Loading...

Mwalimu aishi ndani ya darasa akidai malipo yake.


Geita. Mwalimu Hamis Mumwi aliyekuwa anafundisha katika Shule ya Msingi Mwangimagi Kata ya Nyanguku mjini Geita, anaishi darasani na familia yake kwa miaka zaidi ya kumi sasa akidai stahiki zake baada ya kufukuzwa kazi kwa kumpa mimba mwanafunzi kisha kumuoa.

Hata hivyo, Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Lawrence Mhelela alikiri mwalimu huyo kug’ang’ania darasa akisema hadai stahiki zozote kwa sababu alifukuzwa mwaka 2005 na kusafirishwa hadi kwao Ukerewe kwa gari la Serikali, lakini alirudi na kuzua madai hayo.

Mhelela alisema mwalimu huyo anaonekana jeuri, hivyo halmashauri itamtoa kwa nguvu kwa kutumia polisi.

Akizungumzia madai yake, Mwalimu Mumwi amesema leo kuwa ameamua kuishi darasani hadi atakapolipwa.

Amesema alifukuzwa kazi mwaka 2002 baada ya kushindwa kesi katika Mahakama ya Mwanzo.

Mwalimu Mumwi amesema alikata rufaa katika Mahakama ya Wilaya na kushinda, hivyo mwajiri alitakiwa kumrejesha kazini lakini alifukuzwa tena mwaka 2005 na Mamlaka ya Utumishi wa Walimu (TSD) kwa kosa lilelile la kumpa ujauzito mwanafunzi.

“Huyo hakuwa mwanafunzi kwa sababu alikuwa amemaliza darasa la saba na ninawaambia sitoki hapa hadi wanilipe stahiki zangu,” alisema Mwalimu Mumwi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Thomas Abraham alisema awali Mumwi alikua akiishi kwenye nyumba za walimu lakini ilianguaka na kuamua kuhamia darasani.

Alisema wamejitahidi kumsihi kuhama ili kuachia darasa, lakini amekaidi ilhali chumba hicho kilikuwa kinasomewa na wanafunzi darasa la kwanza na pili.

“Kutokana na mwalimu kugoma kutoka darasani, darasa la tatu wanasomea nje ili kuwapisha la pili na la kwanza. Hii ni changamoto kwa sababu eneo hili halina hata mti wa kivuli,” alisema.

Diwani wa kata hiyo, Elias Ngole alisema alipata taarifa za mwalimu huyo kutoka kwa wananchi.

Ngole aliitaka halmashauri kumuondoa mwalimu huyo darasani ili wanafunzi walitumie.



ZeroDegree.
Mwalimu aishi ndani ya darasa akidai malipo yake. Mwalimu aishi ndani ya darasa akidai malipo yake. Reviewed by Zero Degree on 2/03/2016 06:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.