Loading...

Aliyekuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa, Juma Duni Haji arudisha Kadi ya CHADEMA na kurejea CUF.


Mwanasiasa machachari wa upinzani kutoka Zanzibar, Juma Duni Haji ambaye alikuwa mgombea mwenza wa aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kupitia Chadema, amerejea katika chama chake cha CUF.

Duni amerejea CUF ikiwa imepita miezi takribani tisa tangu alipojiunga na Chadema ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Duni alisema:

“Nimerudi nyumbani CUF na Chadema nilikwenda ili kutimiza matakwa ya kikatiba kwa kuwa mgombea mwenza wa urais lazima atoke upande wa pili wa Muungano. Hiyo ni kwa mujibu wa matakwa ya Katiba yetu.”

Mara baada ya Lowassa kupitishwa na Chadema na Ukawa kuwa mgombea wa urais, Duni ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) alionekana kuwa na sifa ya kuwa mgombea mwenza na hivyo kupewa kadi ya Chadema.

Mwanasiasa huyo amekuwa na historia ndefu na mara tatu amewahi kuteuliwa na CUF kuwa mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano, akiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Jana, Duni alikuwa miongoni mwa viongozi wa CUF waliokaa meza kuu na Maalim Seif wakati Katibu Mkuu huyo akieleza mwelekeo wake na wa chama hicho baada ya kususia uchaguzi wa marudio Zanzibar uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

Akieleza uamuzi wake huo Duni alisema: “Sioni ajabu yoyote mimi kurudi CUF. Kwa nini nibaki Chadema? Siwezi kubaki kwa sababu kule nilikwenda kwa ajili ya makubaliano tu.”

Huku akionekana kutotaka kueleza uamuzi wake huo kiundani, Duni alisema pamoja na kuwa amerejea CUF, ushirikiano wa chama hicho pamoja na vingine vinavyounda Ukawa vya Chadema, NCCRMageuzi na NLD, uko palepale.

Akieleza jinsi CUF walivyompokea, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema ni faraja kubwa kwa mwanasiasa huyo kurejea nyumbani.

“Jana (juzi) saa 10.30 jioni katika tawi la CUF la Kibeni lililopo katika Wilaya ya Kaskazini Unguja jimbo la Mkwajuni ndipo Duni alipofanyiwa hafla fupi ya kukaribishwa tena katika chama chetu na kupewa kadi,”alisema Mazrui.

“Alirejesha kadi ya Chadema na kuchukua na CUF. Tunamkaribisha sana na tunampongeza kwa kuiwakilisha vyema Chadema na Ukawa katika Uchaguzi Mkuu.”

Mazrui alisema si jambo la ajabu kwa mwanasiasa huyo kurejea CUF kwa sababu awali alikuwa katika chama hicho ila aliondoka kwa ajili ya kwenda kutimiza matakwa na ushirikiano ndani ya Ukawa.

“Ndani ya Ukawa lengo letu ni moja wala hilo lisikufanye ukafikiri tofauti... usidhani kuwa kuna tofauti yoyote eti kwa sababu ya uamuzi huu wa Duni,” alisema Mazrui.




ZeroDegree.
Aliyekuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa, Juma Duni Haji arudisha Kadi ya CHADEMA na kurejea CUF. Aliyekuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa, Juma Duni Haji arudisha Kadi ya CHADEMA na kurejea CUF. Reviewed by Zero Degree on 4/11/2016 09:43:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.