Loading...

Kivuko cha MV MAGOGONI kuanza kutoa huduma katikati ya mwezi huu.

SERIKALI imesema ukarabati wa kivuko cha Mv Magogoni jijini Dar es Salaam, upo katika hatua za mwisho na ifikapo katikati ya mwezi huu kitaanza tena kutoa huduma.

Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 2000 na magari 60 na kinatoa huduma eneo la Feri na Kigamboni.

Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (anayesimamia ujenzi), Joseph Nyamhanga, aliyasema hayo jana alipotembelea eneo la Mamlaka ya Bandari (TPA) linalojulikana kama ‘Dock Yard’ kuangalia maendeleo ya uundwaji na ukarabati wa vivuko vitatu vya Mv Magogoni (cha zamani) na vivuko vipya vya Mv Magogoni na Mv Tanga.

Nyamhanga alisema ukarabati wa kivuko cha Mv Magogoni (cha zamani), unaendelea vizuri na upo katika hatua za kukamilika hivyo wananchi wataondokana na usumbufu wa usafiri katikati ya mwezi huu.

Aidha, alisema uundwaji wa kivuko kipya cha Mv Magogoni chenye uwezo wa kubeba tani 150, abiria 800 na magari 22, unaendelea vizuri na mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 50 hivyo Oktoba mwaka huu kitakuwa kimekamilika na kuanza kutoa huduma.

“Kituo hiki kipya cha Magogoni kikikamilika katika eneo hili la Kigamboni kutakuwa na vivuko vitatu. Hivyo huduma katika eneo hilo itaboreka zaidi. Hivi sasa Mv Kigamboni ndio inatoa huduma,” alisema.

Katibu Mkuu huyo alisema kivuko hicho cha tatu, kitatoa huduma katika eneo la Pangani, Tanga. Hivi sasa kimeshakamilika na hatua iliyobaki ni ukaguzi wa mwisho wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

Alisema baada ya ukaguzi huo kufanyika, kinatarajiwa kusafirishwa Mto Pangani kutoa huduma. “Pangani kuna kivuko kingine hivyo kwa kuongezeka kivuko kipya huduma za eneo hilo zitaboreka,” alisema.

Alisema ukarabati wa kivuko cha Magogoni umegharimu zaidi ya Sh bilioni 1.1, mkataba wa ujenzi wa kivuko kipya cha Pangani ni gharama ya zaidi ya dola milioni 1.8 na ujenzi wa kivuko kipya cha Magogoni, umegharimu zaidi ya dola za Kimarekani 2.8.

Katibu Mkuu huyo alisema kukamilika kwa miradi hiyo, kutafanya nchi nzima kuwa na vivuko 30, ambapo sasa kuna vivuko 28 hivyo kuboresha zaidi huduma za vivuko katika maeneo hayo.

ZeroDegree.
Kivuko cha MV MAGOGONI kuanza kutoa huduma katikati ya mwezi huu. Kivuko cha MV MAGOGONI kuanza kutoa huduma katikati ya mwezi huu. Reviewed by Zero Degree on 8/05/2016 09:27:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.