Loading...

Mahakama ya mafisadi kuanza kazi na kesi hizi 10.

WAKATI mchakato wa kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi ukiendelea, kuna taarifa kuwa vigogo kadhaa waliohusika na kashfa mbalimbali zikiwamo 10 zilizolikumba taifa kwa nyakati tofauti ndiyo watakaokuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuguswa na rungu la mahakama hiyo itakayokuwa chini ya Mahakama Kuu.

Uchunguzi umebaini kuwa miongoni mwa vigogo hao, ni wale wote ambao uchunguzi unaoendelea kufanywa na vyombo mbalimbali vya dola utabaini kuwa wanahusika katika kashfa zenye thamani ya mabilioni ya fedha, baadhi zikiwa ni za escrow, utoroshaji wanyama hai wakiwamo twiga, ulipaji mishahara hewa kwa watumishi hewa wa umma, ufisadi kwenye miradi mbalimbali ya halmashauri na pia ufisadi uliotokea kwenye taasisi mbalimbali za umma zikiwamo za Bandari, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Bandari na pia Mamlaka ya Kodi (TRA), likiwamo sakata la hivi karibuni la kuwapo kwa mtu aliyekuwa akijiingizia Sh. milioni 7 kila dakika.

Chanzo kutoka ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria kilisema kuwa vigogo wengine walio katika uwezekano mkubwa wa kutangulizwa katika mahakama hiyo wanaweza kuwa wahusika wa kashfa kama ya Lugumi pindi uchunguzi ukikamilika na kuonekana kuwa kuna watu walijinufaisha binafsi, mikataba ya kifisadi katika halmashauri mbalimbali nchini na pia manunuzi hewa ya bidhaa mbalimbali katika taasisi nyingine za umma.

“Mahakama hii itaanza kazi kwa kishindo… kuna kashfa zaidi ya 10 zinaendelea kuchunguzwa na pindi kazi rasmi itakapoanza, kutakuwa na mshindo mkuu,”.

Chanzo hicho kilisisitiza kuwa makosa yatakayoshughulikiwa, kama sheria hiyo itaridhiwa na Rais na kutangazwa kwenye gazeti la serikali, ni yote yanayoangukia kwenye rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi na kulisababishia taifa hasara ama uharibifu wa mali au raslimali zenye thamani isiyopungua Sh. bilioni moja.

Ilielezwa kuwa kashfa nyingine zitakazowatanguliza vigogo kortini ni zile zinazohusiana na sheria ya misitu, ikiwamo ya usafirishaji holela wa magogo nje ya nchi na uharibifu wa misitu.

“Makosa kwa mfano ya kashfa ya kama ya Escrow, utakatishaji fedha (mabilioni ya Uswisi), mishahara hewa uchunguzi wake ukishafanyika na kubainika, watuhumiwa wake ndiyo watafikishwa katika mahakama hiyo haraka iwezekanavyo,” kiliongeza chanzo hicho.


Source: Mtembezi
ZeroDegree.
Mahakama ya mafisadi kuanza kazi na kesi hizi 10. Mahakama ya mafisadi kuanza kazi na kesi hizi 10. Reviewed by Zero Degree on 7/11/2016 11:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.