Loading...

Matumizi ya Tiketi za karatasi kwenye magari ya mwendokasi kusitishwa tar 30 Julai.

KAMPUNI ya Usafirishaji ya mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (UDART) inatarajia kusitisha matumizi ya tiketi za karatasi ifikapo Julai 30 mwaka huu.

Uamuzi huo unalenga kudhibiti foleni za kununua tiketi za karatasi kutokana na idadi kubwa ya abiria; kati ya 150,000 na 200,000 wanaotumia usafiri wa mabasi hayo kwa siku.

“Kwa siku abiria wapatao laki moja na nusu hadi laki mbili wanatumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka kila siku, sasa kumekuwa na foleni vituoni na pia tunakusanya magunia na magunia ya karatasi na kuna maeneo mengine uchafu unakuwa mwingi,” Mkurugenzi Mtendaji wa UDA-RT, David Mgwasa aliwaambia waandishi wa habari jana.

Hata hivyo, kusitishwa huko kwa tiketi za karatasi, kunalenga watu wazima pekee wanaolipa Sh 650. Wanafunzi wanaolipa Sh 200, wataendelea kutumia tiketi za karatasi ambazo zitakuwa zikipatikana kwenye vituo vya mabasi.

Mgwasa alisema licha ya hatua hiyo kulenga kupunguza foleni kwenye vituo, pia itaondoa uchafu unaotokana na tiketi za karatasi.

Wakati huo huo, alisema kutokana na mpango huo wa kusitisha tiketi, kuanzia leo kampuni imepunguza gharama ya ununuzi kutoka Sh 5,000 kwa tiketi za hadi Sh 2,000, Sh 500 itakuwa gharama ya kadi na Sh 1,500 ni nauli.

“Kuanzia kesho (leo) kadi zitauzwa kwa gharama ya Sh 2,000 kwenye vituo vyote vya mabasi ya mwendokasi,” alisema.

Mgwasa alisema tangu kuanza kuuzwa kwa kadi hizo kwa gharama ya Sh 5,000 tayari kadi 55,000 zimeshanunuliwa na kubakia kadi 150,000 ambazo ziko kwenye promosheni ya kuuza kadi kwa Sh 5000.

Alisema baada ya kadi hizo kuisha, abiria atalazimika kununua kadi hiyo kwa thamani ya Sh 5,000 bila kuwekewa fedha za nauli kama ilivyokuwa awali.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Maxcom Afrika (MaxMalipo), Deogratius Lazari alisema wamejipanga kuhakikisha tiketi za kadi zinapatikana kwenye vituo vya mabasi. Aliwataka wateja kuhakikisha wanaweka salio katika vituo hivyo.

“ Kampuni za simu ziko katika hatua ya mwisho za kukamilisha mifumo yao ili abiria aweze kuongeza salio kupitia mitandao ya simu ila kwa sasa abiria wanatakiwa kutumia vituo vyetu vya mabasi na wakala wa max malipo,” alisema.

Mabasi ya haraka yalianza kutoa huduma Mei mwaka huu kwa kuanza na tiketi za karatasi na baadaye, kuanzishwa utaratibu wa kadi ambao haujaitikiwa kwa kiwango kikubwa.


ZeroDegree.
Matumizi ya Tiketi za karatasi kwenye magari ya mwendokasi kusitishwa tar 30 Julai. Matumizi ya Tiketi za karatasi kwenye magari ya mwendokasi kusitishwa tar 30 Julai. Reviewed by Zero Degree on 7/11/2016 10:58:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.