Polisi watawanya mahafali mengine ya umoja wa wanafunzi vyuo vikuu Chadema [ CHASO ]
Jeshi la Polisi mkoa Kilimanjaro jana liliwatawanya wahitimu wa vyuo vikuu kupitia umoja wa Chadema (Chaso), waliokuwa wamekusanyika mjini Moshi kwa ajili ya mahafali yao.
Dalili za ‘kibano’ hicho zilianza kuonekana asubuhi wakati polisi na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wakiwa wamejihami kwa mabomu ya machozi, walipozingira hoteli ya Keys inayomilikiwa na Philemon Ndesamburo.
Hoteli hiyo iliyopo maeneo ya Kwa Alfonsi nje kidogo ya mji wa Moshi, ndipo ambako mahafali hayo ambayo yalikuwa yahusishe wahitimu 70 kutoka vyuo vikuu vinne yalikuwa yafanyike.
Wanafunzi hao ni kutoka Chuo Kikuu cha Mwenge (Mwekau), Chuo cha Kikuu cha Ushirika Moshi (Mocu), Chuo Kikuu cha Masoka na Chuo Kikuu cha Tiba KCMC (KCMU Co).
Hata hivyo, polisi wakiwa na magari yaliyokuwa yakipeperusha bendera nyekundu, walivamia hoteli hiyo na kuwataka wahitimu hao kutawanyika kwa amani, kwa vile mikusanyiko ya aina hiyo imezuiwa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chadema (Bavicha) mkoani Kilimanjaro, Dickson Kibona alilaani tukio hilo akisema hakukuwa na sababu yoyote ya kuzuia mahafali hayo.
“Wamezuia bila sababu yoyote na hii inakiuka misingi ya kidemokrasia, Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa,” adai Kibona.
Kibona alidai kama isingekuwa kuhofia maslahi ya kibiashara ya Hoteli ya Keys ambapo kulikuwapo pia watalii, wangegoma kuondoka kwa kuwa hawakuvunja sheria yoyote ya nchi.
Source: Mtembezi
ZeroDegree.
Polisi watawanya mahafali mengine ya umoja wa wanafunzi vyuo vikuu Chadema [ CHASO ]
Reviewed by Zero Degree
on
6/20/2016 10:35:00 AM
Rating: