Loading...

Tingatinga lazifikia Nyumba na Bar zilizopo Dagadagaa Legho.


Tingatinga likibomoa Nyumba na Bar zilizopo eneo maarufu lijulikano Dagadagaa Legho, Dar es Salaam jana.

Dar es Salaam. Vilio na simanzi jana vilitawala katika eneo la Kijiji cha Sanaa, Shekilango maarufu ‘dagaadagaa’ baada ya kubomolewa kwa nyumba sita na vibanda vya kuuzia nyama ya nguruwe na pombe.

Bomoabomoa hiyo iliendeshwa jana kuanzia saa 3:00 asubuhi na kampuni ya udalali ya Mem Auctioneers and General Brockers Limited baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa amri kwa watu waliojenga kwenye kiwanja hicho ambacho mmiliki wake ni M/S Cool Makers Limited kuondoka.

Awali, mgogoro wa ardhi wa eneo hilo ulikuwa ukiwahusisha M/S Cool Makers Limited (mdai), Jumuiya ya Wazazi ya CCM na John Ondoro.

Mmoja wa wafanyabishara wa eneo hilo, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa sherehe, Selestian Kimario, alisema walinunua eneo hilo kwa Sh400 milioni.

Mwenyekiti jumuiya hiyo ya CCM, Abdallah Bulembo alisema bomoabomoa hiyo imeendeshwa kinyume na sheria kwa madai kuwa hawakupewa taarifa.

Alisema jumuiya hiyo inakusudia kwenda mahakamani ili kupinga bomoabomoa hiyo.

“Huu ni uonevu na ni ukatili dhidi ya raia wasio na hatia. Hawa watu wanaishi na kufanya biashara, unawezaje kuwabomolea bila kuwataarifu? Nchi gani haiheshimu utawala wa sheria? Jumatatu tutarudi mahakamani,” alisisitiza Bulembo.

Alisema eneo hilo lina mgogoro wa muda mrefu na kwamba kesi ilikuwa inaendelea mahakamani.

Hata hivyo, wakili wa M/S Cool Makers Limited, Said Aziz alisema walifuata hatua zote za kisheria, Januari 25 walipewa agizo kubomoa nyumba zilizopo eneo hilo na Mahakama ya Kisutu.

“Kesi hii ilianza tangu mwaka 1993, na mwaka 2012 ilitoka amri ya kubomoa nyumba katika eneo hili, sisi tunatekeleza,” alisema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo NHC, Amani Sizya alisema ofisi yake haikuwa na taarifa za kuwapo kwa bomoabomoa hiyo.

Sizya alidai kuwa wakiwa viongozi wa mtaa kisheria, walipaswa kujulishwa siku 14 kabla ya ubomoaji wa nyumba hizo kufanyika.

Gazeti la Mwananchi lilishuhudia hali ya taharuki na vilio kutoka kwa wapangaji baada ya kuvunjiwa vibanda vyao.

Baadhi ya wamiliki wa biashara zilizokuwa kwenye eneo hilo, walisema zaidi ya watu 200 wamepoteza ajira kutokana na ubomoaji huo.

Mpangaji wa ghorofa lililobomolewa kwenye eneo hilo, Grancian Kamukara alisema: “Makubaliano ni kuwa nilifanyie ukarabati jengo hilo, kama unavyoona nilikuwa kwenye hatua za mwisho ya kuanza kuishi, sikupewa taarifa zozote nimesikia asubuhi hii kuwa panavunjwa.”

Wateja walaani

Baadhi ya wateja na wananchi waliokuwa eneo la baa iliyovunjwa walilaani kitendo hicho, huku wakihoji watakapokwenda kupata nyama choma na sehemu ya kuburudika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema eneo hilo lilikuwa maarufu Dar es Salaam kwa kuuza nyama choma. “Jamani kwani kuna nini, mbona wanatuvunjia eneo letu la kujivinjali wanataka twende tukastarehe wapi?, Hapa ndiyo tulikuwa tunapata nyama nzuri,” alisema Juliana John.

John alieleza kuwa baa zilizovunjwa zilikuwa zinatoa huduma mbalimbali za starehe, vyakula, vinywaji kwa wakazi wengi wa Dar es Salaam .“Hii Serikali inatunyanyasa wananchi. Imekuwaje tena mambo haya yanatokea? Ukiachia burudani, watu waliwekeza mabilioni ya fedha kujenga hapa,” alisema Ally Mohamed.

Wananchi wapongeza

Wakati eneo hilo likiendelea kuvunjwa baadhi ya wananchi waliokuwa wakipita walisema bora walivyovunja wataokoa maadili ya watoto wao.

“Hili eneo lilikuwa halifai kwa ukahaba na biashara ya ngono. Watoto wetu waliharibikia hapa, nampongeza aliyeagiza eneo hili kuvunjwa,” alisema Mtobe Matuiku.

Jonas Mtatilo alisema eneo hilo la lilikuwa halifai kwa madai kuwa kuna watu walikuwa wanatumia kufanya vitendo vya kihuni.

Credits: Mwananchi



ZeroDegree.
Tingatinga lazifikia Nyumba na Bar zilizopo Dagadagaa Legho. Tingatinga lazifikia Nyumba na Bar zilizopo Dagadagaa Legho. Reviewed by Zero Degree on 2/05/2016 11:53:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.