Loading...

Jina la Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda latumika kutapeli jijini Dar.


POLISI mkoa wa Ilala inamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa kosa la utapeli na kutumia vibaya jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Akizungumza na waandishi wa habari , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema Juni 16 mwaka huu, walimkamata Imarock Rutashobya (37) mkazi wa Pugu kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wa kutumia jina na Makonda.

Alisema alikamatwa baada ya kumpigia simu Mkurugenzi wa kampuni ya Jones Logistic Ltd, James Lupondo na kujitambulisha kwa mtu huyo kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kumsaidia kijana ambaye amepata ufadhili kwenda kusoma nje.

Alisema anahitaji Lupondo achangie asilimia 30 sawa na dola za Kimarekani 3,500 ya gharama za chuo kilichopo nchini Ufilipino, baada ya kupata ufadhili wa asilimia 70.

Aliongeza kuwa katika maongezi yake, mtuhumiwa huyo alimweleza Lupondo kuwa kuna namna tofauti za kutuma fedha hizo za msaada, ikiwa ni pamoja na kuweka kwenye akaunti ya benki au kutoa fedha taslimu huku akimtajia namba ya simu ya kijana anayehitaji msaada huo ambayo ni 0717 338473 na kusema huyo kijana atafika ofisini kwake baada ya saa mbili akiwa na nyaraka zote za fursa ya hayo masomo.

“Naomba nitoe onyo kwa wote wenye tabia ya namna hii ya kutumia majina ya viongozi wakubwa wa serikali kwa lengo la kujipatia fedha, aidha wananchi wanatakiwa kuwa makini wanapopigiwa simu na watu wasiowafahamu na kujitambulisha kwao kwa majina ya viongozi,” alisema Hamduni.

Alisema licha ya kutumika kwa jina la Makonda, pia wapo watu wengine wamekuwa wakitumia jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwatapeli watu wenye fedha.

Source: Mtembezi
ZeroDegree.
Jina la Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda latumika kutapeli jijini Dar. Jina la Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda latumika kutapeli jijini Dar. Reviewed by Zero Degree on 6/23/2016 01:14:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.