Loading...

Siri ya Magufuli kumbakiza Kinana.

SIKU moja baada ya Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli, kukataa ombi la kujiuzulu la wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho wakiongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.


Baadhi ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC-CCM), wamesema kuwa sababu kubwa mbili zimemfanya achukue uamuzi huo.

Juzi baada ya kutangazwa kuchaguliwa kwa asilimia 100 na wajumbe 2,398 waliohudhuria Mkutano Mkuu, Magufuli, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisoma barua aliyoandikiwa na Kinana, ikimtaarifu juu ya kujiuzulu kwake na sekretarieti yote.

Hata hivyo, pamoja na kuibakiza sekretarieti, bado Magufuli aliahidi kuunda kikosi kazi cha kufuatilia mali za chama hicho na kuitaka sekretarieti kutoa ushirikiano kwenye suala hilo.

Mwenyekiti huyo mpya wa CCM, pamoja na kuahidi kufuatilia mali zote za chama hicho kuanzia kwenye ngazi ya chini, lakini pia amepania kusafisha uozo uliomo kwenye chama hicho.

Mmoja wa wajumbe wa NEC-CCM, aliiambia Nipashe jana kuwa kwa mujibu wa ratiba ambayo walikuwa wamepewa, baada ya kupitisha jina la Magufuli kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, jana ilikuwa ikutane kuanzia saa 4:00 asubuhi ili kupitisha majina ya sekretarieti mpya.

“Unajua kwa kawaida Halmshauri Kuu hukaa baada ya Mkutano Mkuu, kwa hiyo yeye jana aliamua kutumia mkutano mkuu kuwabakisha walewale waliokuwepo tangu mwanzo, ndiyo maana aliwahoji kama wanaafiki uamuzi wake alioufanya,” alisema mjumbe huyo.

Mjumbe mwingine alitaja sababu mbili za Magufuli kuchukua uamuzi huo kuwa ni kutokana na kutaka kujua kwa undani chama na shughuli zake na pia apate watu wa kuwabana.

Aliongeza kuwa suala jingine muhimu ilikuwa sekretarieti kwa maana ya Kinana na timu yake wanatakiwa kusimamia kipindi hiki cha mpito baada ya Magufuli kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho.

“Kwa mfano, sasa hivi ndani ya chama kuna malalamiko kwamba fedha za kampeni nyingi sana zililiwa, kwa hiyo ni lazima mwenyekiti apitie ripoti ya uchaguzi mkuu, aichambue na ndani yake kuna mambo mengi ikiwamo hayo ya matumizi ya fedha na wanaotakiwa kufukuzwa kutokana na mambo waliyofanya wakati wa uchaguzi mkuu.

“Sasa akiwaondoa wote leo (jana), unadhani hata kama akipata kasoro kwenye ripoti hizo atamuuliza nani? Kwa hiyo mimi naona ametumia busara kuwabakiza hawa watendaji kwa sababu wenyewe ndiyo kila kitu,” alieleza mjumbe huyo kutoka moja ya mikoa ya pembezoni.

Mjumbe aliongeza kuwa Magufuli bila shaka ameona kuna matatizo mengi mathalani, lile la wafanyakazi wa chama wasiokuwa waaminifu kwani wengi wao waliajiriwa na sekretarieti iliyokuwapo kwa hiyo, kutokana na makosa waliyofanya itakuwa ni vizuri wakafukuzwa na walewale waliowaajiri.

“Wewe mtu umeamuajiri wewe na unajua ana mambo yake ambayo sio mazuri, halafu eti umeshindwa kumfukuza unanipa mimi ripoti nimfukuze, hicho ni kitu kisichowezekana, ndiyo maana kawaacha pale.

“Endapo angekubali wajiuzulu kama ambavyo walikuwa wameomba kwake ingekuwa ni kosa kubwa sana la kiufundi, mbali na kukosa watu wa kuwauliza mambo atakayokuja kuyakuta huko, lakini pia ni rahisi kwake kuwekewa mitego mingine na akishindwa tu watasema ‘unaona? Tulisema hakiwezi chama,” aliongeza mjumbe huyo.

Mjumbe huyo alitolea mfano wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, ambaye Magufuli alipotangaza safu yake ya makatibu wakuu wa wizara, alimuacha serikalini kuendelea kushika wadhifa wake huo, lakini baada ya muda mfupi uteuzi wake ulitenguliwa.

“Kwa hiyo usishangae akakaa na hiyo sekretarieti iliyo chini ya Kinana na ndani ya muda mfupi ukasikia ameitisha
Halmashauri Kuu na kutengua uteuzi wake na akatangaza timu nyingine, usitarajie kuwa Kinana atakaa miaka mingi, hilo sahau, pamoja na sifa zote alizomwagiwa hapa leo, tegemea chochote ndani ya muda mfupi,” alisema mjumbe huyo.

Alisema pia kwamba kutokana na kuwapo kwa malalamiko ya muda mrefu ya ufujaji wa fedha za chama hicho, itambidi kutumia timu hiyo iliyokuwa na uzoefu kuainisha na chanzo cha tatizo hilo na kama ndani ya sekretarieti kuna mtu anahusika na ufujaji huo naye bila shaka atawajibishwa.

Alisema timu itakaayoundwa na Magufuli, itakuwa na jukumu la kuhakikisha chama hicho kinaondokana na taswira ya rushwa kwamba ndiyo njia pekee ya kupata uongozi.

Alisema jambo hilo ambalo pia lilizungumziwa na Magufuli wakati akitoa shukrani kwa wajumbe wa mkutano mkuu, ni
jambo ambalo haliwezi kusimamiwa na sekretarieti iliyopo sasa kwa sababu baadhi yao wanakabiliwa za rushwa na matendo mengine maovu.

“Mimi nakwambia wewe, Magufuli hapendi mtu ambaye ananyooshewa kidole, na hiyo timu aliyosema anabaki nayo ina watu kibao wenye tuhuma na kwenye uchaguzi mkuu uliopita ndiyo tuhuma ziliongezeka zaidi, subiri tu unaona mengi.

Kwa sababu huku kwenye chama mambo yanaenda kwa vikao tofauti, suburi tu utaona kwa sababu kila kitu ataleta kwetu wajumbe wa halmashauri kuu tuamue,” alisema.

Pia Magufuli anakabiliwa na kazi ya kusafisha jumuiya za chama hicho, ambazo ni ile ya Vijana (UVCCM), Wanawake (UWT) na Wazazi.

Jumuiya hizo nazo pia zinakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufisadi kupitia miradi yake mbalimbali ikiwamo majengo na shule.

Pia zinakabiliwa na tuhuma za kuajiri watu wasio na sifa badala yake huangalia zaidi kujuana.

Jambo hilo, aliligusia pia Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Jakaya Kikwete, ambaye alisema tatizo hilo lipo zaidi kwa UWT.

Alisema kwa upande wa Jumuiya ya Wazazi, hali kama hiyo ilikuwapo, lakini sasa imerekebishwa kwa kiasi kikubwa.

Kutoka na hali hiyo, alisema Jumuiya ya Wazazi inabidi ijiangalie kwa sababu kuna uamuzi wa Halmashauri Kuu wa kuifuta na bado haujatekelezwa.

Kutokana na mambo hayo, ni jambo linalotarajiwa kuwa Magufuli anaweza kufumua jumuiya hizo kama ambavyo ameonyesha nia ya kufuta baadhi ya vyeo ikiwa ni pamoja na chipukizi wa chama na makamanda wa vijana.


Credits: IPPMedia
ZeroDegree.
Siri ya Magufuli kumbakiza Kinana. Siri ya Magufuli kumbakiza Kinana. Reviewed by Zero Degree on 7/25/2016 09:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.