Loading...

Hizi hapa sababu za kutumbuliwa kwa RC- Arusha.

Rais john magufuli akiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda(Picha ya maktaba).
WAKATI Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, na kumteua Mrisho Gambo kushika wadhifa huo, kuungua kwa majengo ya shule na siasa za mkoa huo, zimetajwa kuwa ndiyo miongoni mwa sababu za kutumbuliwa kwake.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu, ilieleza kuwa Rais Magufuli amefanya mabadiliko hayo ya uongozi na kumteua Gambo kuwa Mkuu wa Mkoa huo kuanzia jana.

Ilimnukuu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akieleza kuwa Ntibenda amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na atapangiwa majukumu mengine.

Ntibenda anatakuwa Mkuu wa Mkoa wa tatu kuvuliwa wadhifa huo tangu Rais Magufuli aingie madarakani, Novemba 5, mwaka jana.

Wengine ni Anne Kilango aliyeondolewa Aprili 11, mwaka huu kama Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kutuhumiwa kutoa taarifa zisizo sahihi za watumishi hewa na Magesa Mulongo aliyevuliwa ukuu wa mkoa wa Mara, Juni 27, mwaka huu ingawa sababu hazikuwekwa wazi.

Kabla ya uteuzi huo, Gambo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha na alitarajiwa kuapishwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam.

SABABU ZA KUTUMBULIWA

Ingawa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu haikufafanua sababu za kutumbuliwa kwa Ntibenda, vyanzo vyetu vimedai kuwa kushindwa kwake kuzuia madiwani wa Arusha kujilipa posho kubwa huenda kukawa chanzo.

Bila kuhusisha kilichotokea Arusha, wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam jana, Majaliwa aliwataka madiwani kuacha tabia ya kujilipa posho kubwa tofauti na zilizoidhinishwa.

Alisema madiwani wanapaswa kusimamia mapato katika halmashauri na wahakikishe fedha hizo zinakwenda kufanya maendeleo na si kujipangia posho za kujilipa.

“Madiwani watalipwa kwa mujibu wa malipo yaliyoorodheshwa kwenye nyaraka na si vinginevyo,” alisema.

“Najua madiwani hizo ndiyo zenu. Mnapanga fedha za kujilipa. Uamuzi uwe wenye tija. Nyie mnajilipa, wale je?” alihoji Majaliwa.

Aidha, tetesi zilizokuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii jana zilieleza kuwa kuungua kwa majengo ya shule mkoani Arusha kulihusishwa na kutumbuliwa kwake.

Katika kipindi cha muda mfupi, shule tano zimekumbwa na matukio ya majengo yake kuungua kwa moto mkoani humo.

MBUNGE LEMA

Baadhi ya wakazi jijini hapa, wamepokea kwa hisia tofauti kutenguliwa kwa Ntibenda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na nafasi yake kushikwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema uteuzi wa Gambo una walakini kwa sababu hakuwa amefanya vizuri wakati akiwa mkuu wa wilaya.

“Hajui taratibu, amefanya makosa mengi kinyume cha utaratibu wakati akiwa mkuu wa wilaya, hakustahili kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa,” alisema.

“Alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, (Gambo) nilijua anakuja kuvuruga amani iliyopo, nilijua hiki kinachoendelea…nilijua amekuja kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha. Ndio maana amekuwa akivuruga amani iliyopo,” alisema.

Alisema mapambano dhidi ya Gambo bado yanaendelea.

Kwa muda sasa, Gambo amekuwa akituhumiwa kuingilia kati majukumu, na maamuzi yanayopitishwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Arusha ambalo linaongozwa na Chadema.

Hata hivyo, kwa upande wake Gambo amekuwa akidai kwamba katika suala la maendeleo hakuna kitu siasa na kwamba huduma kwa wananchi hazisubiri maamuzi ya Baraza la Madiwani.

Akizungumzia uteuzi wake, Gambo alisema kwa kifupi anamshukuru Mungu na akaahidi kuchapa kazi na kushirikiana na wananchi katika masuala ya maendeleo.

Kuhusu kutenguliwa kwa Ntibenda, baadhi ya wakazi walidai hatua hiyo imetokana na kushindwa kudhibiti matukio ya uchomaji moto katika shule za sekondari.

“Hajachukua hatua kudhibiti kuendelea kwa matukio ya uchomaji moto shuleni, hivyo anastahili kutumbuliwa,” alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Hadi sasa sekondari tano za serikali zimechomwa moto mkoani hapa kwa mwaka huu.

Credits: Nipashe
ZeroDegree.
Hizi hapa sababu za kutumbuliwa kwa RC- Arusha. Hizi hapa sababu za kutumbuliwa kwa RC- Arusha. Reviewed by Zero Degree on 8/19/2016 08:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.