Loading...

Asilimia 95 tunaumwa magonjwa zaidi ya matano.


Wanaamka asubuhi, wanakwenda kazini, wengine kwenye biashara zao na wengine shuleni. Wanakula, wanakunywa, wanaabudu na wanacheza lakini kumbe wote wanaumwa.

Tena hawaumwi ugonjwa mmoja tu bali zaidi ya matano. Hii ni ripoti mpya iliyotolewa na jarida la kimataifa la Sayansi na Tiba, la Lancet.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 95 ya watu duniani wanaumwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo magonjwa matano ambayo watu wengi wanaugua duniani ni maumivu ya mgongo, msongo wa mawazo, ukosefu wa madini ya chuma, maumivu ya shingo. Magonjwa mengine ni yanayotokana na uzee, kama usikivu hafifu na ulemavu.

Hivyo basi kama asilimia 95 ya watu wanaumwa, hiyo ni sawa na kati ya watu 20 unaowaona barabarani, ni mmoja tu mwenye afya njema kwa asilimia 100. Hiyo ni sawa na asilimia 4.3 tu, ya watu wote duniani. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka jana kuhusu mzigo wa magonjwa kidunia na kuchapishwa na Lancet, watu 2.3 bilioni (sawa na asilimia 95) wanaumwa magonjwa zaidi ya matano.

Utafiti unaeleza kuwa katika kipindi cha miaka 23 iliyopita magonjwa yaliyoongoza kwa kuathiri watu wengi ni maumivu ya mgongo, msongo wa mawazo, ukosefu wa madini ya chuma, maumivu ya shingo.

Magonjwa mengine ni yanayotokana na uzee, kama usikivu hafifu na ulemavu. Kwa mwaka 2013, matatizo ya maumivu ya mgongo, shingo, akili, msongo wa mawazo, magonjwa yatokanayo na dawa za kulevya au pombe yalikuwa ni nusu ya magonjwa yote duniani.

Kwa mfano, kisukari kiliongezeka kwa asilimia 43 katika miaka 23 iliyopita. Hata hivyo kiwango cha vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kimeongezeka kwa asilimia tisa.

Katika utafiti huo, madaktari walifanya utafiti kwa kutumia sampuli za watu 35,620 kutoka katika nchi 188 katika kipindi cha 1990 hadi 2014.

Lengo lilikuwa kuangalia ukubwa wa ulemavu, maradhi na mfumo wa afya. Kadhalika walichukua sampuli za magonjwa sugu na yasiyoambukiza kwa kuangali yanaathiri watu gani na kwa kiasi gani.

Mtafiti mkuu katika utafiti huo kutoka Chuo Kikuu cha Washingyon, USA Dk Theo Vos anasema waliangalia madhara zaidi ya 2337 ambayo yanaweza kusababisha watu kuugua magonjwa matano makuu.

Magonjwa 10 sugu

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na msongo wa mawazo yalikuwa ni magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha ulemavu duniani kote.

“Magonjwa hayo yalisababisha madhara kuliko hata kisukari, pumu na magonjwa ya mfumo wa upumuaji,” alisema Dk Vos.

Kidunia, namba ya watu wenye magonjwa zaidi ya moja imeonekana kuongezeka kadri umri unavyosogea.

Idadi ya watu wenye maradhi zaidi ya 10 iliongezeka kwa asilimia 52 kutoka 1990 hadi 2014.

Kadhalika utafiti ulieleza kuwa kuna sababu nane ambazo ndicho chanzo cha watu kuwa na magonjwa sugu. Magonjwa hayo sugu ni yale yanayoathiri asilimia 10 ya watu duniani.

Sababu hizo ni kichwa kisababishwacho na wingi wa kazi au mshtuko. Ukosefu wa damu, ukosefu wa madini ya chuma, malengelenge sehemu za siri, maumivu ya kichwa yasiyokoma, minyoo wakubwa, meno, ukosefu wa sukari na uziwi utokanao na uzee.

Watafiti hao walisema yapo magonjwa yanayosababishwa na maradhi ya kisukari, kwa mfano kushindwa kufanya kazi kwa mishipa ya fahamu, matumizi makubwa ya dawa za maumivu na maumivu au kufa ganzi kwa viungio vya mwili, kiuno na magoti.

Profesa Vos anasema chanzo kikubwa cha magonjwa hayo ni watu kutotilia maanani kwa mfano, magonjwa ya akili katika nchi zinazoendelea hayapewi kipaumbele,

“Kufanyia kazi masuala haya, kunahitaji mabadiliko makubwa ya kiafya duniani kote, lakini suluhisho siyo kuwaongezea watu muda wa kuishi hadi wawe wazee, kwa sababu wengine wanaendelea kuishi na magonjwa yanayotesa, wanatakiwa kuwa na afya,” anasema

Akizungumzia ripoti hiyo, Daktari Bingwa wa Afya ya Jamii na Familia, Ali Nzige, wa Hospitali ya Al Hilal, anasema utafiti huo una ukweli hasa katika nchi zinazoendelea.

Anasema kuna sababu nyingi za watu kuumwa ikiwamo mazingira machafu, maji yasiyo safi na salama, mlo duni, vyakula vya kusindikwa na foleni.

Dk Nzige anatoa mfano kuwa asilimia 20 ya wagonjwa wa kisukari hapa nchini ni watoto.

“Kwa mfano Wamarekani wanaogua kisukari ni 24 milioni lakini wanaojijua ni 18 milioni na wasiojijua ni milioni sita. Hii inadhihirisha kuwa watu wengi hawajijui kama wanaumwa,” anasema

Asilimia 20 ya wagonjwa wa kisukari Tanzania ni watoto. Ipo haja ya kuwa na takwimu za wanaogua jkt itasaidia vijana wawwe na afya njema.

Anataja sababu nyingine ya watu kuumwa ni uzito kupita kiasi, kwa mfano anasema mwanaume mwenye afya kwa wastani anatakiwa awe na kilo 68 na urefu wa futi 5 na inchi 10.

Mwanamke kabla hajashika mimba anatakiwa awe na kilo 58 na urefu wa sentimita 164. Kwa sababu akishika mimba lazima uzito wake uongezeke.

“Mtu akiwa na unene kupita kiasi lazima apate maumivu ya mgongo, miguu, tunatakiwa tuwe na afya kwa namna nyingi, kwa nje na kwa ndani,” anasema.

Dk Nzige anatoa mfano wa hapa nchini kuwa katika kila watu wazima watatu, mmoja ana shinikizo la damu.

Anasema maradhi mengi yanayowakumbatia watu yanatokana na kula vibaya, kutofanya maoezi na msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa maisha, foleni au machafuko.

“Zipo sababu nyingi, ukikaa siku nzima bila kufanya kazi hauna tofauti na mtu ambaye amevuta sigara 14, lakini wazazi nao wanatakiwa kuwa waangalifu, baadaye hakutakuwa na mtoto mwenye meno imara, kwa sababu ya kuzagaa kwa pipi hapa jijini,” anasema.


Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Asilimia 95 tunaumwa magonjwa zaidi ya matano.  Asilimia 95 tunaumwa magonjwa zaidi ya matano. Reviewed by Zero Degree on 7/01/2016 07:14:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.