Loading...

Mbowe asakwa na Polisi.

JESHI la Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamsaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kwa ajili ya kumhoji kuhusiana na mambo mbalimbali.

Kamishna wa Polisi katika kanda hiyo, Simon Sirro, aliiongea na waandishi wa habari kwa njia ya simu jana kuwa tayari wameshawasiliana na mwenyekiti huyo wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusiana na wito wa kumtaka afike kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Kati jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano hayo.

Akifafanua zaidi kuhusiana na swali aliloulizwa juu ya taarifa zilizozagaa kwenye mtandao kuwa wamemuita Mbowe kwa mahojiano, Sirro alisema ni kweli waliwasiliana naye kwa njia ya simu juzi usiku na kumtaka afike leo kwa mahojiano kufikia saa 7:00 mchana.

Sirro hakuwa tayari kueleza kwa undani sababu za kumuita Mbowe wala kile wanachotarajia kumhoji, ingawa inadhaniwa kuwa miongoni mwa mambo atakayohojiwa ni pamoja na taarifa za chama chake kuwa kinajiandaa kufanya mikutano na maandamano nchi nzima ifikapo Septemba Mosi kupitia operesheni yao iitwayo ‘Ukuta’.

Polisi wamekuwa wakizuia mikutano ya hadhara ya kisiasa kutokana na kile wanachoeleza kuwa ni sababu za kiusalama, huku Rais John Magufuli akikazia amri hiyo wakati akiwahutubia wananchi mkoani Singida juzi kwa kusisitiza kuwa kamwe hataruhusu shughuli za aina hiyo kwa sasa.

Akizungumza jana, Kamishna Sirro alisema: “Amepigiwa simu yake juzi na kupewa tarifa ya kutakiwa kuja kesho (Jumapili) mchana kwa ajili ya kuhojiwa. Suala la kujua tunachotaka kumhoji hatuwezi kusema kwa sasa… ni mpaka afike mwenyewe ndipo atafahamu ni kipi atakachohojiwa.”

Jana, katika mitandao mbalimbali ya ya kijamii, kulikuwa na taarifa zinazoeleza kuwa Mbowe ameitwa Polisi ili kuhojiwa. Hata hivyo, alipoulizwa jana kuhusiana na kutakiwa Polisi, Mbowe alisema hana tarifa ya jambo hilo.

“Sina taarifa ya kuitwa polisi… halafu siyo vizuri kuamini sana habari za kwenye mitandao. Umefanya vizuri kuuliza, wakati mwingine habari za kwenye mitando huwa ni za uongo,” alisema Mbowe.

UKAWA WAITA VIONGOZI WA DINI, LOWASSA KUNGURUMA LEO


Wakati huo huo, muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umewaita viongozi mbalimbali wa dini kwa nia ya kuzungumza nao kuhusiana na mambo mbalimbali ikiwamo mwenendo wa kisiasa nchini.

Akizungumza wakati wa mazishi ya baba wa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro jana, Mbowe alisema Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia, ndiye anayeongoza kikao hicho jijini Dar es Salaam kinachotarajiwa kumalizika baada ya siku mbili kuanzia jana.

Mbali na Chadema na NCCR-Mageuzi, vyama vingine vinavyounda Ukawa ni NLD na Chama cha Wananchi (CUF).

Aidha, taarifa nyingine zimedai kuwa aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa kupitia Chadema, Edward Lowassa, anatarajiwa kunguruma leo kupitia mahojiano maalum ya televisheni. Atahojiwa na mtangazaji Tido Mhando na baadhi ya mambo anayotarajiwa kuyazungumzia ni pamoja na hali ya kisiasa nchini. Hata hivyo, hakukuwa na taarifa rasmi kuhusiana na mahojiano hayo ya Lowassa.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, Lowassa aliyehamia Chadema baada ya kuenguliwa katika orodha ya waliokuwa watia nia 38 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alishika nafasi ya pili baada ya kupata asilimia zaidi ya 39 ya kura halali zilizopigwa. Rais John Magufuli alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 58.46.

Source: Nipashe(IPPMedia)
ZeroDegree.
Mbowe asakwa na Polisi.   Mbowe asakwa na Polisi. Reviewed by Zero Degree on 7/31/2016 09:13:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.