Loading...

Takukuru yaivaa polisi ufisadi wa bilioni 60/-

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna Valentino Mlowola.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeanza kuchunguza kashfa ya Sh. bilioni 60 inayolikabili Jeshi la Polisi baada ya kuibuliwa na Rais John Magufuli hivi karibuni.

Rais Magufuli aliibua kashfa hiyo wakati akiwaapisha Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) baada ya kuwapandisha vyeo na kula kiapo cha uadilifu wa utumishi wa umma, Julai 18, mwaka huu Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Kuhusu kashfa hiyo, Rais Magufuli alieleza kuwa mwishoni mwa mwaka jana kuna mtu ndani ya Jeshi la Polisi alipewa kazi ya kununua sare za Jeshi la Polisi na kupewa fedha lakini hakutimiza wajibu huo hadi mwaka huu.

“Naomba suala hili lifuatiliwe, wapo wanaosema fedha zilizotolewa zilikuwa Sh. bilioni 20, wengine Sh. bilioni 60, kwa hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira wewe ni mwanasheria, waliohusika wapelekwe mbele ya haki,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumza na Nipashe jana kwa simu, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna Valentino Mlowola, alisema suala hilo walianza kulifanyia kazi tangu walipopata taarifa.

Alisema hadi sasa uchunguzi unaendelea kuhusu suala hilo kwani tuhuma zozote zenye viashiria vya rushwa zinapotokea hufanyiwa kazi mara moja na taasisi hiyo.

“Zoezi hili tulilianza siku ileile aliyosema Rais, uchunguzi unaendelea kuhusu suala hilo, na uchunguzi wowote utakaousikia wewe uwe wa kiuchumi, kijamii au kisiasa sisi tunaufanyia kazi,” alisema Mlowola.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Rwegasira, ambaye alisema kashfa ya ubadhirifu wa Sh. bilioni 60 za kununua sare za polisi iliyoibuliwa na Rais Magufuli, bado inachunguzwa na vyombo husika.

Rwegasira alisema vyombo vinavyofanya kazi hiyo havikupewa muda maalumu wa kumaliza kazi hiyo.

“Kwa sasa siwezi kusema chochote kwa sababu ripoti ya uchunguzi wake bado sijaipata na unajua mtu anapochunguza hawezi akawa anakupa ripoti kidogo kidogo,” alisema Rwegasira.

Hatua hiyo inakuja baada ya Rwegasira kulieleza gazeti hili hivi karibuni kuwa kuwepo kwa kashfa nyingi katika Jeshi la Polisi kunalipaka tope jeshi hilo na kwamba wana mpango wa kupitia upya mikataba yote ya jeshi la polisi, lengo likiwa ni kulisafisha jeshi hilo.

Alisema kashfa zinazotokea sasa katika jeshi la polisi zinapunguza uaminifu na kupoteza imani kwa wananchi.

Kashfa hiyo ya Sh. bilioni 60 imeibuka siku chache tangu Meja Jenerali Rwegasira, amsimamishe kazi Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Frank Msaki kwa makosa ya kufanya malipo hewa ya posho ya chakula kwa watu wasio askari.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema Msaki alisimamishwa kazi kwa kufanya malipo hayo yanayofikia Sh. milioni 305.

Malipo hayo kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni ya kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2015/2016.

Kashfa nyingine iliyohusishwa na jeshi hilo ni ile ya mkataba iliyoingia na Kampuni ya Lugumi Enterprise Limited, ambayo ilitakiwa kufunga mashine za kutambua alama za vidole kwenye vituo 108 vya polisi nchini, hawakutekeleza vyema kazi hiyo licha ya kulipwa Sh. bilioni 34 kati ya Sh. bilioni 37 zilizokuwa kwenye makubaliano ya mkataba.

Bunge lilitoa miezi mitatu likielekeza kufanyiwa kazi kwa mapungufu yaliyojitokeza kwenye utekelezaji wa mkataba huo baada ya kamati iliyochunguza suala hilo na kubaini matatizo.

Pia Rais Magufuli aliwahi kuzungumzia anavyokerwa na mikataba mibovu inayohusishwa na Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za dola wakati alipofungua mkutano wa makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa serikali wa mikoa na wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi, uliofanyika Aprili 29, mwaka huu mjini Dodoma.

“Oysterbay (jijini Dar es Salaam) pale ni eneo ambalo ni very `prime’ (lenye thamani kubwa), kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba mnayoijua ninyi, akapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo yanafaa,” alikaririwa Rais Magufuli wakati akizungumzia suala hilo.

Source: IPPMedia
ZeroDegree.
Takukuru yaivaa polisi ufisadi wa bilioni 60/-   Takukuru yaivaa polisi ufisadi wa bilioni 60/- Reviewed by Zero Degree on 7/29/2016 09:54:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.