Loading...

Ugonjwa wa ajabu bado haujaingia nchini, serikali yawatoa hofu wananchi na kusema imejipanga kuhakikisha hauingii nchini.


Dodoma. Siku moja baada ya gazeti la mwananchi kuandika habari ya virusi hatari vinavyosababisha ugonjwa wa zika vinavyoendelea kusambaa kwa kasi duniani, Serikali imewatoa hofu Watanzania kwamba ugonjwa huo haujaingia nchini na imejipanga kuhakikisha hauingii.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema jana kuwa dalili za ugonjwa huo zinafanana na za homa ya dengue, ambazo ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo, macho kuwa mekundu na kupata vipele vidogovidogo kama harara.

 Mbu wanaoeneza virusi vya zika, ni aedes egyptiae ambao pia husababisha homa ya dengue, ugonjwa ulioenea nchini mwaka 2014 kabla ya kudhibitiwa.

Alisema dalili za ugonjwa wa zika zinaweza kufanana na zile za malaria, hivyo ni vizuri wananchi wanapokuwa na dalili hizo waende hospitali kwa kuwa zika inatibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.

Alipoulizwa kama ugonjwa huo una dawa maalumu, alisema; “Hauna dawa maalumu wala chanjo. Unatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa husika kama vile homa, kupungukiwa maji au damu.”

Alisema baada ya kupata taarifa za kuibuka kwa ugonjwa huo, Serikali imefuatilia ugonjwa huo katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini na mipakani kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa.

Aliwataka wananchi kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama na kunyunyizia viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu, kufyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu na kufunika mashimo ya majitaka kwa mifuniko imara, kuvaa nguo ndefu, kutumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu na kuweka nyavu kwenye madirisha na milango.

Alisema kwa sasa Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi.

Virusi vya zika siyo vipya duniani, lakini madhara yake ni mapya kwa kuwa sasa vinawaathiri watoto wanaozaliwa na wajawazito walioumwa na mbu hao.



ZeroDegree.
Ugonjwa wa ajabu bado haujaingia nchini, serikali yawatoa hofu wananchi na kusema imejipanga kuhakikisha hauingii nchini. Ugonjwa wa ajabu bado haujaingia nchini, serikali yawatoa hofu wananchi na kusema imejipanga kuhakikisha hauingii nchini. Reviewed by Zero Degree on 2/01/2016 11:14:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.