Rais Magufuli amtega Jaji Mkuu.
Rais John Magufuli, akizungumza wakati wa Siku ya Sheria ya Kimataifa iliyofanyika, Dar es Salaam jana. Kutoka kulia ni Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana alimuweka Jaji Mkuu wa Tanzania kwenye wakati mgumu baada ya kumuahidi kumpa Sh12.5 bilioni ili ashughulikie kesi za ufisadi ambazo Serikali inatarajia kupata takriban Sh1 trilioni.
Rais, ambaye alikuwa akizungumza kwenye kilele cha Wiki ya Sheria, pia alimuahidi Jaji Mkuu kuwa ili kuiwezesha Mahakama kufanya kazi zake vizuri, ataipatia idara hiyo Sh250 bilioni zitakazopatikana katika kesi hizo na nyingine Sh750 bilioni zitumike kununulia ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Rais pia alizungumzia jinsi anavyozungumzwa kuwa ni diktekta, akisema yeye ni mpole na si dikteta, lakini inafika hatua anafumba macho na kusema “lazima nifanye” kwa kuwa kazi hiyo ni ngumu.
Rais Magufuli alisema hayo baada ya Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othuman kueleza changamoto zinazoikabili Idara ya Mahakama, hasa kutotengewa fungu la kutosha kumudu kuendesha shughuli za Mahakama na za maendeleo.
Akizungumzia kesi zilizopo mahakamani kwa muda mrefu, Rais Magufuli alieleza kushangazwa na kitendo cha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuchelewa kuwapeleka mahakamani watuhumiwa ambao walikamatwa na ushahidi.
“Wale waliokamatwa ‘red handed’, unasubiri nini kuwapeleka mahakamani?” alihoji Dk Magufuli ambaye alionyesha kuchukukizwa na jambo hilo.
“Wale wanaokamatwa ‘red handed’ na meno ya tembo, peleka mahakamani wakafungwe siku hiyohiyo.”
Alisema katika Mahakama ya Kisutu kuna kesi 26 za watu walioshikwa wakiwa na nyara za Serikali kama meno ya tembo, lakini kesi zimechukua zaidi ya miaka mitano na hazijatolewa uamuzi.
Alisema katika maelezo yanayotolewa ni kwamba upelelezi unaendelea wakati wahusika wa kufanya upelelezi wapo na watu wameshikwa wakiwa na hivyo vitu.
“Inawezekana hakimu anataka kutoa hukumu, lakini DPP na polisi wanaofanya uchunguzi, wanasema upepelezi unaendelea. Sasa atatoa hukumu gani?”alihoji Rais Magufuli.
“Kwa hiyo unaweza ukaona hapo tatizo lipo mahali gani. DPP uko hapa ukimshika mtu na meno ya tembo mkononi, mpeleke siku hiyohiyo akafungwe. Unahitaji upelelezi gani au unatafuta rushwa?”
Alisema vyombo vyote vinavyohusika katika kutoa haki vitimize wajibu wao.
“Hata mimi ninapochukua hatua serikalini msifikiri mimi ni mnyama sana, kichaa au dikteta. Mimi ni mpole sana, lakini inafikia mahali lazima ufumbe macho useme lazima nifanye. Kazi hii ni ngumu,” alisema Rais Magufuli.
“Kwa sababu yanayofanyika ndani ya Serikali ni ya ajabu sana. Ndiyo maana inaweza kufika mahali ukaona ugumu wa kuongoza nchi ambayo iliingiliwa na wadudu wa kila aina.”
Mashauri ya ufisadi
Akijibu changamoto hizo za Idara ya Mahakama, Rais Magufuli alisema yuko tayari kutoa fedha wakati wowote kuanzia leo ili kesi ziendeshwe na kumalizika mapema.
“Mimi nikuombe (Jaji Mkuu) hata leo hii (jana), ukatoe hukumu ya hizo kesi 442, robo ya fedha hizo nitazileta mahakamani,” alisema Rais Magufuli jana wakati ya kilele cha maadhimisho hayo.
“Hizo fedha zingelipwa hata malalamiko haya unayotoa ya kukosa fedha za maendeleo za kusaidia Mahakama kuendeshea shughuli zake, yasingekuwapo.”
Kutokana na hilo, aliahidi kumpa Jaji Mkuu Sh12.5 bilioni mapema iwezekanavyo ndani ya siku tano kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kusaidia kuendesha kesi hizo.
“Watu walipe hizo Sh1 trilioni. Ninakuahidi tena kweupe jua linawaka kati ya hizo, Sh250 bilioni nitazileta mahakamani ili kusudi sisi tubaki na Sh750 bilioni kwa ajili ya kununua ndege za Serikali,” alisema.
“Tukifanya hivyo tutakuwa na ndege ya Tanzania yenye uhakika, lakini wale wafanyakazi wa Air Tanzania (Shirika la Ndege la Tanzania, ATCL), wote 200 tutawaondoa moja kwa moja.”
Dk Magufuli alibainisha kuwa thamani ya ndege moja aina ya airbus yenye uwezo wa kubeba kati ya watu 100 na 120 au zaidi ni dola 90.6 za Marekani (sawa na Sh193.8 bilioni). Rais Magufuli, ambaye alikuwa anazungumza bila kusoma hotuba iliyochapishwa, alisema ametoa kauli hiyo kwa sababu anataka mabadiliko.
“Haiwezekani nchi kama Tanzania ina kila kitu halafu bado tukawa maskini. Tumebaki kuomba msaada wakati kila kitu tunacho,” alisema huku akieleza kwamba maneno aliyotoa ni ya moyoni ndiyo maana hajataka kusoma hotuba iliyoandikwa na mtu mwingine.
Rais huyo, ambaye tangu alipoingia madarakani amekuwa akiwawajibisha baadhi ya watendaji katika kutekeleza kazi aliyojipa ya kutumbua majipu, alisema kuna changamoto kubwa katika kuweka maadili yaliyo mema.
Alisema wapo watu wanacheza na pesa kama wanavyotaka, hivyo akaomba Mahakama na watoa haki mahali popote watoe hukumu kwa haki.
“Lakini kwa hawa ambao wanaweza kuifikisha nchi pabaya toeni hukumu haraka,” alisema huku akisisitiza kuharakisha kuanzishwa kwa Mahakama ya mafisadi na wahujumu uchumi.
Awali, katika hotuba yake, Jaji Mkuu alimueleza Rais Magufuli kuhusu changamoto zinazoikabili Mahakama ikiwamo fedha za maendeleo.
Akizungumzia kuhusu Rais Magufuli kutoa fedha hizo na sehemu yake zisaidie kwenye uendeshwaji wa kesi hizo, Profesa Abdallah Safari alisema: “Miaka mitano mbona chamtoto! Mimi nina kesi ya mirathi ya tangu mwaka 1989,” alisema Profesa Safari.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utetezi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia aliutazama uamuzi huo kwa pande mbili.
“Hakuna mtu anapenda kuona kesi zinaendeshwa mahakamani muda mrefu bila hukumu kutolewa. Huenda Rais Magufuli ameliona hilo ndiyo maana kasema hivyo,” alisema.
Sungusia alisema upande mwingine ni kuhusu Mahakama kutopewa fungu la kutosha kwa ajili ya kuendesha shughuli zake. “Umefika wakati sekta nzima za uendeshaji wa shughuli za kutoa haki zipewe fungu la kutosha,” alisema.
ZeroDegree.
Rais Magufuli amtega Jaji Mkuu.
Reviewed by Zero Degree
on
2/05/2016 11:41:00 AM
Rating: