabara.

Juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya kuzungumzia tukio hilo, ziligonga mwamba.

Credits: Mwananchi




ZeroDegree.
Kontena lazua kizaazaa Tabata Kontena lazua kizaazaa Tabata Reviewed by Zero Degree on 2/11/2016 04:57:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.