Loading...

Hofu yazuka nchini kufuatia wimbi la mauaji.


Msikiti uliopo jijini Mwanza ambao Mei 18 waumini watatu waliuawa walipokuwa wakifanya ibada msikitini humo. 

Dar es Salaam. Ongezeko la mauaji yanayoacha maswali, sasa linatia hofu wananchi baada ya watu takriban kumi kuuawa katika mazingira ya kutatanisha katika kipindi kisichozidi siku 15.

Mikoa ya Kanda ya Ziwa inaongoza kwa mauaji hayo ambayo safari hii hayajachukua sura ya sababu za imani za kishirikina kama ilivyozoeleka. Mbali na mikoa hiyo, mauaji hayo sasa yamesambaa kona tofauti za nchi.

Katika muda wa siku hizo, sababu za mauaji ya baadhi ya matukio hazijafahamika, lakini mengine yameripotiwa kuwa ni kutokana na mapenzi, itikadi za kidini, visasi na biashara, ingawa sababu hizo ni ubashiri wa polisi kutokana na mazingira ya vifo.

Matukio mengi yamekuwa ni ya kutumia silaha za jadi, kama mapanga, shoka na visu kuchinja na wahusika kutokomea bila ya kuchukua vitu, isipokuwa kwenye matukio machache walikobeba simu.

“Matukio hayo yanasababisha taharuki na hofu kwa jamii kwa sababu hayaonyeshi kama ni ujambazi bali yana dalili za kulipiza visasi,” alisema Dk Hellen Kijo-Bisimba, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), alipohojiwa kuhusu ongezeko la mauaji hayo tata.

“Inatisha kwa sababu zamani ilikuwa ni Mwanza, sasa hivi ni nchi nzima. Mimi siamini kama ni ujambazi, kama ni ujambazi huwezi kuchinja mtu kiasi kile.”

Dk Bisimba alisema suala la visasi lisipopata suluhisho nchi inaweza kuwa ni ya visasi na mauaji yataongezeka.

Alisema njia nzuri nya kumaliza matatizo ni kufuata mfano wa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, ambaye alipotoka gerezani alisamehe yote ndiyo maana nchi hiyo imekuwa na amani.

Alisema jamii inapoteza maadili na utu ndiyo maana wengi wanapoteza hofu ya Mungu na kufanya ukatili wa aina hiyo.

Katika matukio hayo ambayo yameripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini, ni la mauaji ya wanafamilia saba yaliyotokea katika kijiji cha Sima wilayani Sengerema, mkoani Mwanza.

Tukio hilo lilitokea saa 7:00 usiku Mei 10, baada ya watu kuvamia nyumba ya mjane ambaye alikuwa akiishi na watoto wake na wafanyakazi wake wawili wa ndani. Wote waliuawa kwa kukatwa kwa mapanga na hadi sasa watu waliofanya uovu huo hawajajulikana.

Ofisa habari wa Mkoa wa Mwanza, Atley Kuni aliwataja waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Eugeni Philipo (62), Maria Philipo (56), Yohana Mabula (20), Regina Aloyce (12) na Mkiwa Philipo (13) huku wengine wawili wakitambulika kwa jina moja kila mmoja kuwa ni Donald na Samson

Baada ya wiki moja, watu wengine watatu waliuawa kwa kukatwa mapanga wilayani Nyamagana.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi alisema mauaji hayo yalitokea Mei 18, saa 2:30 usiku kwenye msikiti Masjid Rahman.

Msangi alisema watu wasiozidi 15 waliofunika nyuso zao, wakiwa na mapanga, shoka na bendera nyeusi yenye maandishi meupe, waliingia msikitini wakati wa swala.

Alisema watu hao walizima taa na kutoa sauti wakisema “kwa nini mnaswali wakati wenzetu wamekamatwa na wanashikiliwa na polisi?”

Alisema hapohapo wakaanza kuwashambulia kwa mapanga na kusababisha vifo vya Feruz Ismail (27), Mbwana Rajab (40) na Khamisi Mponda (28).

Tukio jingine lilitokea Mei 22 mkoani Tabora ambako Kashidye Shija (22) aliuawa kwa kuchomwa kisu sehemu mbalimbali baada ya kukataa kufanya mapenzi na kijana aliyedaiwa alikuwa akimtaka.

Kamanda ya polisi wa mkoa huo, Hamisi Issa alisema wanamshikilia Lugala Makalesia kwa tuhuma za kuhusika kwenye mauaji hayo ambayo yalitokea saa 1:00 usiku.

Dar es Salaam pia ilikumbwa na mauaji Mei 25 wakati mtumishi wa Wizara ya Fedha, Aneth Msuya (30) ambaye ni mdogo wa Bilionea Erasto Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi 22 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia). Aneth aliuawa kwa kuchinjwa akiwa nyumbani kwake usiku, eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Usiku huo pia, watu wawili ambao wanasadikiwa kuwa ni mke na mume, waliuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana mjini Butiama, mkoani Mara.

Mei 26, mwaka huu, mtu na mkewe wakazi wa wilaya ya Butiama mkoani Mara waliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana waliowavamia nyumbani kwao wakiwa wamelala.

Sababu kuu mbili.


Akizungumzia mauaji hayo, Chris Mauki, ambayeni mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya ndoa, alisema mauaji hayo yanatokana na sababu kuu mbili.

“Sababu kubwa zaweza kuwa ni ugumu wa maisha na kutafuta fedha,” alisema mtaalamu huyo aliyehojiwa na Mwananchi kuhusu sababu za ongezeko la mauaji hayo tatanishi nchini.

“Mtu anadiriki kuua ili apate ujira. Anajitosa; litalokuwa na liwe.”

Mwanasaikolojia huyo alionya kuwa baadhi ya matukio hayo hushuhudiwa na watoto na hivyo kuwaathiri kisaokolojia.

“Watoto ambao wameshashuhudia mauaji yakitendeka mbele yao, wanaweza kufanya haya siku za baadaye,” alisema.

Naye Kijo-Bisimba aliungana na Mauki kusema hali ngumu ya uchumi pia inachangia ongezeko hilo la mauaji.

“Kuna tofauti kubwa kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho. Hilo nalo ni tatizo. Kuna haja ya kurudisha maadili, viongozi wa dini wafaye kazi yao na tuwe macho,” alisema

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alipoulizwa kuhusu mauaji yanayoendelea nchini na hatua ambazo Serikali inachukua kuyadhibiti, alisema suala hilo litazungumziwa leo Bungeni.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella na kamanda Msangi wamesema mauaji watu kupigwa risasi au kukatwa mapanga yanayotokea mkoani humo ni uhalifu wa kawaida unaohusisha mitandao wa uhalifu ambayo imeshagundulika.

“Yanayotokea Mwanza ni uhalifu wa kawaida unaotekelezwa na mitandao ya uhalifu. Hakuna ugaidi Mwanza,” alisema Mongella.

“Vyombo vya dola tayari vimebaini mitandao hii na kuwatia mbaroni wahusika na juhudi zinaendelea kuwasaka watu wanaoaminika kuwa vinara wa mitandao hii waliofanikiwa kutoroka muda mfupi kabla ya kukamatwa,”

Mongella alikuwa akijibu swali kuhusu wimbi la mauaji mkoani Mwanza na kama mauaji hayo ya msikitini yana uhusiano na ugaidi kutokana na wauaji kubeba kitambaa kilichoandikwa “Dola la Kiislamu”, kundi linaloendesha mashambulizi ya kigaidi duniani.

Alisema pamoja na sababu ningine, udhaifu kiutendaji wa baadhi ya wakuu na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama vimechangia wimbi la matumizi ya silaha katika kuvamia, kupora, kujeruhi na kuuawa wafanyabiashra katika maduka ya fedha kwa njia ya mtandao.

“Serikali imeshachukua hatua kwa kufanya mabadiliko katika safu ya uongozi wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola mkoani Mwanza na matunda yameanza kuonekana kwa mitandao ya uhalifu kujulikana na kudhibitiwa,” aliongeza Mongella, ambaye alipendekeza kamanda wa polisi aliyemkuta wakati akihamia Mwanza kutokea Kagera, ahamishwe.

Kwa upande wake, Kamanda Msangi alisema polisi imefanikiwa kuwakamata watu kadhaa ambao ushahidi unadhihirisha wameshiriki katika matukio ya mauaji kwenye maduka ya fedha kwa njia ya mtandao na yale ya kukata watu kwa mapanga.

“Baadhi ya watuhumiwa tumewakamata na ushahidi ukiwamo mali za marehemu zilizoporwa wakati wa tukio. Wapo waliokutwa na simu na nguo zilizolowa damu za marehemu Eugenia Phillipo aliyeuawa na wengine sita wa familia moja kwa kukatwa mapanga tumeikamata,” alisema Msangi.

Kamanda huyo alisema hivi sasa polisi inawasaka watu wawili wanaoaminika kuwa vinara wa mitandao ya uhalifu mkoani Mwanza.

Akizungumza na wananchi wilayani Misungwi mwezi uliopita, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema vyombo vya dola vimebaini mitandao saba ya uhalifu mkoani Mwanza na tayari miwili ilishasambaratishwa.

Pamoja na mkoa wa Mwanza, Geita na Mara pia imekuwa ikishuhudia mauaji ya kukatwa kwa mapanga yanayohusishwa na imani za kishirikina na ugomvi wa mali ikiwamo migogoro ya mipaka ya ardhi au mashamba.

Mbali na matukio ya mauaji kwa kutumia mapanga yaliyotokea katika mwezi huu, watu wawili waliuawa kwa kukatwakatwa mkoani Geita, akiwamo muuguzi wa Zahanati ya Kagu kwa kile kinachodaiwa kuwa imani za kishirikina.

Waliouawa ni Helena Paulo (56) mkazi wa kijiji cha Luhuma ambaye alikatwa mapanga wakati akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake, sawa na muuguzi huyo, Elizabeth Masango (54) aliyeuawa kwa kukatwa kwa mapanga akiwa nyumbani kwake, kwa mujibu wa taarifa ya polisi.

Mwezi huo huo, mume na mke ambao ni wakulima na wakazi wa kijiji cha Tambukareli, tarafa ya Itigi, wilaya ya Manyoni mkoani Singida, waliuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.

Wanandoa hao ni Mbulalina Shomi (80) na mke wake, Joyce Mathayo (70).

Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka, alisema tukio hilo lilitokea Aprili 10 saa sita 6:00 za usiku katika kijiji cha Tambukareli.

Sedoyeka alisema siku ya tukio wakati wanandoa hao wamelala, walivamiwa na watu waliovunja mlango wa mbele kuingia ndani na kufanya uovu huo.

Zaidi ya watu 37 wanadaiwa kuuawa kwa kukatwa mapanga mkoani Geita kati ya Desemba, mwaka jana hadi Aprili, mwaka huu.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema atatoa maelezo yake leo katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Sirro alisema ameweka utaratibu wa kuzungumza na waandishi wa habari kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.





ZeroDegree.
Hofu yazuka nchini kufuatia wimbi la mauaji. Hofu yazuka nchini kufuatia wimbi la mauaji. Reviewed by Zero Degree on 5/30/2016 12:53:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.