Loading...

Hivi ndivyo bosi polisi alivyouawa na majambazi.

ASP, Thomas Njiku.
IMEFAHAMIKA kuwa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (ASP), Thomas Njiku (40), ambaye aliuawa kwenye mapambano na majambazi ana mwezi mmoja tu tangu ahamishiwe Kanda Maalum ya Dar es Salaam, akitokea mkoani Manyara.

Ilielezwa na vyanzo mbalimbali kuwa Njiku alikuwa Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Majambazi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Marehemu Njiku aliuawa alfajiri ya jana eneo la Vikindu, wilayani Mkuranga mkoani Pwani, wakati akiongoza kikosi maalum cha kuwasaka watu wanaosadikika kuwa ni majambazi.

Ilielezwa kuwa marehemu pia alikuwa akionekana mara kadhaa kwenye Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam akiongoza misafara ya ulinzi wa askari waliokuwa wakisindikiza watuhumiwa wa kesi za ugaidi.

“Kila mara alikuwa akija na msafara watuhumiwa wa makosa ya ugadi katika kesi ya wakina Sheikh Faridi Hady Ahmed na wenzake zaidi ya 20,” kilieleza chanzo hicho.

Pia kilielezai kuwa marehemu Njiku alikuwa akiongoza misafara ya kesi za viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani kama Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) walipokuwa wanafikishwa mahakamani kwa kesi mbalimbali.

Chanzo kingine katika Mahakama hiyo kilisema hadi juzi marehemu alikuwa katika Mahakama hiyo akitekeleza majukumu yake kabla ya alfajiri ya jana kwenda kwenye tukio hilo lililokatisha uhai wake.

“Tulikaa naye juzi (Jumatano) tukawa tunakunywa naye chai hapa Kisutu, tukawa tunapiga porojo za maisha ya hapa na pale na nakumbuka aliniambia nisilipie chai yangu atalipa yeye, ni mtu mpole na mcheshi alikuwa rafiki yangu sana,” kilieleza chanzo hicho.

Mmoja wa askari aliyekuwa akifanya kazi na Njiku alimwelezea kuwa ni mchapa kazi na hodari kwenye utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.

“Siwezi kumzungumzia sana marehemu Njiku kwa sababu nimemfahamu kwa kipindi cha mwezi mmoja tu tangu ahamishiwe hapa, lakini alikuwa mchapa kazi na anayejituma sana,” alisema mmoja wa askai hao, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Namna afande Njiku alivyouawa

Umauti ulimkuta afande Njiku muda mfupi baada ya vikosi vya Jeshi la Polisi vikiwa na silaha mbalimbali kuwasili kwenye nyumba hiyo meeneo ya Vikindu.

Njiku ambaye alikuwa ndiye kiongozi wa msafara wa vikosi hivyo vya polisi alifariki baada mtuhumiwa anayedaiwa kuwa ni jambazi kumfyatulia risasi ambazo zilimpata kichwani kusababisha kifo chake.

Kifo cha afande Njiku kimeongeza idadi ya askari waliouwawa ndani ya wiki moja pekee kufikia watano baada ya wale wanne waliouwawa na majambazi Mbande Wilaya ya Temeke.

Njiku aliuawawa mara tu askari hao walipofika karibu na nyumba hiyo na yeye kuanza kuwapanga vijana wake kwa kutoa maelekezo ya namna ya kukabiliana na watuhumiwa waliokuwa ndani ya nyumba hiyo.

“Wakati Njiku akitoa maelekezo kwa polisi wenzake, inasemekana mtuhumiwa huyo aliyefyatua risasi iliyomuua askari wetu alikuwa kwenye moja ya madirisha ya nyumba hiyo akiangalia namna askari hao wanavyojipanga nje ya nyumba hiyo na ndipo akamuua,” alisema.

Chanzo hicho kilieleza kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kupiga risasi hizo zilizosababisha kifo cha askari huyo, majibizano ya risasi kati ya polisi na watuhumiwa wa ujambazi waliokuwamo ndani ya nyumba yalipoanza na polisi kufanikisha kuwaua watu 14.

Pia chanzo hicho kilisema kuwa Jeshila Polisi lilifanikiwa kuwakamata watu watano akiwemo askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ambaye alikuwa mtaalamu wa utunguaji (Sniper).

Jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro hakuwa tayari kuzungumzia lolote kuhusu tukio hilo na aliahidi kuwa leo ndipo ataweka hadharani kilichotokea huko Vikindu.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Hivi ndivyo bosi polisi alivyouawa na majambazi.   Hivi ndivyo bosi polisi alivyouawa na majambazi. Reviewed by Zero Degree on 8/27/2016 10:58:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.