Loading...

Mgodi wasababisha vifo vya watu watano na kujeruhi wengine watatu mkoani Geita.


Wakazi wa Kijiji cha Mgusu wilayani Geita, wakishuhudia eneo ambalo gema la mwamba limemeguka na kusababisha vifo vya watu watano na wengine kadhaa kujeruhiwa jana. 



Watu watano wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa kwa kifusi cha mchanga wakati wakichimba dhahabu katika machimbo ya Mgusu mkoani 
Geita.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni wakati wachimbaji wadogo wakichimba dhahabu katika eneo lililokuwa limepigwa marufuku kutokana baada ya kuonyesha dalili za mwamba wake kumeguka.

Kutokana na maafa hayo, Kaimu Ofisa Madini mkoani hapa, Fabian Mshai amefunga mgodi huo wenye leseni 20 za uchimbaji zinazomilikiwa na chama cha ushirika wa wachimbaji wadogo wa Mgusu hadi uchunguzi utakapokamilika.

Mshai alisema Machi 4, mwaka huu, ofisi ya madini Geita iliwataka wamiliki wa mgodi huo ambao ni chama hicho kusitisha uchimbaji katika eneo hilo kwa kuwa ni hatarishi baada ya kubainika kuwa gema lina ufa na kuanguka muda wowote.

Kaimu ofisa madini huyo, aliwataka wachimbaji, hususan wamiliki wa migodi kuzingatia sheria za afya na usalama kazini ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Rufaa mkoani hapa, Adam Sijaona alisema amepokea miili mitano ya wachimbaji hao na majeruhi watatu.

Dk Sijaona alisema majeruhi hao Simon Jonathan (28), Mkwimba John (54) na Mbokwe Upepo (30), wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa Bugando kwa matibabu zaidi.

Katibu wa Chama cha Ushirika Mgusu, Zacharia Otange alisema chama hicho kina leseni za uchimbaji 20 zinazomilikiwa na wachimbaji wadogo zipo eneo la mgodi wa Mgusu. 

Alisema pamoja na kutangaza kwa wachimbaji kutoingia katika eneo hilo, baadhi ya wachimbaji walikaidi na kuingia kinyemela kwa kuwa eneo lilikuwa wazi na kuonyesha mawe yanayoashiria uwapo wa dhahabu, hivyo kushawishika kuingia.




ZeroDegree.
Mgodi wasababisha vifo vya watu watano na kujeruhi wengine watatu mkoani Geita. Mgodi wasababisha vifo vya watu watano na kujeruhi wengine watatu mkoani Geita. Reviewed by Zero Degree on 3/11/2016 08:25:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.