Loading...

Rais Magufuli atengua uteuzi wa wakuu wa wilaya wapya watatu


RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa wakuu wa wilaya wapya watatu huku mmoja akiwa amebakiza muda mfupi kabla ya kula kiapo cha uadilifu, Ikulu, Dar es Salaam.

Imegundulika kuwa wawili waliteuliwa kimakosa na mmoja tayari ana wadhifa mwingine wa ubunge.

Akitoa ufafanuzi juu ya hatua hiyo Ikulu Dar es Salaam jana, wakati wa kuapisha wakuu wa mikoa wapya watatu na shughuli ya kula kiapo cha uadilifu kwa ma-DC wapya 139, Dk Magufuli alisema alitengua uteuzi wa Fikiri Avias Said kwa kuwa jina lake lilikosewa.Alisema kwamba Mkuu wa Wilaya halali wa Ikungi mkoani Singida ni Miraji Mtaturu. Mtaturu alikuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza.

Aidha, Dk Magufuli alisema ametengua uteuzi wa Fatma Toufiq kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kwa kuwa tayari mteule huyo ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM).

Badala yake, nafasi hiyo imezibwa na Agnes Hokororo aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia chama hicho tawala. Katika Serikali ya Awamu ya Nne, Toufiq alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

“Nilishasema katika utawala wangu, kila kazi itakuwa na mtu mmoja ili kuwe na ufanisi katika utendaji. Mtu mmoja, kazi moja,” alisisitiza Rais Magufuli akifafanua kuhusu Fatma Toufiq.

Mwingine ‘atumbuliwa’

Ikulu Kamishna wa Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda alimtoa nje ya Ukumbi wa Ikulu kabla ya kiapo cha uadilifu mteule wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Emile Yotham Ntakamulenga baada ya kubainisha kuwa uteuzi wake ulikosewa na kwamba nafasi hiyo kihalali ni ya Nurdin Babu.

“Kwa heshima naomba Ntakamulenga utupishe ukumbini, haya mambo yanatokea sana, pole,” alisema Jaji Kaganda huku Ntakamulenga akitoka ukumbini hapo.


Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Mteule wa Serengeti, Emile Ntakamulenga akiondoka ukumbini, Ikulu, baada ya Kamishna wa Sekretarieri ya Maaili ya Vionozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda kumuomba atoke baada ya kubainika kasoro kwenye uteuzi wake wakati wa hafla ya kuwalisha kiapo Wakuu wa Wilaya Wateule iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana.

Babu alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani na amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi. Wakuu wa mikoa Wakuu wa mikoa walioapishwa ni Dk Binilith Mahenge wa mkoa wa Ruvuma, Dk Charles Mlingwa wa mkoa wa Mara na Zainab Telack wa mkoa wa Shinyanga.


ZeroDegree.
Rais Magufuli atengua uteuzi wa wakuu wa wilaya wapya watatu Rais Magufuli atengua uteuzi wa wakuu wa wilaya wapya watatu Reviewed by Zero Degree on 6/30/2016 08:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.