Loading...

Viunzi 6 Magufuli kuhamia Dodoma.

Rais John Magufuli, akiweka mkuki na ngao katika kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa katika Uwanja wa Mashujaa Mjini Dodoma jana.

Wakati serikali imetangaza kupeleka bungeni muswada wa sheria ya kuifanya Dodoma kuwa mji mkuu wa Tanzania, gharama za kuufanya mji huo kuwa makao makuu ya nchi ni Sh. trilioni 1.3.

Aidha, serikali imekiri kuwapo kwa changamoto sita ambazo zinapaswa kushughulikiwa ili kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.

Mara tu baada ya kukabidhiwa kijiti cha uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jumamosi iliyopita, Rais John Magufuli, alisema atahakikisha serikali inahamia Dodoma kufikia mwaka 2020. 

Pia Rais Magufuli alisisitiza agizo hilo wakati akituhutubia kwenye shughuli ya Siku ya Mashujaa iliyofanyika jana kitaifa mjini Dodoma.

“Nawahakikishia mimi na serikali yangu tutahamia Dodoma ndio maana mipango inafanyika kuepukana na vikwazo vya kuhamia hapa,” alisisitiza Rais Magufuli.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwekea msisitizo agizo hilo kwa kuahidi kuhamia Dodoma Septemba, mwaka huu, ikiwa na maana ya siku 36 kutoka sasa.

Akihutubia kwenye shughuli hiyo ya kukumbuka mashujaa , Majaliwa hakuishia kwa suala la yeye kuhamia tu, bali pia aliagiza mawaziri nao wamfuate huko ili kutekeleza agizo la Rais.

Akizungumza na Nipashe jana, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Dk. Abdallah Possi, alisema serikali iko mbioni kuliweka suala hilo kisheria.

Alisema serikali itawasilisha bungeni muswada wa sheria ya Dodoma kuwa mji mkuu wa Tanzania katika Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 utakaoanza Septemba 6, mwaka huu.

"Serikali inatarajia kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya Dodoma kuwa makao makuu. Tunatarajia kuwasilisha muswada huo katika mkutano ujao kwa sababu licha ya kuwa mwaka 1973 mji wa Dodoma ulitangazwa kuwa mji mkuu, lakini bado suala hilo lilikuwa kisera zaidi, halikuwa kisheria.’

"Ilianzishwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA). Hii ilianzishwa kisheria na imekuwa ikipangiwa bajeti. lakini hakuna sheria inayoitambua Dodoma kama mji mkuu," aliongeza kusema Dk. Possi.

ZINAHITAJIKA TRILIONI 1.3/-

Naye Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Mhandisi Paskasi Muragili, aliliambia Nipashe kuwa, zinahitajika Sh. trilioni 1.3 kutekeleza mpango huo, sawa na asilimia 4.4 ya bajeti yote ya serikali kwa mwaka huu wa fedha ambayo ni Sh. trilioni 29.5.

Mhandisi Muragili alisema: "Mpango huu ni mkubwa. Tunazungumzia ujenzi wa ofisi, nyumba za watumishi, barabara, umeme, maji, hospitali, maduka makubwa kwa ajili ya 'shopping', shule, hoteli na mambo mengine mengi muhimu."

"Katika makisio ya miaka miwili iliyopita, tulibaini zitahitajika Sh. trilioni 1.3 kukamilisha mpango huu, zikiwamo fedha za serikali na sekta binafsi, hivyo baadhi ya shughuli zitabebwa na 'private sector' (sekta binafsi) ambayo itabeba asilimia kubwa zaidi kwa mujibu wa makisio yetu.

Tutakaa tena kuangalia makisio mapya kuona serikali itabeba kiasi gani na `private sector' itachukua asilimia ngapi maana makisio yaliyopo sasa ni ya miaka miwili iliyopita.”

"Tutakamilisha mpango huu na huenda ikawa kabla ya muda uliosemwa kwa kuwahamisha awamu kwa awamu mradi tu kufikia 2020 wote wawe wameshahamia hapa Dodoma kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa Rais."

Mkurugenzi huyo alisema yanahitajika mambo makuu matatu kutekeleza mpango huo ambao walipanga kuukamilisha 2030. Aliyataja mambo hayo kuwa ni mpango, rasilimali fedha na utashi wa kisiasa.

"Tayari mpango upo kwa maana imeundwa CDA na tayari Rais ameshaonyesha utashi wa kisiasa wa kuagiza serikali ihamie hapa Dodoma kufikia 2020.

Nitoe wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa hii nzuri kwa kuja kuangalia maeneo ya kuwekeza kama viwanda, chakula, elimu, afya, huduma za hoteli, nyumba za makazi na usafirishaji," aliongeza kusema Mhandisi
Muragili.

VIGEZO KUWA MJI MKUU

Mtandao wa www.quora.com unabainisha vigezo 12 vya mji mkuu kuwa ni pamoja na uhakika wa usafiri wa umma, mpangilio mzuri wa mji husika na miundombinu mizuri (barabara, umeme, mawasiliano na mfumo wa majisafi na taka), uwe mji rafiki kwa watu wote (usibague aina ya watu wanaopaswa kuishi ndani yake), weledi (kiutawala) na uwe na taasisi nzuri za elimu na vifaa vya kufundishia.

Vigezo vingine ni urahisi na upatikanaji wa chakula bora, usalama wa uhakika (Mji Mkuu inapotokea vita huwa unatazamwa kwa karibu na maadui), jiografia (mfano katikati ya nchi husika kama vile Madrid - Hispania, Brasilia - Brazil) na uwe na sifa za kuwa kitambulisho cha taifa, serikali na siasa ya nchi husika.

Katika mahojiano na gazeti hili, Dk. Possi alikiri Dodoma kutokidhi baadhi ya hivyo, lakini akasisitiza Serikali ya Awamu ya Tano haitarudi nyuma katika kutekeleza azma yake ya kuihamishia serikali mjini humo.

Dk. Possi alizitaja changamoto sita ambazo zitapaswa kushughulikiwa ili mji wa Dodoma ufikie kiwango cha kuwa mji mkuu na kufanikisha utekelezaji wa azma ya serikali ya kuhamia huko.

HUDUMA ZA AFYA

Dk. Possi alisema upatikanaji wa huduma bora za afya mjini humo huenda ukawa changamoto katika siku za mwanzo kutokana na mji huo kuwa na hospitali moja ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) inayotoa huduma za kiwango cha kibingwa.

"Udom ni hospitali kubwa na ya kisasa. Ndiyo kwanza inaanza lakini ina vifaa vya kisasa. Itasaidia kwa kiasi kikubwa pamoja na hospitali ya mkoa na zile za watu binafsi. Lakini kadri watu watakavyoongezeka, suala hili itabidi liangaliwe," alisema Dk. Possi.

TAASISI ZA ELIMU

Ingawa hakutaka kulizungumzia sana suala la elimu kwa maelezo kuwa haliko chini ya wizara yake, Dk. Possi alikiri kuwapo kwa changamoto ya uhaba wa shule hasa za sekondari na za awali mjini Dodoma.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo alisema serikali imejipanga kukabiliana na changamoto hizo kadri watu watakavyokuwa wanaongezeka.

"Serikali inatambua kwamba hili ni suala lake, kuna uhaba wa shule hasa za sekondari na za awali Dodoma, lakini Wizara ya Elimu na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wanaweza kulizungumzia zaidi hili," alisema.

USALAMA

Msomi huyo alisema Dodoma pia itakabiliwa na changamoto ya kiusalama, lakini akadokeza kuwa, mji huo ni rahisi kuulinda kutokana na mindombinu yake kulinganisha na Dar es Salaam.

"Kila mkoa wa Tanzania una ulinzi, lakini pia Rais atakapohamia Dodoma, Ngome (makao makuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania) pia naamini italazimika kuhamia hapa ingawa pia hapa Dodoma tuna kambi kadhaa.

Hatuwezi kuyazungumzia zaidi haya masuala ya kiusalama lakini Tanzania haina uadui na nchi nyingine na tuna jeshi imara hata hivyo," alisema.

UHABA WA CHAKULA

Naibu Waziri huyo alikiri mkoa wa Dodoma kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa chakula katika baadhi ya wilaya zake, lakini akasisitiza hawawezi kuhofia njaa kuhamishia makao makuu ya nchi mjini humo.

Alisema kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara na reli na maendeleo ya kilimo cha kisasa kutasaidia kutatua changamoto hiyo.

MAKAZI

Dk. Possi alisema CDA kwa kushirikiana na Manispaa ya Dodoma wamefanya kazi nzuri kuupanga mji wa Dodoma na wanaendelea kushughulikia changamoto ya uhaba wa makazi mjini humo.

Alisema serikali pia inamalizia ujenzi wa makazi ya Waziri Mkuu na baadaye itaanza kujenga nyumba za mawaziri na watendaji wake wengine.

UHAKIKA WA USAFIRI

Kadhalika, kiongozi huyo wa serikali alikiri kuwapo kwa changamoto ya usafiri mjini Dodoma, lakini akasema serikali itatua changamoto hiyo kadri watu watakavyokuwa wakiongezeka.

"Hapa Dodoma usafiri unaotumika kwa sasa ni daladala, sijaona mabasi makubwa kama yale ya Dar es Salaam, lakini hili linatatulika kirahisi kwa kuleta magari kwa ajili hiyo," alisema Dk. Possi.

SABABU ZA KUCHELEWA KUHAMIA DODOMA

Naibu Waziri huyo alisema vita vya Kagera vya mwaka 1978/79 wakati Tanzania ilipovamiwa na majeshi ya kiongozi wa zamani wa Uganda, Idi Amin na anguko la uchumi la miaka ya 1980, ndizo sababu kuu zilizoichelewesha Dodoma kuwa Mji Mkuu wa Tanzania.

"Mipango mingi ya serikali iliathiriwa na mambo hayo mawili. Pia kuongezeka kwa idadi ya watu kumekuwa changamoto kubwa kwa serikali. Kumbuka asilimia 70 ya Watanzania wanapewa huduma za afya 'free' (bure), hivyo serikali kulazimika kutumia fedha nyingi kuhudumia wananchi badala ya kutekeleza mipango iliyopo," alisema.

Serikali ilishatangaza Dodoma kuwa mji mkuu wa Tanzania tangu mwaka 1973 lakini bado ofisi nyingi za serikali, ikiwamo Ikulu na balozi, ziko Dar es Salaam.

Source: IPPMedia
ZeroDegree.
Viunzi 6 Magufuli kuhamia Dodoma. Viunzi 6 Magufuli kuhamia Dodoma. Reviewed by Zero Degree on 7/26/2016 10:07:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.