Makaburi Dar sasa pasua kichwa
Dar es Salaam. Kiimani, ndugu zetu wanapopoteza maisha tunawalaza kaburini tukidhani wanapumzika kwa amani, lakini kama tunaamini kuwa sehemu hiyo wanapumzika kwa amani, tunajidanganya; maiti zinafukuliwa kupisha nyingine, Mwananchi inaweza kukuthibitishia.
Si Kinondoni, Temeke au Ilala ambako maeneo maarufu ya kuzikia bado yana nafasi. Yote yamejaa na kuna uwezekano baadhi ya watu wakakuta makaburi ya ndugu zao hayaonekani kwenye sehemu hizo jijini Dar es Salaam.
Wale waliozoea kuzika na wanatarajia kwenda kuzika maeneo kama Kinondoni Makaburini, Kisutu, Chang’ombe, Wailes na Buguruni, sasa hakuna nafasi.
Lakini kinachofanyika sasa ili kuwezesha maeneo hayo kuendelea kutumika, ni kufukua makaburi yaliyopo na kuzika miili mipya. Lakini pia, kujaa kwa maeneo ya kuzikia kumezua mbinu mpya ya uzikaji; double decker au maiti juu ya maiti.
Na umaarufu wake Kinondoni imejaa
Moja ya maeneo maarufu ya kuzikia ni makaburi ya Kinondoni ambako miili ya viongozi, wafanyabiashara wakubwa, wasanii wakubwa na watu maarufu, VIP, hulazwa. Wakati tunaandika habari hii, bado watu wenye uwezo mkubwa kifedha wanazikwa eneo hilo.
Ndilo eneo walimozikwa watu kama Steven Kanumba, muigizaji nyota wa filamu aliyeipaisha tasnia hiyo nje ya Tanzania, Ndanda Kosovo aliyekuwa mwimbaji nyota kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rahel Haule aliyekuwa mwigizaji na wengine wengi.
Eneo hilo lina ukubwa wa takriban ekari nne kwa ujumla kwa kuangalia sehemu wanakozikwa watu wa kawaida na eneo la Kwa Manyanya.
Ukweli ni kwamba eneo kwa ajili ya kuzika kwenye makaburi hayo limejaa, kwa mujibu wa mamlaka husika.
Msimamizi mkuu wa makaburi hayo, Nasib Rashid alisema hivi sasa maeneo mengi jijini Dar es Salaam yamejaa.
“Hata hapa Kinondoni kumejaa na imefika hatua ndugu wanatuandikia barua kuomba yachimbwe makaburi ya ndugu zao, ili wafukue na kuwazika wengine juu yao,” alisema.
Alisema tatizo ni kwamba watu wengi bado wanang’ang’ania kuzika wapendwa wao Kinodnoni, lakini Manispaa ya Kinondoni imeshatenga eneo kubwa lililoko Tegeta Kondo na kuwataka wananchi kutong’ang’ania kuzika Kinondoni.
Madalali Kinondoni
Utafiti wa Mwananchi ulibaini kuwa wapo baadhi ya watu wanaoshinda kwenye Kinondoni Makaburini wakisubiri wanaosaka eneo la kuzika na kufanya udadlali ili kuwawezesha kupata eneo kwa makubaliano ya malipo.
Mwandishi wetu aliyeenda kwenye makaburi hayo kutafuta eneo la kuzika, aliambiwa lipo, lakini kinachotakiwa ni taratibu. “Usihofu kukosa eneo la kumzika ndugu yako, cha msingi tuandikie barua na ukishaileta utapewa maelekezo,” alisema.
Barua hiyo iliandikwa na ilipofikishwa, mtu huyo aliipokea na kutaka ipelekwe hati ya kifo ili kuthibitisha kifo hicho.
Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, alitokea dalali mwingine ambaye alisema hakuna haja ya kutafuta cheti hicho isipokuwa ziandaliwe fedha.
Eneo la kuzikia Sh1 milioni
Mwandishi wetu alijifanya akisaka eneo la kuzika, bei aliyoambiwa ya makaburi ni vigumu kwa mtu wa kawaida kuimudu.
Kaburi ambalo lililojengwa ambalo wazikaji wanatakiwa kuingiza mwili tu linalipiwa kati ya Sh1.5 milioni na Sh1.7 milioni, wakati kaburi la mchanga ni Sh500, 000.
“Unachotakiwa kufanya utuambie tarehe ambayo ndugu yako atazikwa halafu ulipie nusu ya gharama ya kuandalia kaburi, ili siku ya kuzika umalizie fedha yote tuanze kazi,” alisema mmoja wa madalali hayo aliyejitambulisha kwa jina moja la Haruna.
Wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo walisema, ikiwa familia haina fedha na aliyefariki siyo kiongozi wala mtu maarufu, ni vigumu kupata eneo. “Ndiyo maana eneo hili tunaliita VIP kwa sababu mtu maskini hawezi kupata nafasi ya kuzikwa hapa,” alisema Luis John, mfanyabishara mdogo karibu na makaburi hayo.
Alisema kama eneo hilo limejaa, lizuiwe badala ya hali ilivyo ambayo ni lazima sehemu kunakochimbwa kaburi jipya kuwa na mabaki ya miili ya mtu mwingine.
“Wachimbaji wana siri nzito ya kufukua mafuvu ya waliozikwa zamani ndiyo maana siyo rahisi mtu mwingine kuruhusiwa kufanya kazi hiyo hata kama mna uwezo wa kuchimba,” alisema.
Mkazi mwingine anayeishi karibu na eneo hilo, Linus Mgulla alisema wapo watu ambao watakuja kugundua kuwa makaburi ya ndugu zao hayapo kutokana na tabia ya kuendelea kuzika wakati ukweli ni kwamba, eneo hilo limejaa.
“Serikali ijue tu kwa mijini maeneo ya kuzika ni bomu linaloweza kuja kulipuka wakati wowote ikiwa ndugu watabaini ndugu yao alifukuliwa na eneo hilo kuzikwa mtu mwingine,” alisema.
Viwanja vyahodhiwa
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alisema wanaoendelea kuzikwa kwenye makaburi hayo ni wale walionunua viwanja na kuvihifadhi kwa muda mrefu. Nasoro alisema yapo maeneo yaliyokuwa yamehodhiwa na watu tangu miaka ya 1950 kwa ajili ya kuwazika ndugu zao.
Alisema maeneo hayo yanaendelea kutunzwa na mara kadhaa ndugu hao hufika kuyasafisha.
Hali halisi Kinondoni
Rashid alisema utaratibu uliopo hauruhusu mtu yeyote kulipishwa eneo kwa ajili ya kuzika.
“Kwa kawaida kiwanja cha kuzikia mtu akifariki ni bure kabisa kwenye ofisi yetu,” alisema.
Alidai kuwa malipo ya maandalizi ya kaburi hutegemea makubaliano ya wachimbaji na wafiwa kulingana na aina ya kaburi, huku akionyesha kushangazwa na bei zilizotajwa na madalali hao ikiwamo Sh500,000 ya kaburi la mchanga.
Hata hivyo, alisema atalishughulikia suala hilo na kuwataka wananchi kutumia eneo la Tegeta Kondo lililotengwa kwa ajili uzikaji.
Kuhusu kufukua mafuvu ya watu wengine, alisema ilishatokea mara moja walipokuwa wakichimba kaburi walipobaini kuwa kuna mtu mwingine alikuwa amezikwa.
“Tukio hili lilisharipotiwa na ndiyo maana tunawashauri wananchi watumie eneo la Tegeta,” alisema.
Hata hivyo, alisema maeneo mengi ya makaburi yalitengwa wakati idadi ya watu ilipokuwa ndogo.
Alisema kadri siku zinavyoongezeka ndivyo ambavyo mahitaji ya kuzika yanakuwa makubwa. Rashid alisema watu wasio na ndugu peke yao kwa mwaka hufikia 400 kwa jiji hilo, idadi ambayo ni kubwa ikijumlishwa na waliofariki wakiwa na ndugu. [ Itaendelea kesho..... ].
Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Makaburi Dar sasa pasua kichwa
Reviewed by Zero Degree
on
5/21/2016 02:51:00 PM
Rating: