Loading...

Atakayeshindwa kutoa au kudai risiti kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyopungua shilingi milioni 3.


Dodoma. Mtu atakayeshindwa kutoa au kudai risiti anakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyopungua Sh3 milioni, iwapo muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 utapitishwa na Bunge.

Kuwasilishwa kwa muswada huo ni mwendelezo wa agizo la Rais John Magufuli la kuwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kudai risiti kwa malipo wanayoyafanya, kwa kuwa ndani yake kuna ‘percentage’ ya Serikali kwa masuala ya maendeleo.


Muswada uliowasilishwa bungeni awali Juni 8, kifungu cha 61 kinapendekeza kufanyia marekebisho kifungu cha 86 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015 na kuongeza makosa katika matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD).

Moja ya mapendekezo ya makosa hayo ni mtu kutodai risiti au kushindwa kuripoti kuwa amenyimwa risiti, au ankara ya malipo wakati wa kununua bidhaa na huduma.

Awali kifungu hicho kilikuwa kikijumuisha kosa moja tu la mfanyabiashara kutotumia EFD au kutotoa risiti au kutotoa ankara ya malipo na adhabu, ilikuwa faini isiyopungua Sh1.5 milioni au kuzidi Sh 2.25 milioni au kifungo kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Adhabu iliyopendekezwa katika makosa hayo iwapo mtu atatiwa hatiani ni faini ya kiasi kisichopungua Sh3 milioni na kisichozidi Sh4.5 milioni au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Iwapo hakutakuwa na mabadiliko makubwa yatakayowasilishwa leo, muswada huo ulikuwa unapendekeza kuwa mbali na adhabu hiyo, atakayekutwa na makosa hayo pia atatakiwa kulipa faini mara mbili ya kodi aliyokwepa au kifungo kisichopungua miaka mitatu.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani zinaeleza kuwa kamati inapendekeza adhabu hiyo ipunguzwe angalau faini iwe isiyozidi Sh 30,000 na kifungo kisichozidi miezi sita.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia alisema iwapo kuna jambo hilo itajulikana leo bungeni atakaposoma mapendekezo ya kamati yake.

Muswada huo utawasilishwa leo kwa mara pili na kujadiliwa na wabunge kabla ya kuupitisha baada ya kuahirishwa mara mbili kutokana na Kamati ya Bajeti kutokamilisha kazi yake kwa wakati.

Awali zilikuwepo taarifa kuwa kulikuwa na mvutano kati ya kamati na baadhi ya wabunge waliotaka mapendekezo yao yazingatiwe yakiwamo ya kupinga kuanzishwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye huduma za utalii na kodi ya usajili wa bodaboda.

Lakini jana, Ghasia alieleza kuwa hakukuwa na mvutano wowote na kwamba wabunge wenye mapendekezo ya majedwali ya marekebisho walishauriwa kuyawasilisha bungeni.

Alisema sababu ya kuchelewesha muswada huo ni ufinyu wa muda wa kamati kukutana na Waziri wa Fedha na Mipango na pia wajumbe kuchambua kwa kina masuala yaliyomo kutokana na kuwepo mapendekezo ya maboresho ya sheria nyingi.

“Tofauti na miaka ya nyuma, bajeti imesomwa Jumatano, tulipumzika Alhamisi na siku zote hizo waziri alikuwa bungeni alikosa nafasi ya kukaa na alianza kukaa na kamati Ijumaa iliyopita hivyo muda ulitubana.

“Ila tumeshamaliza tangu jana saa nane usiku na tunahitaji taarifa iandikwe na kusahihishwa hivyo tuliomba Serikali itusubiri na kesho (leo) muswada utaingia bungeni,” alisema.

Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kuwa tarehe ya mwisho ya muswada huo kuingia bungeni ilikuwa jana lakini kutokana na kamati kutomaliza kazi yake ilibidi wasubiri ila leo utawasilishwa na kujadiliwa.

Muswada huo unawasilishwa huku wabunge wengi wakionyesha kutoridhishwa na baadhi ya hatua za kikodi zilizochukuliwa na Serikali wakisema zitawaumiza wananchi.

Mbunge wa Nzega Mjini(CCM), Hussein Bashe alieleza jana kuwa amejiandaa kumbana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwa kupeleka jedwali la marekebisho la kuondoa ongezeko la kodi ya usajili wa magari, bodaboda na mitumba.

Bashe aliwaambia wanahabari bungeni jana kuwa marekebisho hayo atayawasilisha leo.

Alisema marekebisho mengine ni kodi katika utalii, kufuta kodi katika mazao yasiyosindikwa, uhamishaji wa fedha na Sheria ya Mawasiliano ambayo inalazimisha makampuni ya simu kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Alipinga kulazimisha kampuni za simu kujisajili katika soko hilo ndani ya miezi sita kwa sababu hiyo itaua thamani za kampuni hizo. Alisema badala yake Serikali iweke vivutio kama kupunguza kodi mbalimbali, hali itakayofanya kampuni si tu za simu bali na nyingine kujiunga na soko hilo.

“Pia nimeishauri vyanzo vingine vya mapato ambavyo havitaathiri bajeti kuu. Wao kama watahitaji mabadiliko ya sheria nyingine kuwezesha vyanzo vipya walete kwenye mkutano wa mwezi wa tisa,”alisema.

Alivitaja vyanzo vipya vya mapato kuwa ni pamoja na uvuvi katika bahari kuu ambapo kutakuwa na mapato ya Sh200 bilioni.

“Kwa kuanzisha soko la madini, watu wawe wanaingia na madini yao bila kutozwa ushuru tutapata fedha kwa watu kulala katika hoteli, kununua vitu na tutakayotoza kwa kuuza madini nje ya nchi,”alisema.

Hata hivyo, juzi jioni wakati Dk Mpango akizungumza na wanahabari katika mkutano wa dharura alionyesha kutupilia mbali sehemu kubwa ya mapendekezo ya wabunge yakiwamo kuondoa VAT katika huduma za utalii na kodi ya usajili katika bodaboda na magari.

Alisema hata kabla ya pendekezo la VAT kwenye utalii, Tanzania bado ilikuwa na watalii wachache kuliko washindani wake kama Kenya na Afrika Kusini lakini mapato yalikuwa makubwa.

“Watalii hawangalii vigezo vya kodi pekee. Wanaangalia hali ya usalama, miundombinu ya hoteli, barabara, hospitali bora na vivutio vizuri.”

Katika hoja ya wabunge kuondoa kodi ya usajili wa bodaboda iliyopanda kutoka Sh150,000 hadi Sh 250,000, Dk Mpango alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kulipa kodi na Rais ameshaonyesha mfano kwa kubali kukatwa kodi katika kiinua mgongo chake hivyo wamiliki hao wa pikipiki hawana namna zaidi ya kuilipa kodi hiyo.

Ni pendekezo moja tu la wabunge na wadau lilizingatiwa ambalo ni kufuta pendekezo la awali la ufutaji misamaha ya kodi kwa taasisi za dini kwa maelezo kuwa iwapo lingetekelezwa lingechelewesha utoaji wa huduma za elimu na afya kwa wananchi kupitia taasisi hizo.

Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Atakayeshindwa kutoa au kudai risiti kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyopungua shilingi milioni 3. Atakayeshindwa kutoa au kudai risiti kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyopungua shilingi milioni 3. Reviewed by Zero Degree on 6/23/2016 01:29:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.